ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 3, 2012

Nusu wafeli mtihani kidato cha pili nchini

Fredy Azzah
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha pili ambayo yanaonyesha kuwa watahiniwa 228,759 kati ya 419,040 waliofanya mtihani huo mwaka jana 2011, wameshindwa.Idadi hiyo ya watahiniwa walioshindwa, ni sawa na asilimia 54.59 ya watahiniwa wote waliofanya mtihani huo ambao pia umeonyesha kuwa wanafunzi wengi wameshindwa kufaulu masomo ya Hisabati ,Fizikia na Kemia.
Matokeo ya Mtihani huo ambayo Mwananchi imeyapata jana, yanaonyesha kuwa ufaulu wa mwaka jana umeshuka kwa silimia 16.38 ikilinganishwa na mwaka juzi wakati ufaulu uliopokuwa asilimia 61.78.Kwa mujibu wa matokeo hayo, wanafunzi walionekana kufanya vizuri zaidi katika masomo ya  Kiswahili, Historia na Uraia.

“Watahiniwa 228,759 ( 54.59%) wakiwemo wasichana 115,983 na wavulana 112,776, hawakufaulu mtihani wa kidato cha pili mwaka jana na walioshindwa mwaka 2010 ni watahiniwa 171,395 sawa na asilimia 38.20,” ilisema taarifa ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Ukaguzi Shule wa Wizara hiyo, Hidaya Mohamed.
Matokeo hayo yanaonyesha kwamba, watahiniwa waliofaulu ni 190,259 sawa na asilimia 45.40; kati yao wasichana ni 77,366 na wavulana 112,893.

“Watahiniwa waliofaulu kwa kiwango cha alama A, B na C walikuwa 94,462  (22.5%) na kiwango cha D ni 95,797 (22.9%),” ilifafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Shule 10 bora
Taarifa hiyo imetaja shule za Serikali zilizoshika nafasi 10 za juu kuwa ni Iliboru, Mzumbe, Tabora Wavulana, Kibaha, Iyunga, Jana, Shishiyu, Mbeya, Kilakala na Tanga Ufundi.
Shule zisizokuwa za Serikali zilizoongoza ni  St. Francis, Kaizirege, Carmel, Marian Wavulana, Queen of Apostles, Thomas More, Mwanza Alliance, Marian Wasichana, St. Amedeus na Anwarite.

Shule 10 za mwisho
Kwa mujibu wa matokeo hayo, shule 10 za Serikali zilizoshika nafasi ya mwisho ni Vugiri, Barabarani, Ighombwe, Milina, Miruli, Nangaru, Maskati, Serya, Likawage na Makata.
Taarifa imeonyesha pia shule 10 zisizokuwa za Serikali zilifanya vibaya kuwa ni Mbonea, Mfuru, Temeke Muslim,  Bishop Kisula,  Ummu-Saalam, Doreta, Nkuhungu, City, Rumanyika na Kigurunyembe.

Matokeo yazuiliwa
Taarifa hiyo pia ilifafanua kwamba, watahiniwa 22 matokeo yao yamezuiliwa kutokana na tuhuma za udanganyifu, idadi ambayo kwa mwaka huu imepungua ikilinganishwa na mwaka 2010 kulipokuwa na watahiniwa 64 waliofutiwa matokeo.
Taarifa hiyo ilibanisha kwamba watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani huo ni 466,567; wasichana 212,235 na wavulana 254,332.

Hata hivyo, watahiniwa 419,040  ambayo ni sawa na asilimia 89.81 yenye jumla ya wasichana 193,357 na wavulana 225,683, ndio waliofanya mtihani huo.

“Watahiniwa 47,527 (10.19%) hawakufanya mtihani,  wasichana wakiwa ni 18,878 na wavulana 28,649 kwa sababu mbalimbali, mojawapo ikiwa ni utoro,” iliongeza sehemu ya taarifa hiyo.
Wizara katika taarifa hiyo ilifafanua zaidi kwamba, “Kushuka kwa ufaulu kumeenda sambamba na ongezeko la watahiniwa wasiofanya mtihani huu.”

Mipango ya baadaye
Katika hatua nyingine, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imesema kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha mazingira ya utoaji elimu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maabara za sayansi.

Taarifa hiyo imetaja vitu vingine vitakavyoboreshwa kuwa ni mafunzo ya kujenga uwezo wa walimu na ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia..

Agizo la Wizara
Taarifa hiyo ilisisitiza, “Wizara inaagiza wadau wote wa elimu kanda, manispaa na halmashauri za wilaya, kuhakikisha kuwa wanafunzi wote walioshindwa kufikia wastani wa asilimia 30 katika mtihani wa kidato cha pili mwaka 2011, wapatiwe mafunzo rekebishi ili waweze kuendelea vema na masomo yao ya kidato cha tatu na nne.”

Kurejeshwa kwa ufaulu wa lazima
Baada ya malalamiko ya muda mrefu ya kushuka kwa ufaulu wa kidato cha pili na nne, mwaka huu Serikali ilitangaza  kurudisha makali ya mtihani wa kidato cha pili ambao wanafunzi watakaopata chini ya asilimia 30 ya masomo yao yote kuanzia mwaka 2012, watakariri kidato cha pili.

Wakosoaji wa mpango wa awali wa kuondoa utaratibu wa kukariri darasa kwa wanafunzi wanaoshindwa mtihani huo wa kidato cha pili, walisema  wimbi la wanafunzi wanaofeli mtihani huo  kuruhusiwa kuingia kidato cha nne, ni moja ya sababu iliyochangia kushusha kwa kasi ya ufaulu wa kidato cha nne.

Mwananchi

No comments: