ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 1, 2012

Siri 20 usizozijua za kufurahia mapenzi-2


AFYA yangu ni kielelezo tosha kuwa nimewaandalia kitu kizuri sana kwa ajili ya kupanua mawazo yetu juu ya mambo ya uhusiano na mepenzi. 
Nazungumzia siri ishirini ambazo kama zikitumika vyema, huongeza ladha katika mapenzi, lakini pia mateso na matatizo yatakuwa hayana nafasi kabisa kwa watu wa aina hiyo.
Nilianza wiki iliyopita, lakini kwa uchache sana nilieleza siri mbili za awali, leo tunaendelea na siri nyingine. Rafiki zangu, nawahakikishia kwamba, mara baada ya kumaliza kusoma mada hii, kila kitu kitabadilika.
Mtazamo wako juu ya mapenzi utakuwa mwingine kabisa, huwezi kubabaishwa kamwe. Bila kupoteza muda, rafiki zangu, hebu twende tukaone siri zinazofuata.


3. MPE UHURU
Wengi wanaamini kumbana mpenzi ni njia sahihi ya kumfanya awe mwaminifu, si kweli. Kuna wenye tabia ya kuvizia simu za wenzao na kuzipekua, si utaratibu mzuri. Mpe uhuru, usimbane! Kuonesha kumwamini sana mpenzi wako, kunamfanya naye aishi ndani ya uaminifu.
Kumchunga hakumnyimi kuendelea na mambo yake, sana sana atafanya kwa siri kubwa. Kumpa uhuru, kutamwogopesha, atajua yupo na mwaminifu ndiyo maana hafuatiliwi, hapo utakuwa umechochea naye awe mwaminifu kama wewe. 

4. ACHA PAPARA
Katika hatua za mwanzo kabisa za uhusiano wenu, hutakiwi kuwa na papara katika jambo lolote. Kila kitu kifanywe kwa utaratibu. Huna sababu ya kurukia mambo, hasa makubwa.
Wengi wamekuwa na haraka sana ya kukutana kimwili, haya ni makosa makubwa sana. Haraka ya nini kama unatarajia awe wako wa maisha. Ngoja nikuambie rafiki yangu, unapoanza kuulizia mapema mambo ya faragha, unamfanya mwenzako ashindwe kukuamini.
Kwanza, atahisi wewe upo kwa ajili ya kutaka kujistarehesha tu, lakini pia anaweza kufikiria kwamba unapenda sana mambo ya chumbani. Kumfanya agundue kasoro hiyo ni tatizo kubwa sana kwako. 
Hata hapo baadaye mtakapoingia kwenye ndoa, ni rahisi zaidi kukumbuka mambo ya zamani, kwamba yupo na mtu anayependa sana mambo ya mahaba. Kwa maneno mengine, hata akihisi tu au kusikia kwamba una mtu mwingine pembeni, atapeleka moja kwa moja hisia zake kwenye kuamini moja kwa moja juu ya jambo hilo. 
Papara si jambo jema kabisa kwa mwenzi ambaye unatarajia awe wako wa maisha. Tulia, mchunguze kwanza. Kumbuka unatakiwa kufikiria kuhusu mustakabali wa maisha yako ya baadaye, kama ndivyo, huna haja ya kuharakisha mambo ya mapenzi.

5. JENGA URAFIKI
Ukitaka kutengeneza uhusiano wenye nguvu, basi zingatia zaidi urafiki. Kumfanya mwezi wako rafiki ni silaha kubwa na yenye nguvu katika kuuimarisha uhusiano.
Mwenzi wako anapojiona kama rafiki, anakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumza chochote, ikiwemo matatizo na migongano mbalimbali kama rafiki zaidi.
Hawezi kukuficha siri zake. Atakuwa na wewe muda wote na atakusogeza karibu yake kwa kila kitu. Hata penzi lenu pia litakuwa na nguvu zaidi. Urafiki ni kila kitu ndugu zangu. 
Acha tabia ya kumkaripia mpenzi wako, jenga mazoea ya kujadiliana zaidi kuliko kutumia kauli za ukali. Rafiki zangu, yote hayo niliyoyazungumza yanajengwa na jambo moja tu; urafiki!

6. MSIFIE
Wengine wanaweza kushangazwa na kauli hiyo, lakini nataka kuwaambia kuwa kati ya mambo muhimu kabisa kumfanyia mpenzi wako na kulifanya penzi kuwa jipya ni kumsifia. Unapomwambia mwenzako kauli nzuri za kumbembeleza kuwa yeye ni mzuri, anakuvutia kwa kila hali, unajenga penzi.
Unamfanya anajihisi wa thamani, atajiamini kuwa yeye ni mkamilifu, si kwa watu wanaomzunguka pekee, bali hata wewe ambaye umemchagua na kumfanya awe wako. 
Kama huna utamaduni wa kumsifia mpenzi wako, huu ni wakati wako wa kufanya hivyo kwa lengo la kuzidisha mapenzi na kuyapa nguvu. 

7.  SAIDIA KUKUZA UHUSIANO WENU
Kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha penzi linazidi kukua siku hadi siku. Kwa maana hiyo, wewe kwa nafasi yako unatakiwa kuhakikisha unakuwa mstari wa mbele kukuza uhusiano wenu.
Kuna mambo mengi sana ambayo yakifanyika, yanakuza uhusiano. Vipo vitu vya kufanya, kutoka pamoja ni njia mojawapo ya kukuza uhusiano. Rafiki zangu, mnapokwenda katika matembezi, husaidia kubadilisha mapenzi na kuonekana mapya.
Si lazima kwenda nje ya mji, kikubwa ni kuzingatia mfuko wako. Hata mkienda mahali pa kawaida tu, mkanywa juice na keki, bado ni nafasi nzuri kwenu ya kukuza uhusiano huo.
Kila mmoja ana wajibu wa kufanya hivyo, lakini hutakiwi kumsubiri mwenzako afanye, wewe kwa nafasi yako unatakiwa kuhakikisha unamfanya mwenzi wako afurahie uhusiano wenu. Kufanya hivyo, kutampa deni na yeye la kufanya hivyo kwako.
Bado kuna siri nyingi zimesalia, wiki ijayo tutaendelea. Tukimaliza kumi za kwanza, tutaingia kwenye siri nyingine kumi za mwisho ambazo zitakuwa zinahusu mambo ya ndani zaidi ya ndoa.
 Wiki ijayo si ya kukosa. Ahsanteni sana.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani

1 comment:

Betty said...

Mdau uko sahihi kabisa. Pia kukumbuka kuwa usilopenda kufanyiwa wewe, jua na mwenzako halipendi!!!!