ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 18, 2012

Ndoa, mapenzi huundwa na katiba, isome ikusaidie-3

Na Luquman Maloto
Wiki iliyopita kwenye kipengele cha hofu, nilieleza kwamba faida ya hofu kwenye uhusiano ni kuwa kila nukta, dakika, saa na siku, utaishi kwa tahadhari.
Lile ambalo unajua haliwezi kumpendeza mwenzi wako, hutalifanya, hivyo kufanya maelewano kuwa makubwa zaidi.

Husaidia kuepusha migogoro na kuumizana bila sababu za msingi.
Kiburi kimejikita kwenye vichwa vya watu wengi, hivyo kufanya hata yale ambayo wapenzi wao hawataki.
Mathalan, mtu anaweza kutambua kuwa nikivaa nguo za aina fulani, mpenzi wake hawezi kufurahi lakini kwa sababu ya kutokuwa na hofu, anavaa na kuibua ugomvi usio wa lazima.
Mtu anajua fika kwamba mwenzi wake hapendelei tabia ya kutembea usiku lakini kwa sababu ya kiburi, unasaga rumba mpaka usiku wa manane ndiyo unarudi nyumbani.
Ni kutafuta shari, hiyo ni tabia ya kutopenda amani na mwenzi wako. Sisemi uogope, ila unatakiwa uwe na hofu kutoka moyoni.
Kila jambo linalotokea, hebu jiulize mara mbili mpaka tatu. Ukiona ni zito, jipe muda zaidi wa kutafakari kabla hujapata uamuzi sahihi. Inawezekana ukalichulia ni dogo, kumbe mwenzako akalitafsiri kwa undani zaidi, mwisho akaona muachane kwa sababu amehisi unamdharau.
Zingatia kwamba kufanya jambo la kumkera mpenzi wako kwa makusudi ni dharau.
Kama mchambuzi wa masuala ya mapenzi, nimegundua baada ya utafiti wake kuwa asilimia kubwa ya migogoro kwenye mapenzi hutokea kwa sababu ya wawili wanaoamua kupendana kukosa hofu.
Hoja hapa ni kwamba ukiishi kwa kujiamini kupita kiasi mbele ya mwenzi wako ni janga. Ni sawa na kuuweka uhusiano wenu hewani.
Sina maana kuwa watu wasijiamini, mantiki ni kwamba kila mmoja ajipe hofu kwenye matendo yake ili asimkere mwenzake.
Ajue kuwa dogo linaweza kuhatarisha mapenzi, kwa hiyo hatakiwi kuthubutu kutenda.
Uhusiano wa kimapenzi, huunganisha pande mbili zenye matarajio ya furaha, kwa hiyo ni vizuri kuishi kwa kuheshimu matarajio hayo.
UAMINIFU
Kifungu hiki kina vifungu vidogo viwili.
Mosi: Uaminifu binafsi. Yaani mhusika anakuwa anasukumwa kutorahisi mwili wake kutumika kiholela kutokana na kulinda heshima yake.
Hii ina maana ya nidhamu binafsi. Nitoe msisitizo kwamba mwenzi bora wa maisha ni yule anayejitunza kwa nidhamu binafsi. Nidhamu ya woga inasaidia lakini si nzuri sana.
Pili: Ni uaminifu unaotokana na hofu.
Mtu anakutana na vishawishi vya hapa na pale lakini anaogopa kuingia kwenye uhusiano wa pili kwa sababu ya hofu aliyonayo kutokana na macho ya jamii inayomzunguka.
Anajua watu wakijua watamuona mhuni (malaya), anataka aheshimike, kwa hiyo anabaki na uaminifu wake wa woga.
Katika kipengele hicho cha woga, anaweza pia kuogopa kusaliti kwa sababu anajua za mwizi ni arobaini. Anatambua kwamba ipo siku mwenzi wake atajua na kuanzia hapo penzi litakufa.
Naye hataki uhusiano wake ufe, kwa hiyo anajilinda, ingawa ndani yake kunakuwa na msukumo wa kuanzisha figa la pili na tatu. Hata huu nao ni uaminifu.
Ogopa mno mwenzi ambaye haoni cha kupoteza.
Huyo anaweza kukufanyia jambo baya wakati wowote.
Anaweza kuanzisha uhusiano mwingine katika kipindi ambacho bado unamhitaji. Anaweza kukuacha na asijali maumivu yako. Hivyo basi, tazama uendako, mtathmini mwenzio kama ana sifa zinazofaa kisha amua kwa faida yako mwenyewe.
HESHIMA
Unahitaji mpenzi ambaye anajiheshimu. Weka akilini hilo halafu lifanye kuwa muongozo wa maisha yako ya kimapenzi. Heshima ina matawi mengi lakini muhimu kwako ni kuwa lazima awe anakidhi vipengele vyote.
Wengi wanateswa na mapenzi leo hii kwa sababu hawakuzingatia kipengele cha heshima wakati wanaamua kuhusu hatma ya uhusiano wao.
Lazima awe anajiheshimu. Nalilisisitiza hilo kwa mara ya pili kwa sababu kama hana heshima binafsi, maana yake hatakuwa nayo ya kumpa mwingine.
Watu wanaojiheshimu ndiyo haohao huwaheshimu wengine.
Nakuomba ulizingatie hilo kwa umakini mkubwa kwa sababu huamua furaha ya wapenzi, wachumba na hata wanandoa.
Mtu asiyejiheshimu anaweza kufanya jambo lolote na wakati wowote.
Anaweza pia kutoheshimu umuhimu wa mwenzi wake.
Tia akilini kuwa mtu asiyejiheshimu huwa hana soni mbele ya macho ya jamii. Anaweza kugombana na watu sehemu yoyote hata ukweni kwake.
Anaweza kuvaa nguo za ‘kishenzi’ ambazo zitamuacha kwenye aibu mwenzi wake.
Yeye hawezi kuona aibu, kwani hajiheshimu. Binadamu wengi hujipa mizigo mibaya kwa kuzoa watu ambao hawajui kujistahi, mwisho wanapata tabu kuwarekebisha. Wanasema, samaki mkunje angali mbichi, sasa wazazi na familia yake, walishindwa kumuweka sawa, wewe utawezaje wakati ameshakubuhu? Tia akilini.
Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

No comments: