Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, leo ataanza kuhutubia mikutano ya kampeni ya kumnadi mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Arumeru mashariki, Sioi Sumari.
Habari kutoka ndani ya CCM zinaeleza kuwa Lowassa amekigomea chama chake ambacho kilimtaka kutoshiriki kampeni kwa sababu anakabiliwa na kashfa ya Richmond, kwa kuhofia kuwa kufanya hivyo kumgekiathiri chama hicho katika kampeni hizo.
Hata hivyo, pamoja na Lowassa kutotakiwa kusimama katika majukwa ya kampeni, lakini alikataa wakati wa kikao kilichofanyika juzi usiku chini ya Meneja wa Kampeni za CCM, Mwigulu Nchemba.
Habari zinasema kuwa kikao hicho kilifanyika katika kambi ya CCM iliyoko katika Hoteli ya Gateway.
Kumekuwepo na taarifa kuwa ndani ya CCM kuna kundi ambalo limekuwa likipinga Lowassa, ambaye ni Mbunge wa Monduli asisimame katika majukwa ya kampeni za Arumeru Mashariki.
Hata hivyo, kundi linalimuunga mkono limekuwa likisisitiza kuwa ana haki ya kumkampenia Sioi ambaye anamuoa binti yake, Pamela Lowassa.
Waziri chupu chupu
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole Medeye amejikuta katika wakati mgumu katika Jimbo la Arumetu Mashariki mkoani Arusha baada ya kunusurika
kipigo kutoka kwa wananchi wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Chama ChaDemokrasia na Maendeleo (Chadema), alipokutwa akifanya shughuli za chama chake huku akitumia gari la serikali.
Ole Medeye alikumbwa na mkasa huo juzi jioni katika Kijiji cha Shambarai Kata ya Mbuguni kwenye ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), zilizopo karibu na Shule ya Msingi Oldeves ambapo alifika akiwa na shangingi la serikali likiwa na bendera ya Taifa huku likiwa na namba za usajili zinazoonyesha cheo chake cha NWAR.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kwamba gari hilo ndilo lililowashtua wananchi ambao walianza kuulizana sababu za gari la Naibu Waziri kuwa kwenye ofisi za CCM wakati huu wa kampeni.
Naibu Waziri huyo aliongozana Diwani wa Kata ya Mbuguni, Thomas Mollel maarufu kama askofu, Katibu wa CCM kata hiyo, Samia Ndesaulo Kaaya na mjumbe wa kamati ya siasa kwenye kata hiyo, Yahya Hassan pamoja na raia mmoja mwenye asili ya kiasia ambaye anamiliki mashamba makubwa ya Karangai Sugar Estate yaliyopo wilayani Arumeru.
Hata hivyo, waandishi wa habari walipomtafuta kwa nyakati tofauti kujua ukweli wa mkasa huo, Medeye alitoa kauli zenye utata akieleza kwamba alikuwa kwenye shughuli za kiserikali kusuluhisha migogoro ya ardhi na alipotafutwa jana alikanusha kunusurika kupigwa kwa kueleza kwamba alikuwa kwenye mashamba yake wilayani hapa.
Taarifa zinaeleza kwamba Medeye alifanya ziara ya kiserikali katika Jimbo la Arumeru Magharibi ambalo analiwakilisha kama mbunge ambako alisuluhisha mgogoro wa ardhi katika Kata ya Mringarini na alikuwa ameongozana na viongozi kadhaa wa serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Mercy Silla.
Akisimulia tukio hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Hamad Musa Yusuf, alisema wananchi walilazimika kuvamia ofisi hizo, lakini Medeye alikimbilia kwenye ofisi ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Oldeves na kuacha gari lake kwenye ofisi za CCM.
Hata hivyo, alisema ili kuepusha shari, aliwapigia simu polisi ambao walimfuata na kisha walifungua jalada la uchunguzi katika kituo kidogo cha Polisi Kata ya Mbuguni na kuandikiwa RB namba MNG/RB/81/2012.
Alisema jalada la shauri hilo limewasilishwa katika kituo cha Polisi Usa River. Mkuu wa Operesheni ya Polisi katika uchaguzi huu mdogo, Isaya Mngulu, alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, alikanusha kuwepo kwake, lakini alipotajiwa namba ya RB, alisema hana taarifa zake kwa maelezo kwamba alikuwa katika ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha kwenye kikao.
WAWILI WADAIWA KUTEKWA
Kampeni za kuwania ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki, sasa zimeanza kuingia dosari, baada ya Juma Ally (32), mkazi wa Tengeru, kutekwa na watu wanaodhaniwa kuwa wanasiasa na kumwibia gari namba T 563 BTM, kisha kumvua nguo na kumjeruhi katika paji la uso.
Aidha, kijana mwingine anayedaiwa kuwa kada maarufu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Omary Abdul maarufu kwa jina la Omary Matelephoni, mkazi wa Sakina, Mjini Arusha, ametekwa tangu Machi 25 na hadi sasa hajulikani alipo.
Akizungumzia tukio la kwanza, Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Thobias Andengenye, alithibitisha kupokea taarifa za Juma Ally kutekwa na kupigwa na kitu chenye ncha kali katika paji la uso na kujeruhiwa vibaya.
Alisema tukio hilo lilitokea Machi 27, mwaka huu, majira ya saa 2:00 usiku katika eneo la Usa River, ambapo alisema siku hiyo kijana huyo alifuatwa na watu wanne waliokodisha gari hilo na kutaka wapelekwe eneo la Makumira.
“Lakini walipopanda gari hilo kabla ya kufika Makumira, mmojawao alimtaka dereva kusimamisha gari na aliposimama alishitukia anakabwa shingoni na kupigwa na kitu chenye ncha kali kwenye paji la uso na kuumizwa vibaya, kisha kuvuliwa nguo, kuibiwa simu, fedha na gari lake na kumtupa katika korongo,” alisema.
Andengenye alisema wakati tukio hilo linatokea, kijana huyo alipiga kelele na kusababisha kijana mmoja wa eneo la jirani na hapo kuwasha simu yake ya mkononi kama tochi na kusogelea eneo la tukio na alipokaribia aliona gari hilo linaondoka kwa kasi na kutokomea.
Alisema kijana huyo alipofika eneo hilo alishangaa kuona mtu hana nguo na akiwa anatokwa na damu usoni, ndipo alipotoa taarifa kwa wenzake na kumpeleka katika hopsitali ya Wilaya ya Arumeru ya Tengeru ambako amelazwa kwenye wodi ya wanaume.
Akizungumza kwa taabu katika wodi hiyo, alisema siku ya tukio mara baada ya kufika hospitalini hapo, nyuma yao kulikuwa na gari likiwafuatilia aina ya Noah na lilifika hadi hospitalini hapo na kusimama kwa muda bila kushuka mtu na kisha kuondoka.
“Mimi nadhani imenitokea hivi kwa sababu za kisiasa na kwa kuwa nashabikia upinzani, ndio sababu watu wamenifanyia unyama huu,” alisema kwa shida akilalamika shingo kuuma.
Tukio la pili linahusu la mfuasi wa Chadema, Omary Abdul, mkazi wa Sakina, aliyetekwa na watu wanaodhaniwa wanasiasa na hajulikani alipo, limezidi kuzua hofu kwa famili yake.
Mmoja wa marafiki wa karibu wa kada huyo, Chris Mbajo, alisema mara ya mwisho alikuwa naye katika mkutano wa Chadema uliofanyika Machi 25, 2012 mwaka huu viwanja vya Ngaresero Usa River na usiku huo waliachana, lakini kesho yake alipomtafuta kwa simu zake za kiganjani hakumpata .
Hata hivyo, alisema Alhamisi iliyopita rafiki yake huyo aligombana na Makamu Mwenyekiti wa UVCCM, Beno Malisa kwenye ukumbi wa Triple ‘A’ baada ya kumtaka avue nguo za Chadema na ugomvi huo ulisababisha kufika hadi Usalama wa Taifa, ambao walimuita kijana aliyepotea na kutakiwa kuacha ugomvi.
Taarifa zinaeleza kwamba kada huyo wa Chadema aliitwa na Ofisa Usalama wa Taifa mkoani Arusha japokuwa ugomvi ulikuwa kati ya kada wa Chadema na wa CCM.
NIPASHE ilipomtafuta Malisa kwa njia ya simu, alikana kumjua kijanahuyo akieleza kwamba: “Mimi simfahamu mtu huyo kabisa.”
Kwa upande wake, Meneja kampeni wa Chadema, Vincent Nyerere, alisema kuna kikundi cha wahalifu kutoka Musoma na kwamba tayari ametoa taarifa polisi kwa kuwataja kwa majina wahusika, lakini anasikitishwa kuona hakuna hatua zozote zilizochukuliwa huku watu wakitamba kwa kupiga na kuteka watu.
“Hawa watu sio wageni, wengine wana kesi Musoma na wanajulikana na walishawahi kuja kule Igunga na sasa wapo Meru, alafu wanaachwa,” alisema Nyerere.
NAPE AIBUKIA ARUMERU
Katibu wa itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, ameibuka katika kampeni za, akidai mgombea wa Chadema, Joshua Nasari, anamsindikiza mgombea wa CCM, Sioi Sumari.
Alisema hayo wakati akiwasalimia mamia ya wakazi wa eneo la Ambureni Mughalu jana.
“Wale wenzetu walisema nijitokeze jukwaani, sasa nawaambia wasiombe mchezo uishe mapema, tupigane hadi mwisho…lakini hata yule Nassari jina lake liliporudishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kugombea ubunge, kazi yake ni kumsindikiza Sioi, na kazi hiyo itaisha Aprili 1, na sisi tutaenda na Sioi wetu bungeni,” alisema.
MWIGULU NCHEMBA
Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM, Mwigulu Nchemba, amewataka wakazi wa Arumeru Mashariki, kutofanya makosa kumchagua mpinzani kwa madai kuwa wapinzani hawatafanyakitu.
“Mkifanya makosa wapinzani hawatafanya kitu na mkiwauliza watawaeleza serikali iliyopo madarakani ni ya CCM,” alisema na kuongeza: “Ili mkwepe hayo, Aprili Mosi mpelekeni Sioi bungeni kwa sababu serikali iliyopo ni ya CCM na inatekeleza sera za CCM.”
Alidai kuwa wapiga kura wa Arumeru Mashariki wajifunze kutoka kwa wenzao wa Arusha Mjini kwani zamani ilikuwa ikijulikana kama Geneva of Africa, lakini sasa haipo hivyo tena.
SIOI AOMBA KURA
Sioi aliwaomba wampigie kura kwa madai kuwa CCM imeingia mkataba na jimbo hilo wa kuliletea maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano.
Alisema kwa kuwa muda huo bado upo hivyo wamachague yeye kubeba mizigo ya madeni ya kuwaletea maendeleo wakazi hao. “Naomba mniamini, mimi na chama changu tutawaletea maendeleo,” alisema.
Imeandikwa na Restuta James, Cynthia Mwilolezi na Charles Ole Ngereza, Arumeru.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment