ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 3, 2012

Agakhan yasitisha kufadhili miradi Zanzibar

Waziri wa Ardhi, Makazi,
Maji na Nishati Zanzibar,
Ali Juma Shamuhuna


Taasisi ya Agakhan imesitisha miradi yake yote iliyokuwa ikifadhili katika sekta mbali mbali Zanzibar.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Zanzibar, Ali Juma Shamuhuna, alipokuwa akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura, Hamza Hassan Juma, katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea Chukwani.
Hata hivyo, Waziri Shamuhuna, alisema hafahamu sababu za taasisi hiyo kusitisha ufadhili wa miradi yake ya maendeleo waliyokuwa wakiidhamini visiwani humo.
Miongoni mwa miradi iliyokuwa ikifadhiliwa na taasisi hiyo ni pamoja na uendelezaji wa eneo la ukanda wa ufukwe wa Forodhani, ukarabati wa majengo ya historia ya Mambo Msige kabla ya kupewa kampuni ya Zamani Zanzibar Kempiski.


Kuhusu lililokuwa jengo la yatima Forodhani, Shamuhuna, alisema kufuatia kuhamishwa yatima waliokuwa wakiishi katika jengo hilo, sasa litageuzwa Makumbusho ya Mambo ya Baharini Afrika Mashariki.
Alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume, kuwa litumike kuanzisha makumbusho hayo.
Hata hivyo, alisema jengo hilo kwa sasa limekondishwa baadhi ya sehemu kwa ajili ya mradi wa mgahawa, lakini hafahamu watu waliokondishwa wanalipa kodi kiasi gani na kuahidi kujibu swala hilo kwa maandishi.
Waziri Shamuhuna alisema  kwamba Wizara inatafuta fedha kwa kuwasiliana na wafadhili ili kulifanyia matengenezo jengo hilo kabla ya kuanzishwa kwa makumbusho hiyo.
Awali mwakilishi huyo alitaka kujua agizo la Rais Karume kutaka jengo hilo kutumika kuanzishwa makumbusho imefikia hatua gani za utekelezaji wake.
CHANZO: NIPASHE

No comments: