WATUMISHI watatu akiwemo dereva wa treni wa Kampuni ya Reli (TRL), wamesimamishwa kazi katika sakata la kusababisha treni ya abiria kusimama porini baada ya kuishiwa mafuta.
Mhandisi wa TRL, Muungani Kaupunda alimwambia Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Athumani Mfutakamba kwamba baada ya tukio hilo, wamesimamishwa wakati uchunguzi ukiendelea.
Bila kutaja majina ya waliosimamishwa, Kaupunda alisema utakapokamilika, taarifa itatolewa. Taarifa hiyo ilitolewa juzi katika mkutano wa Dk. Mfutakamba na wafanyakazi wa karakana ya reli mkoani Tabora.
Ilitokana na agizo lililotolewa na Mfutakamba kwamba wafanyakazi waliosababisha tukio hilo wafukuzwe kazi.
Treni hiyo ya abiria kutoka Mpanda kwenda Tabora usiku wa Machi 23 mwaka huu iliishiwa mafuta katika vituo vya Urambo na Ussoke wilayani Urambo.
Akizungumza na wafanyakazi hao, Dk. Mfutakamba alisema tukio hilo limemkera kwani maisha ya abiria yaliwekwa hatarini posipo sababu za msingi.
Alisema kwamba haiingii akilini treni kuishiwa mafuta njiani wakati bajeti ya mafuta inajulikana.
Alisema ingekuwa bora endapo abiria wangeachwa kwenye kituo na sio porini. Naibu Waziri huyo alisema kitendo kilichofanyika ni cha kinyama na hakikubaliki katika utendaji wa kazi za shirika hilo na kwamba wamejipanga kuhakikisha matatizo kama hayo hayatokei tena.
No comments:
Post a Comment