KATIKA makala haya ambayo naendelea kuchambua katiba katika maisha ya uhusiano wa kimapenzi na ndoa, nilieleza kwamba unahitaji mpenzi ambaye anajiheshimu. Weka akilini hilo halafu lifanye kuwa mwongozo wa maisha yako ya kimapenzi.
Heshima ina matawi mengi lakini muhimu kwako ni kuwa lazima awe anakidhi vipengele vyote. Wengi wanateswa na mapenzi leo hii kwa sababu hawakuzingatia kipengele cha heshima wakati wanaamua kuhusu hatma ya uhusiano wako.
Lazima awe anajiheshimu. Nalisisitiza hilo kwa mara pili kwa sababu kama hana heshima binafsi, maana yake hatakuwa nayo ya kumpa mwingine. Watu wanaojiheshimu ndiyo haohao huwaheshimu wengine. Nakuomba ulizingatie hili kwa umakini mkubwa kwa sababu huamua furaha ya wapenzi, wachumba na hata wanandoa.
Mtu asiyejiheshimu anaweza kufanya jambo lolote kwa wakati wowote. Anaweza pia kutoheshimu umuhimu wa mwenzi wake. Tia akilini kuwa mtu asiyejiheshimu huwa hana soni mbele ya macho ya jamii. Anaweza kugombana na watu sehemu yoyote hata ukweni. Anaweza kuvaa nguo za ‘kishenzi’ ambazo zitamuacha kwenye aibu mwenzi wake.
Yeye hawezi kuona aibu, kwani hajiheshimu. Binadamu wengi hujipa mizigo mibaya kwa kuzoa watu ambao hawajui kujistahi, mwisho wanapata tabu kuwarekebisha. Wanasema, samaki mkunje angali mbichi, sasa wazazi wake na familia yake, walishindwa kumuweka sawa, wewe utawezaje wakati ameshakubuhu? Tia akilini.
FURAHA ITIMIZWE PANDE ZOTE
Watu wengi wamekuwa wakishindwa kustawisha uhusiano wao kwa sababu wanashindwa kuishi ndani ya wenzao. Wanatenda mambo ambayo yanawaumiza wenzi wao bila kujiuliza. Hawana malengo chanya!
Mtu mwenye malengo mazuri katika mapenzi ni yule ambaye anajiuliza kabla ya kuzungumza au kutenda. Anatafakari kauli au kitendo na matokeo yake. Pointi kuu ni mapokeo ya mwenzi wake. Ni kosa kufanya tukio lolote au kutoa matamshi yanayoweza kumuudhi mwenzako.
Ni lazima uwe na angalizo kwamba kwako linaweza kuwa dogo lakini kwa mwenzako ni kubwa. Heshimu kosa lolote kwamba linaweza kuhatarisha uhusiano wako, kwa hiyo jichunge kila eneo.
Wewe ni mtu tu duniani, inawezekana uzito wako ni mdogo. Ukiwepo au usipokuwepo taifa halisomi upungufu wowote! Hata hivyo, kupitia mapenzi wewe ni dunia mbele ya mwenzi wako. Kila kitu hakina thamani kwake bila uwepo wako, kwa hiyo heshimu hisia zake, ingia gharama kumletea furaha.
Nimeeleza hapo juu kuwa mfumo sahihi wa mapenzi ni kuishi ndani ya mwenzako. Yaani kuzijulia hisia zake na kujenga nidhamu ya kuepuka kumpa maumivu yasiyo na sababu. Unaelewa kuwa mwenzako hapendi uchelewe kurudi nyumbani, kwa hiyo usifanye makusudi mitaani.
Ni kweli unapenda kuketi na wafanyakazi wenzako au marafiki mkipata za moto na baridi baada ya kazi. Lakini wakati unatekeleza hilo, kwa kila hatua jiulize, je, hicho ndicho ambacho mwenzi wako anakihitaji? Kama ndiyo basi fanya, ikiwa jibu ni kinyume chake, changamsha miguu umuwahi nyumbani.
Jiulize: Kuna sababu gani ya kugandana na marafiki mitaani wakati mwenzako amenuna nyumbani? Jiongeze lingine: Mtakapokuwa ‘mnaparurana’ nyumbani, hao unaowaendekeza watakuwepo? Pengine wakati wao wanalala usingizi mzuri, wewe kwako hakulaliki.
Tafakari: Kuna mambo mengi ambayo mnachangia pamoja, ulimwengu ambao unapita naye ni usiku wa giza kwa wengine. Hulioni kama hilo ni maalum? Tambua thamani ya mwenzi wako, hivyo tekeleza furaha yake na umtimizie kwa vipimo sahihi.
Furaha ya mpenzi wako ni gharama, kwa hiyo unahitaji kujipanga ili kumtimizia. Katika uhusiano wa kimapenzi, hauna cha kupoteza kwa kugharamia amani na furaha ya mpenzi wako. Umegundua kwamba ili mwenzio awe sawa ni lazima uende Zanzibar, uwezo upo fanya hivyo!
Tafsiri yake ni kuwa unatakiwa kufanya kila linalowezekana ili mpenzi wako awe na furaha. Sifa ya ubabe na kupuuza hisia za mwenzi wako haina maana. Ukimpuuza leo, maana yake unataka kesho akupuuze. Akikutenda wewe utafurahi? Usingoje msemo wa mkuki kwa nguruwe ukufike!
Zipo hasara nyingi ambazo unaweza kukutana nazo endapo utashindwa kugharamia furaha ya mwenzi wako. Hii ina maana kuwa ni vema unisome vizuri ili ujifunze.
Itaendelea.
www.globalpublishers.info.
No comments:
Post a Comment