ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, February 18, 2012

Yanga hawaponi leo, Zamalek yatamba

Timu ya Zamalek ikiwa kwenye mazoezi mepezi jana Ijumaa February 17, 2012 uwanja wa Taifa.
(Picha kwa hisani ya Michuzi)
Licha ya kusema kwamba wanaifahamu Yanga kuwa ni timu nzuri, kocha msaidizi Ossam Nabil wa klabu ya Zamalek ya Misri amesema kuwa wamekuja na kikosi chao kamili na kwamba ni lazima washinde katika mechi yao ya leo.

Itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ili wajiwekee mazingira mazuri ya kutwaa taji la mwaka huu la Ligi ya Klabu Bingwa Afrika.
Akizungumza kwa niaba ya kocha mkuu Hassan Shehata wakati wa mkutano na waandishi wa habari jana, Nabil alisema kuwa wamejiandaa kuonyesha soka safi na kuibuka na ushindi wa kuvutia dhidi ya wenyeji.
"Tunaijua Yanga ni timu nzuri na kwamba, ni lazima watakuwa wamejiandaa vya kutosha kwa ajili ya mechi hii… lakini na sisi tumejiandaa vizuri sana kwa sababu mwaka huu tumedhamiria kutwaa ubingwa wa Afrika tulioukosa kwa muda mrefu sasa," alisema Nabil.
Alisema kuwa kwenye msafara wao, hawajaongozana na mashabiki lakini wanaamini kwamba mashabiki wa Tanzania watafurahia soka watakaloonyesha na hivyo baadhi yao watajikuta wakiwashangilia.
Aliongeza kuwa kikosi nchake kina wachezaji wawili tu wa kigeni, ambao ni Mcameroon Alex Mundomo na Razaq Thomas ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Benin.
Akizungumzia mechi hiyo, kocha wa Yanga, Mserbia Kostadian Papic, alisema kuwa wamejiandaa kufanya vizuri licha ya kwamba leo watawakosa viungo Nurdin Bakari na Rashid Gumbo, kipa Mghana Yaw Berko na beki Salum Telela wanaosumbuliwa na mjeraha.
"Tuko tayari kwa mechi hii. Naamini tutafanya vizuri kwa sababu lengo letu ni kushinda," alisema Papic.
Papic alisema kuwa pamoja na kukutana na timu nyingi za Afrika akiwa na timu mbalimbali kama Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na Enyimba ya Nigeria, leo itakuwa ni mara yake ya kwanza kuikabili Zamalek.
Alisema kuwa atatumia uzoefu wake kuhakikisha kwamba kikosi chake kinacheza vizuri na kushinda mechi hiyo ili kuwapa raha mashabiki wao.
NSAJIGWA ‘FUSO’
Nahodha wa Yanga, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’, alisema kuwa wanafahamu Zamalek ni timu ngumu, lakini wamejiandaa vyema kuhakikisha kwamba wanapata ushindi na hivyo mashabiki wajitokeze ili kuwaunga mkono.
"Tunaomba mashabiki waje kutushangilia kwa wingi, tunajua hii ni timu kubwa Afrika, lakini na sisi tunataka kuwaonyesha kuwa kuna timu inaitwa Yanga, tunaomba mashabiki waje uwanjani kutuunga mkono," alisema Nsajigwa.
Nsajigwa hakutaka kutabiri matokeo, lakini aliwahakikishia mashabiki kuwa watacheza kwa nguvu zao zote ili kupata matokeo mazuri ya nyumbani kabla ya kurudiana na ‘waarabu’ hao jijini Cairo, Misri kati ya Machi 2 na 4.
Mechi hiyo itaanza saa 10:00 jioni ambapo milango ya uwanja itakuwa wazi kuanzia saa 3:00 asubuhi.
CHANZO: NIPASHE

No comments: