ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 29, 2012

Sababu 4 za wake za watu kutembea na wapangaji wao

Awali ya yote, namshukuru Mungu kwa kunikutanisha nanyi tena kupitia safu hii nikiamini kuwa muwazima na mnaendelea vyema na mishemishe zenu za kila siku.
Mpenzi msomaji wangu, ndoa ni kitu cha kuheshimika sana na wale wanaobahatika kuingia katika maisha hayo, wanafurahi kwa kuwa wanajua kwa kuolewa au kuoa wanapata heshima kubwa mbele ya jamii inayowazunguka.
Leo hii kuna baadhi ya wanawake hawachagui wanaume wa kuwaoa, wanachoangalia ni kwamba awe mwanaume anayeweza kumpa furaha katika maisha yake, mengine yatafuata baadaye.
Cha kushangaza sasa wapo wanawake ambao wamepata bahati ya kuolewa lakini wanaichezea nafasi hiyo kwa kufanya mambo ya ajabu kwa waume zao. Katika siku za hivi karibuni, kumekuwepo na matukio mengi ya wake za watu kuwa na uhusiano na wapangaji wenzao.
Ni mambo ya kusikitisha sana na inafika wakati unaona ni jinsi gani baadhi yetu tunajikosesha heshima kwa kujitakia. Hivi karibuni nilizungumza na kaka mmoja mkazi wa Manzese jijini Dar, jina lake nalihifadhi kwani ni aibu kwake nikilianika.
Anasema: “Mimi nafanya kazi katika kampuni moja ya ulinzi, nimeoa na mke wangu nimeishi naye kwa muda wa miaka 3 sasa ila hatujabahatika kupata mtoto. Sijui kwa nini hatujapata mtoto lakini nilibaki kuamini labda Mungu bado hajapanga.
“Jambo lililoniumiza sana ni la hivi karibuni kupata fununu kuwa mke wangu ana uhusiano na jamaa mmoja ambaye ni mpangaji mwenzangu na nikaambiwa kila nikitoka kwenda kazini mke wangu huwa anaingia chumbani kwa mshikaji na wanafanya mambo.
“Kinachoniuma sasa ni kwamba, wakati najiandaa kuweka mtego niwakamate, juzi mke wangu akaniambia ana mimba. Nampenda sana lakini kwa sasa nimebaki njia panda.”
Hiyo ni sehemu ya maelezo aliyonipa kijana huyo na nimeshamshauri kwa kadiri nilivyoweza lakini nikaona nisiishie hapo, niandike pia kwenye safu hii ili tujifunze kwa pamoja na tuone ni kwa jinsi gani sisi binadamu tunatendeana mambo ya kuumizana.
Kwa ninavyojua mapenzi, hakuna kitu kinachouma kama mke wako kukusaliti tena kwa kutembea na mpangaji mwenzako. Lakini cha kujiuliza ni kwamba, kwa nini mwanamke afikie hatua ya kujivinjari aidha na baba mwenye nyumba au mpangaji wake?
Unaweza kufikiria sana lakini ukakosa jibu kwani ni kitu kisichoingia akilini kabisa. Hata hivyo, nimejaribu kufanya uchunguzi na nikabaini mambo kama manne ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangia wake za watu kutembea na wapangaji.

Mazoea ya kijinga
Kuna mazoea ambayo mke wa mtu akiwa nayo kwa mpangaji mwenzake wa kiume kitakachofuata ni kusaliti. Unaweza kukuta mwanamke mume wake hayupo, aidha yuko safarini au kazini, yeye anaingia kwenye chumba cha mpangaji na wakati mwingine kufikia hatua ya kumpikia. Huku si kujiweka katika mazingira ya kumfanya ahisi wewe ni mke wake?
Ndiyo maana katika hili wanaume wanatakiwa kuwa wakali wanapoona wake zao wanakuwa na mazoea ya kijinga, kujichekesha na kupiga stori zisizoeleweka na wapangaji wenzao wa kiume.

Mavazi ya kimitego
Hili nimekuwa nikilikemea sana na ni moja kati ya sababu ambazo zimekuwa zikiwafanya wake za watu kujikuta wanatembea na wapangaji wao. Inakuwaje? Unakuta mke wa mtu ambaye amejaaliwa kuwa na ‘figa’ anatoka kwenda bafuni akiwa kafunga khanga moja.
Anatoka bafuni kuelekea chumbani kwake huku akiwa amelowa na kuchezesha makalio yake mbele ya wapangaji wa kiume, unadhani nini kitatokea? Katika hali hiyo ni rahisi sana kwa mwanamke huyu kumshawishi mwanaume mkware kumtokea, kwa nini? Kwa kuwa mwanaume huyo ataona ametegwa na kama asipomtokea ataonekana ni ‘mwanaume suruali’.
Kwa maana hiyo mwanaume anatakiwa kuwa mkali sana na mavazi anayovaa mke wake popote anapokuwa. Hata akiwa nyumbani mke wa mtu anatakiwa kuvaa mavazi ya heshima ili kujiepusha na wanaume wakware wanaoweza kumfanya aisaliti ndoa yake.

Tamaa
Kuna wanawake ni wa ajabu sana, hawa ni wale wasioridhika na kile wanachokipata kutoka kwa waume zao. Unakuta mke anapata kila kitu kutoka kwa mumewe lakini bado anakuwa na tamaa za kijinga na kuona penzi la nje ni tamu kuliko analolipata ndani.
Huu ni ulimbukeni uliopitiliza na siku zote wanawake wa sampuli hii ni vigumu sana kudumu kwenye ndoa zao.

Mambo ya ushirikina
Haya mambo yako sana uswahilini, si ya kuamini sana lakini kwa kuwa wapo ambao wamekuwa wakitoa ushuhuda basi si vibaya nalo tukaliweka kwenye uangalizi. Unaweza kukuta mwanaume anamtamani sana mke wa mtu, anachokifanya ni kwenda kwa mganga na kutumia nguvu za giza kumvuta mwanamke huyo.
Hili limeshawahi kutokea. Kuna mke wa mtu aliwahi kunieleza kuwa siku moja mumewe akiwa amesafiri, usiku wa manane alijikuta yuko kwenye chumba cha mpangaji mwenzake wa kiume akiwa kama alivyozaliwa bila kujijua.
Alichoniambia ni kwamba, yeye hakujua alifikaje pale na baada ya kuzinduka yule mwanaume akamwambia awe anampa penzi kwa siri kila atakapojisikia na akikataa atamwambia mumewe. Hayo yanatokea huko uswahilini tunakoishi hivyo kikubwa ni kuwa makini na mifumo ya maisha yetu.
Kwa leo niishie hapo, tukutane tena wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

1 comment:

Anonymous said...

je wanaume wanaotembe na wapangaji wao inakuwaje mbona hujalielezea hilo