ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 30, 2012

Waziri matatani Arumeru

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape Nnauye (kushoto) akimnadi mgombea wa ubunge wa chama hicho katika kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki, Sioi Sumari (katikati) kwenye mkutano uliofanyika katika kijiji cha Ambureni jana. Picha na Edwin Mjwahuzi.
VIJANA WA CHADEMA WAMZINGIRA , AHOJIWA NA POLISI
Waandishi Wetu, Arumeru
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodlucky Ole Medeye juzi usiku aliingia matatani baada ya kutiwa msukosuko na vijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wakimtuhumu kujihusisha na utoaji rushwa kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge zinazoendelea Jimbo la Arumeru Mashariki.
 
Tukio hilo, lilitokea kati ya saa 12:30 jioni na saa 1.20 usiku eneo la Kata ya Mbuguni wilayani Arumeru, pale Naibu Waziri huyo alipokurupushwa na vijana hao, kisha kukimbilia Shule ya Msingi Oldevesi, kabla ya kuokolewa na polisi.
 
Taarifa kwamba Medeye amekamatwa, zilisambaa kwa kasi hali iliyosababisha watu kadhaa kwenda Kituo cha Polisi Usa River kupata taarifa kamili za tukio hilo, lakini ilifahamika kuwa, Naibu waziri huyo hakufikishwa polisi baada ya kutolewa Mbuguni.
 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, alisema walipata taarifa kutoka kwa vijana hao juzi kwamba Naibu Waziri huyo alikuwa anafanya kampeni eneo la Shambarai.
 
Gazeti hili lilipomtafuta Naibu waziri huyo kupata ukweli wa tukio hilo,  alikiri kukumbwa na mkasa huo, lakini alikanusha madai kwamba alikuwa akigawa fedha kwa lengo la kukisaidia Chama Cha Mapinduzi(CCM).
 
Hata hivyo, habari kutoka Mbuguni zilizolifikia Mwananchi, zilidai kuwa Medeye ambaye pia ni Mbunge wa Arumeru Magharibi, alikutwa na mkasa huo alipokuwa kwenye mazungumzo na mmoja wa wamiliki wa mashamba makubwa katika eneo hilo, mwenye asili ya kiasia (jina tunalihifadhi), pamoja na wanawake kadhaa ambao ni wakazi wa kata hiyo.
 
Baadhi ya vijana wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chadema, walimzingira Medeye na kuanza kumhoji sababu za kuwepo eneo hilo  na kugawa fedha kwa lengo la kukisaidia CCM huku akitumia gari la Serikali, hali iliyozua tafrani na kusababisha Naibu Waziri huyo kutimua mbio hadi Shule ya Msingi Oldeves.
 
Wakati wakiendelea kujibizana, mmoja wa vijana hao alimpiga picha Naibu Waziri huyo pamoja na gari hilo lililokuwa na bendera ya taifa, na kwamba kitendo hicho kilimkera kiongozi huyo kiasi cha kutaka kuvunja kamera, hatua iliyochangia kuongeza kwa tafrani hiyo.
 
“Baada ya hali ya hewa kuchafuka, baadhi ya wakereketwa wa CCM walipiga simu Kituo cha Polisi Mbuguni, askari wakafika mara moja na kuondoka na Medeye hadi Kituo cha Polisi Mbuguni," alidai mmoja kati ya mashuhuda wa tukio hilo.

Ilikuwaje?

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema,  Zanzibar,  Hamid Mussa Yusuph, ambaye alikuwa eneo la tukio, alisema wakiwa katika kazi ya kutangaza mikutano ya chama chao juzi, waliona gari la waziri huyo na walipolisogelea, walimkuta akiwa jirani huku akizungumza na  mkulima huyo mwenye asili na kiasia na baadhi ya akina mama.
 
"Sisi tulimhoji anafanya nini jioni katika eneo hilo akiwa na gari la Serikali? Akatujibu ana shughuli zake, hapo yakatokea majibizano, ndipo alikimbia kwenda kujihifadhi Shule la Oldevesi," alisema Yusuph.
 
Alisema kutokana na idadi ya watu kuendelea kuongezeka katika eneo hilo, yeye (Yusuph) aliamua kupiga simu polisi, kuwaarifu na kwamba baada ya muda mfupi, askari walifika na baada ya kumhoji sababu za yeye kuwepo hapo, waliondoka naye.
 
Yusuph alisema baada ya hapo, waliamua kwenda kutoa taarifa polisi na kufungua faili la uchunguzi ambalo lilipewa namba MNG/RB/81/2012 na baadhi ya wanachama waliokuwepo, waliandika maelezo yao.
 
Hata hivyo jana Mkuu wa Operesheni wa Polisi katika uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, Naibu Kamishna, Isaya Mngulu, alisema hakuna jalada lolote lililofunguliwa kuhusu tukio hilo na wala polisi hawajamshikilia Naibu Waziri huyo.
 
Baada ya Mngulu kutajiwa namba ya faili la keshi iliyofunguliwa Mbuguni, alisema: “Mimi sina hiyo taarifa bwana, labda kama ndio hivyo mtafute RCO (Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Arusha) akueleze zaidi”.
 
Aliongeza: "Ninachojua mimi hakuna kesi yoyote ya Naibu Waziri huyo na kama kuna faili limefunguliwa, atafutwe huyo Mkuu wa Upelelezi".
 
Medeye na RPC Arusha
Medeye kwa upande wake, alisema alikutana na vijana hao, akiwa katika shughuli zake za kiofisi jioni na alishangazwa na uvumi kuwa alikuwa akigawa fedha jambo ambalo ni uongo mkubwa.
 
"Hawa vijana wa Chadema ni waongo, mimi nilikuwa katika shughuli zangu za kiofisi, ndipo walipokuja nikashtukia wakinizingira na kuanza kunihoji maswali ambayo si ya msingi," alisema Medeye.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Andengenye alisema: "Naomba uandike ninayokueleza, baada ya kupata habari hizo, tuliwasiliana na Waziri ambaye alituambia kwamba yupo kwenye shughuli za Serikali nasi tukamshauri kuwa asitishe shughuli hizo kwa ajili ya muda kwani tayari ilikuwa ni jioni sana.”

Alisema baada ya maelekezo hayo, Naibu Waziri huyo aliondoka, hivyo habari zilizoenea kuwa aliandikishwa maelezo au kufunguliwa jalada, siyo sahihi.
 
Utekaji washamiri
Wakati huohuo, hali ya amani katika uchaguzi mdogo wa Jimbo  la Arumeru Mashariki sasa ni tata kutokana na kuibuka vitendo vya utekaji wafuasi wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo.
 
Chadema ndiyo wamelalamikia kutekwa kwa makada wake wawili, Omar Abdul ambaye hadi jana alikuwa hajulikani alipo wakati kada mwingine, Juma Ally (32) amelazwa hospitali baada ya kutekwa na kunyang’anywa gari, kisha kutupwa mtoni baada ya jaribio la kumuua kushindikana.
 
Kamanda Andengenye amethibitisha matukio yote mawili ambayo yamekuja kipindi ambacho kimegubikwa na vurugu katika mikutano ya kampeni za CCM na Chadema, huku vijana kadhaa wakiripotiwa kujeruhiwa kwa mapanga na wengine kukamatwa na polisi.
 
Katika tukio la kwanza, Juma ambaye ni mkazi wa Tengeru, juzi alitekwa na watu asiojulikana akiwa na gari lake, kisha kutaka kumuua.  Andengenye alisema tukio hilo lilitokea Machi 27 usiku, wakati watu wanane, walikodi gari la Juma katika eneo la Usar River na kutaka kupelekwa Makumira lakini kabla ya kufika mmoja wao, aliomba kushuka na ghafla watu hao, walianza kumshambulia dereva huyo na kumtupa kwenye korongo.
 
Alisema wakati watu hao, wakimshambulia, kijana huyo alianza kupiga kelele, ndipo walimvua nguo zote na kuchukua simu na fedha kisha kutoweka na gari hilo aina ya Toyota lenye namba za usajili, T563 BTM.
 
 Andengenye aliongeza kuwa kutokana na sauti aliyokua akitoa Juma, mpita njia mmoja aliisikia na kumulika tochi kwenye Korongo hilo ndipo alimwona na kuita watu wengine kusaidiana kumtoa kisha kumkimbiza Hospitali ya Wilaya ya Arumeru iliyopo Tengeru akiwa uchi huku amejeruhiwa vibaya.

Hadi jana Juma alikuwa bado amelazwa. Akizungumza kwa taabu na waandishi wa habari, alisema watu hao kabla ya kumteka na kumpora gari, walimuomba awapeleke eneo la Makumira.
 
Katika tukio lingine, Omar maarufu kama Omar Matelephone, ambaye amekuwa akivalia kanzu iliyoshonwa kwa rangi za bendera ya Chadema, kwa siku nne hadi jana, alikuwa hajulikani alipo ikiwa ni siku mbili tangu alipokwaruzana na Makamu Mwenyekiti wa UVCCM, Benno Malisa katika klabu ya ‘Triple A’ baada ya kiongozi huyo wa UVCCM, kumtaka avue mavazi yake ya Chadema.
 
Tangu Machi 25 Omar alipohudhuria mkutano wa Chadema katika kata ya Songoro, hajaonekana na simu zake zote hazipatikani, pia nyumbani kwake hayupo.
 
Rafiki wa Omar, Christopha Mbajo alisema jana kuwa yangu  walipoachana naye jioni ya Machi 25, hawajamuona hadi jana na simu zake zote hazipatikani.
 
“Hatujui yuko wapi ila tunakumbuka mara ya mwisho aligombana na Malisa na baadaye waliombana msamaha, kisha aliitwa na Ofisa Usalama wa Taifa Mkoa wa Arusha, Suleiman Mombo na kuhojiwa juu ya ugomvi huo,”alisema Mbajo.
 
Akizungumza na Mwananchi jana kwa simu, Malisa alikana kumfahamu Abdul na kueleza kuwa hajawahi kugombana naye katika ukumbi wa ‘Triple A’ uliopo jijini Arusha kama inavyodaiwa.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Meneja Kampeni wa Chadema, Vincent Nyerere, alidai vitendo hivyo vinafanywa na kundi la vijana wa CCM walioletwa kutoka nje ya Arumeru na kwamba polisi wanapaswa kulaumiwa kwa kushindwa kuwadhibiti
 
“Tuliwaambia kuna kundi la vijana linakuja na basi la Manko Express toka Musoma na kwamba wawazuie kwani ni vijana wa vurugu, tukawapa na majina yao lakini wameshindwa kuwadhibiti na sasa wanatishia maisha ya watu!”Alilalamika Nyerere.


Mwananchi

No comments: