Waziri Nahodha alisema uchunguzi umekwisha kuanza
Hata hivyo ang`ang`ania taarifa haitawekwa hadharani Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha, baada ya kukwepa kwa muda mrefu kujibu utata uliopo nchini kuhusu ugonjwa wa Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kwamba kuugua kwake kumetokana na kulishwa sumu, hatimaye amesema Jeshi la Polisi limeanza kufanya uchunguzi wa madai hayo ili kupata uhakika kama yana ukweli.
Nahodha aliweka wazi jana kufanyika kwa uchunguzi huo baada waandishi wa habari mkoani Mbeya kutaka kujua kutoka kwake kama Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imefanya uchunguzi wa madai ya kwamba Dk. Mwakyembe, ambaye pia ni mbunge wa Kyela, mkoani Mbeya alilishwa sumu na wamebaini nini.
Alisema suala hilo uchunguzi wake unaendelea kufanywa na Jeshi la Polisi na kwamba hata utakapokamilika suala hilo halitawekwa wazi haraka haraka kama baadhi ya watu wanavyotaka, mpaka itakapolazimu kufanya hivyo kwa sababu hilo ni jambo kubwa.
“Suala hili tunaendelea kulitafiti, lakini masuala yanayohusu haki za watu makubwa kama haya tafiti hazifanywi kwa kupitia vyombo vya habari. Hata tukichunguza hatutasema tumeona nini mpaka hapo itakapobidi, lakini kama mnataka taarifa za haraka mwiteni mhusika mwenyewe (Dk. Mwakyembe) halafu muulizeni nani alimpa sumu,” alisema Waziri Nahodha.
Nahodha ambaye amekuwa akikwepa kujibu suala hilo, alisema wananchi lazima watambue kuwa kazi ya Jeshi la Polisi siyo kupiga ramli na yeye kama Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kazi yake kubwa ni kusimamia sheria kama zimetekelezwa na kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia vinatekelezwa.
Alisema kama mtu ana malalamiko juu ya kuhatarishwa usalama wa maisha yake, Jeshi la Polisi linapelekewa taarifa na hapo hatua zinaanza kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.
“Kama kuna mtu anakudai kama hukuja kwangu kuniambia namdai mtu fulani unabaki kulalamika huko pembeni sasa unadhani nitafanyeje?” alihoji Nahodha.
Alisema kazi ya dola kushughulikia mambo magumu kama ya kijinai ni kuchunguza na kuchukua hatua. “Lakini ili hatua ziweze kuchukuliwa vizuri, ni lazima awepo mtuhumiwa na mtuhumu na anayetuhumu ni lazima aseme yule aliyemlisha nanihii ni mtu fulani na hiyo itasaidia na kurahisisha kazi, vinginevyo itakuwa polisi tunapiga ramli,” alisema.
“Polisi utafiti wao unakuwa unafanikiwa zaidi raia wanaposaidia kutoa ushahidi, inaweza kuna hoja kweli labda Dk. Mwakyembe kalishwa sumu, lakini aliyefanya hivyo ni nani ndiyo mtu akileta ushahidi hatua ya pili inaanza ambayo ni kuchukua hatua,” alisema Nahodha bila kueleza kama kuna ushahidi umeshawasilishwa kuhusiana na madai ya Dk. Mwakyembe kulishwa sumu.
Nahodha aliongeza kuwa suala linalohusu afya ya mtu na tiba yake ni vizuri akaulizwa mwenyewe kwani hata Waziri wa Afya hawezi kutoa siri ya mteja wake kwani maadili ya kazi za udaktari hayaruhusu kufanya hivyo.
Dk. Mwakyembe alianza kuugua mwishoni mwa mwaka jana kwa kuvimba mwili mzima, ngozi kugeuka na kuwa na magamba, nywele kunyonyoka kisha akakimbizwa matibabuni India, ambako alikaa kwa takribani miezi mitatu.
Tangu arejee nchini mwishoni mwa mwaka jana, Dk. Mwakyembe amekuwa haonekani hadharani. Alipata kuzungumza na vyombo vya habari vya IPP nyumbani kwake Kunduchi, kabla ya kuibukia kanisani Jumapili iliyopita na kusema; “tumshukuru Mungu shetani ameshindwa.”
Alitoa kauli hiyo katika ibada ya kumshukuru Mungu iliyofanyika usharika wa KKKT Kunduchi na baadaye ibada ya kuombea nchi iliyofanyika viwanja wa Tanganyika Parkers siku hiyo hiyo.
Miongoni mwa watu ambao wamekuwa hawatafuni maneno juu ya madai ya Dk. Mwakyembe kulishwa sumu ni pamoja na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta. Sitta ametangaza wazi kuwa Mwakyembe alilishwa sumu na kutaka Wizara ya Mambo ya Ndani kufanya uchunguzi wa suala hilo.
PANGUA MAOFISA UHAMIAJI YAIVA
Akizungumzia ahadi aliyoitoa ya kufanya mabadiliko ya maafisa uhamiaji, Nahodha alisema utekelezaji wake umeanza na barua zitaanza kusambazwa kwa watakaokumbwa na mabadiliko hayo wiki hii na kwamba kufika Jumatatu ijayo kazi itakuwa imekamilika.
“Unapoingia kwenye nyumba mpya ambayo umeitengeneza vizuri ina mwanga mzuri sasa si utabidi utafute na viti vizuri vinavyoendana na rangi ambayo umeipaka, kwa hiyo kwa kuwa mimi ndiyo nipo kwenye wizara hii natafuta watu ambao wataendana na falsafa yangu ya weledi ninayoitaka mimi,” alisema.
Alisema alipoapishwa na Rais Jakaya Kikwete, aliahidi mambo makuu mawili ambayo ni kusimamia weledi na maslahi ya watumishi wa taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo, kwa hiyo katika suala la weledi watendaji ambao hawatekelezi kazi vizuri wanaondolewa na kuwekwa wengine.
Alisema katika kipindi cha wiki mbili zilizopita ofisa mmoja wa Mkoa wa Tanga amehamishwa na kupelekwa makao makuu ya Uhamiaji akapewe uzoefu wa utendaji kazi kwa sababu kasi yake katika kusimamia masuala la wahamiaji haramu katika mkoa aliokuwa ilikuwa hairidhishi.
“Kimsingi kazi yangu ya kufanya mabadiliko nimeshaimaliza pale wizarani, tayari barua nimeambiwa wanaanza kuzitoa wiki hii. Mpaka Jumatatu kazi hiyo itakuwa imekamilika kwa barua kusambazwa kwa wahusika watakaokubwa na uhamisho na Katibu Mkuu amenihakikishia kufanyika kwa zoezi hilo haraka,” alisema Nahodha.
Nahodha alisema katika kufanya mabadiliko hayo ya maofisa uhamiaji amefuata taratibu za kiutawala zinavyotakiwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment