ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 18, 2012

Sefue- Nitatumia uwezo wangu kumsaidia Rais

Mhe. Balozi Ombeni Sefue
BALOZI wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Ombeni Sefue amesema amejipanga vema kumsaidia Rais Jakaya Kikwete na serikali kwa ujumla kupitia wadhifa wake mpya wa Katibu Mkuu Kiongozi. 

“Ninatambua dhamana hii ni kubwa, nzito na yenye changamoto nyingi, lakini nimejipanga kutumia uwezo wangu, maarifa yangu na ujuzi wangu wote kumsaidia Rais na Serikali kwa ujumla na nimejipanga kuzikabili changamoto zinazoambatana na dhamana hiyo,” alisema. 

Balozi Sefue alisema hayo wakati wa hafla fupi ya kumuaga na kumpongeza kwa wadhifa wake huo mpya, hafla iliyoandaliwa na Jumuiya ya Watanzania waishio jijini New York na vitongoji vyake. 

Katika hafla hiyo, Balozi Sefue licha ya kuwahakikishia Watanzania hao kwamba amejipanga vema katika jukumu lake hilo jipya, lakini pia aliwashukuru kwa kutenga muda wao kuagana naye. 

Katika mazungumzo yake na Watanzania hao, Balozi Sefue alisisitiza umuhimu wa kuzidumisha na kuziendeleza sifa ambazo zimeifanya Tanzania kuwa moja kati ya nchi zinazoheshimika Barani Afrika. 

Alizitaja sifa hizo kuwa ni umoja, mshikamano, upendo na kutobaguana kwa misingi ya dini, rangi, kabila au jinsia. 

Akisisitiza umuhimu wa kusaidiana, Balozi Sefue alisema Watanzania wataweza kusaidiana pale tu watakapokuwa na Jumuiya inayowaunganisha. 

Balozi Sefue aliwataka kuienzi na kuendelea kuiimarisha Jumuiya yao ambayo yeye, licha ya kuwa mlezi wao lakini aliwasaidia sana kwa ushauri na mawazo yaliyopelekea kuanzishwa kwa Jumuiya ya Watanzania New York na vitongoji yake. 

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Hajji na Katibu wake Shaaban Musemba wakizungumza kwa nyakati tofauti walimhakikishia Balozi Sefue kwamba kama sehemu ya kuenzi mchango wake watahakikisha jumuiya yao haifi. 

Walisema katika kipindi kifupi ambacho Balozi amekuwa mlezi wa jumuia hiyo, wamejifunza mengi kutoka kwake na kwamba wanasikitika watakosa mchango wake wa mawazo, ushauri na mwongozo.

No comments: