Vurugu kubwa zimeibuka katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani wa Kata ya Kiwira, wilayani Rungwe, Mkoa wa Mbeya baina ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha Mapinduzi (CCM), hali iliyosababisha Mbunge wa Viti Maalum kupitia Chadema, Anna Mallack na mwanaye kuonyeshwa bastola na kutishiwa kuuawa.
Tukio hilo ilitokea jana majira ya saa 6:00 mchana nje ya ofisi za Chadema za Kata hiyo, baada ya wanawake watatu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa CCM kuvamia eneo hilo na kuanza kutoa matusi ya nguoni kwa viongozi wa Chadema.
Akizungumza na NIPASHE, Mallack alisema kuwa jana aliondoka mjini Tukuyu kwenda Kiwira kwa ajili ya kuendelea na mikutano ya kampeni na alipitia katika ofisi ya Chadema ya kata hiyo kwa ajili ya kujadiliana na viongozi wenzake kabla ya kuelekea kwenye mikutano ya kampeni.
Alisema baada ya majadiliano hayo, yeye pamoja na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mbeya Mjini, John Mwambigija maarufu kama “Mzee wa Upako” walipanda kwenye gari lake ambalo linaendeshwa na mtoto wake, Philipo Mallack, na kuanza safari kwenda kwenye eneo la mkutano kwa mujibu wa ratiba ya kampeni za chama chake.
Alisema walipoanza safari, hatua chache kutoka kenye ofisi hizo, ghafla waliwaona wanawake watatu waliovalia nguo za CCM ambao walianza kucheza kwa staili ya kufunua nguo zao na kubaki uchi na wakiwatukana matusi ya nguoni, huku wakonyesha ishara ya vidole viwili na kuweka kingine katikati.
Alisema kuwa yeye na Mwambigija hawakupendezwa na hali hiyo, hivyo wakamwamuru dereva kusimamisha gari na wao wakatelemka kwenda kuwakamata wanawake hao.
Mallack alisema kuwa wanawake hao walipoona hivyo walianza kutimua mbio, lakini yeye alifanikiwa kumkamata mmoja, huku wengine wakikimbilia migombani.
Alisema baada ya kumkamata mwanamke huyo, walimpandisha kwenye gari ili kumpeleka kituo cha Polisi, lakini kabla hawajaondoka ghafla yalifika magari matatu ya CCM na waliposimama waliteremka watu waliokuwemo na kuanzisha vurugu, huku wakiwauliza kwa nini wanawakamata watu wao.
“Waliponiuliza kuwa kwa nini tunawakamata watu wao, mimi pia iliwauliza kama wao ndio wanaowatuma kututukana, ndipo mmoja wao alitoa bastola na kunielekezea mimi, Mzee wa Upako na kijana wangu, wakatuambia kuwa anaweza kutuua sasa hivi, kwa kweli nilisikitishwa sana na tukio hilo,” alisema Mallack.
Alisema aliokolewa kutoka kwenye mdomo wa bastola na vijana wa Chadema ambao walikimbila eneo hilo na kuigonga bastola ya mtu huyo ikadondoka chini.
Mbunge huyo aliendelea kusimulia kuwa bastola hiyo ilipoanguka chini vijana walitaka kuikimbilia, lakini mtu huyo aliwahi kuiokota na kukimbilia kwenye gari lake na kuondoka kwa mwendo wa kasi.
Mallack alisema baada ya mtu huyo na wenzake kukimbia, waliwachukua wanawake wawili waliokuwa wakiwatukana na kuwapeleka kituo cha Polisi na kufungua jalada.
Kwa upande wake, Mzee wa Upako alisema alimtambua mtu aliyekuwa na bastola kuwa ni kada wa CCM, (jina tunalihifadhi), ambaye aligombea ubunge katika Jimbo la Rungwe Magharibi mwaka 2010 na kubwagwa kwenye kura za maoni na Mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Profesa David Mwakyusa.
“Nilimtambua kuwa ni (anamtaja jina) kwa sababu alipofika alitoa bastola na kuniuliza kama mimi ndiye Mzee wa Upako, nikamwambia ni mimi akanielekezea bastola na kusema leo (jana) nitamtambua, ndipo alipomwelekezea bastola hiyo na Mheshimiwa Mbunge na kusema kuwa wote tuko chini ya ulinzi,” alisema Mzee wa Upako.
Habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa vijana wa Chadema walitaka kufunga barabara kumsaka kada huyo, lakini ofisa mwandamizi wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Rungwe aliwazuia na kuwaahidi kuwa polisi watashughulikia suala hilo kwa kuwa ni jukumu lao.
NIPASHE lilipowasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, alithibitisha utokea kwa vurugu hizo ingawa alidai kuwa maofisa wa Polisi waliofika eneo la tukio hawakueleza kuwa kulikuwa na tukio la kutishia kwa bastola.
“Ni kweli vurugu zimetokea pale Kiwira na watu wawili wanawake wanashikiliwa na Polisi, lakini tukio la bastola sijaambiwa na ninaendelea na uchunguzi kwani ikibainika hatua za kisheria zitachukuliwa,” alisema Kamanda Nyombi.
Uchaguzi mdogo wa kata hiyo unatarajiwa kufanyika keshokutwa kuziba nafasi ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo, John Mwankenja, aliyeuawa kwa kupigwa risasi mwaka jana.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment