ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 28, 2012

Vimini, milegezo marufuku CBE

KAMPENI ya kupinga mavazi yasiyo na heshima imeingia katika sura mpya baada ya uongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kampasi ya Dar es Salaam, kubuni sera inayopiga marufuku mavazi yanayokiuka mila na utamaduni wa Mtanzania, vikiwamo vimini, mlegezo na wanaume kusuka nywele. 

Katika sera hiyo iliyoingizwa katika kanuni za maisha ya mwanafunzi shuleni, mwanafunzi atakayekiuka ataadhibiwa ikiwamo kusimamishwa chuo kwa miezi mitatu. 

Adhabu nyingine ni pamoja na kuzuiwa kuingia getini kwa wanaotoka nje ya hosteli na wanaoishi ndani ya eneo la chuo hawatapewa huduma yoyote kama vile kuingia darasani, kantini, maktaba au ofisi yoyote ya chuo. 

Akitangaza uamuzi huo jana Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Athman Ally Ahmed, alisema chuo kimefikia uamuzi huo baada ya kukithiri kwa uvaaji mavazi yasiyo na staha unaofanywa na wanafunzi chuoni hapo hali inayosababisha udhalilishaji wa utu wa wanafunzi ndani na nje ya chuo. 


Mavazi yanayopigwa marufuku kwa wanaume ni pamoja na uvaaji wa suruali au kaptula na kuacha sehemu ya makalio nje, maarufu kama mlegezo, suruali za kiume zilizopasuliwa kama zilizochakaa (jeans), kusuka nywele, kuvaa kofia aina ya kapelo, pama au bosholi darasani na kuvaa hereni. 

Kwa wanawake mavazi yaliyopigwa marufuku ni vimini, suruali hata za jeans zinazobana na blauzi zinazoacha tumbo, kiuno na kifua wazi, na suruali zinazobana bila kitu kingine kinachoziba mapaja. 

CBE pia imepiga marufuku kaptula za kike au suruali fupi za kubana maarufu kama pedopusha na mavazi yanayoonesha mwili wa mwanamke kuanzia kifuani mpaka mapajani. 

Pia imepiga marufuku sketi fupi zinazoacha wazi mapaja wanapokaa na vazi lolote linaloacha sehemu ya nyuma ya kiuno cha mwanamke wazi au linaloacha wazi sehemu ya juu ya nguo ya ndani wakati amekaa. 

Ahmed alionya kuwa, uongozi wa chuo, hautasita kumchukulia hatua mwanafunzi au mfanyakazi yeyote atakayefika chuoni hapo amevaa mavazi yasiyo ya heshima huku ukitoa mwito kwa wananchi kuunga mkono kampeni hiyo yenye manufaa katika kujenga Taifa lenye maadili mazuri. 

Alisema wanafunzi ambao wengi wao ni vijana chuoni hapo wamekuwa mstari wa mbele kuiga kila aina ya vazi kutoka utamaduni wa watu wa Magharibi hali ambayo 
aliielezea kuwa ni ukiukaji wa mila, desturi na utamaduni wa Mtanzania. 

“Mtindo huu wa kuiga utamaduni wa Magharibi bila kuangalia wapi tunakwenda haukubaliki hata kidogo, ukiangalia katika vyuo vingi vya elimu nchini, wanafunzi wamekuwa wakivaa mavazi ya ajabu na yasiyofaa katika maeneo ya chuo,” alisema. 

Makamu Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mafunzo, Bertha Kipillimba, alisisitiza kuwa sera hiyo itahusu pia wafanyakazi wote wa kampasi ya Dar es Salaam na wanafunzi zaidi ya 6,000 wa chuo. 

Mlezi wa Wanafunzi, Faustin China, alifafanua kuwa umefika wakati wanafunzi hao kujitambua huku akisisitiza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakinyoshewa vidole na jamii kuhusu suala la uvaaji na mienendo ya wanafunzi chuoni hapo. 

“Tumesemwa vibaya kwa muda mrefu, hatuwezi kuachia suala hili likaendelea, tunataka wanafunzi wetu wavae vizuri kwa mujibu wa kanuni tulizojiwekea, ili kujenga heshima ya chuo,” alisema. 

Kampeni dhidi ya uvaaji wa mavazi yasiyo na staha, hivi karibuni ilishika kasi katika madhehebu ya dini hasa Kanisa Katoliki ambako walianzisha matumizi ya kaniki maalumu kuvisha wanaovaa vibaya.

No comments: