Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Zuberi Kabwe, amesema kuwa hana nia ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama chake katika Uchaguzi wa ndani wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Zitto aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na NIPASHE jijini Mbeya, alikokuwa amekwenda kuongeza nguvu katika kampeni za uchaguzi wa udiwani katika kata ya Kiwira wilayani Rungwe.
Alisema kuwa hana nia ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama hicho kwa sababu anaona timu ya sasa ya uongozi wa chama hicho inatosha na inafaa kuendelea kukiongoza kwa miaka mingine mitano ijayo.
“Sina interest (nia) na sifikirii kama nitagombea uongozi ndani ya chama katika uchaguzi wa ndani wa Chadema mwaka huu, naona timu iliyopo inatosha na inafaa kuendelea kukiongoza chama,” alisema Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini.
Alisema ingawa katika uchaguzi uliopita alijitosa kuwania nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho, lakini safari hii nafsi yake haimtumi kufanya hivyo kwa kuwa ana imani kuwa uongozi wa sasa unastahili kuendelea kuwa madarakani kwa manufaa na maslahi ya chama na Watanzania kwa ujumla.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment