Advertisements

Tuesday, April 3, 2012

Wabunge Chadema- Waliotushambulia walitaka kutuua

Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Highness Kiwia (kushoto) na Mbunge wa jimbo la Ukerewe, Salvatory Machemli (kulia) wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada kujeruhiwa na kundi la watu mjini Mwanza. (Picha na Robert Okanda).
WABUNGE wawili wa Chadema wa Ilemela na Ukerewe, Mwanza, wamedai watu waliowashambulia mwishoni mwa wiki jijini Mwanza na kuwajeruhi, walikuwa na nia ya kuwapotezea maisha. 

Aidha, wamedai kwamba wanawatambua kwa sura na majina baadhi yao, hivyo wanaliachia Jeshi la Polisi lifanye uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria dhidi yao. 


Highness Kiwia (Ilemela) na Salvatory Machemli (Ukerewe), wamelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, wakiendelea na matibabu baada ya kupata rufaa Hospitali ya Rufaa Bugando, Mwanza. 

Wabunge hao wanadaiwa kupigwa mapanga, marungu na mawe na watu wanaosadikiwa kukodiwa ili kutekeleza mauaji usiku wa kuamkia juzi, ambako kulifanyika uchaguzi wa udiwani wa Kirumba ambapo chama hicho cha upinzani kilishinda. 

Hata hivyo, Machemli alidai wakati akishambuliwa, alijishikiza mguuni mwa askari Polisi ili amwokoe, lakini askari huyo alijichomoa na kukimbia hatua kadhaa mbele wakati Kiwia akidai kipigo alichopata ni mateso makubwa na simanzi ambayo ilikuwa na lengo la kuutoa uhai wake. 

Wakizungumza kwa awamu wakiwa hospitalini hapo, Kiwia alisema anashukuru amehudumiwa vizuri kwa kupimwa vipimo vyote na sasa anasubiri kipimo cha MRI ambacho kinaangalia usalama wa kichwa. 

Tukio lilivyokuwa Kuhusu mazingira ya tukio, alidai ilikuwa saa sita usiku akiwa kwenye vikao vya ndani vya chama ambapo alitumiwa ujumbe mfupi kwenye simu kuwa katika eneo la Ibanda Mlimani kuna wafuasi wa CCM, wanatoa rushwa. 

Alisema baada ya muda mfupi, mgombea udiwani wake alimwambia yeye amepigiwa simu na kuambiwa hivyo hivyo. Kiwia alisema simu hiyo ilionekana ya mtego, na alimwambia diwani waongozane kuona ukweli ili watoe taarifa Polisi, walipofika eneo hilo walikuta gari aina ya Toyota, Land Cruiser jeupe likiwa na watu wengi likielekea mtaa wa Bujumbura na gari lao likashindwa kupita hivyo kutafuta mahali pa kugeuzia. 

Hata hivyo, alidai wakati wakigeuza, gari lingine jeupe lilifika likiwa na watu wengi na kuwaziba kwa mbele na kukosa pa kupita kwani kulia kuna kilima na kushoto kuna korongo. 

Alisema baada ya hali kuwa hivyo, aliingiwa na shaka na kumpigia Mkuu wa Polisi wa Wilaya simu, akimjulisha kuwa ametekwa huku akiomba msaada na kujibiwa kuwa yuko likizo nyumbani na kuahidi kuwasiliana na wengine ili apate msaada. 

Kiwia alisema alikaa muda mrefu eneo hilo bila msaada huku kundi hilo la watu likitoa maneno ya “tumekukamata, leo (Kiwia) ndio mwisho wako, si umezoea kujidai unapokuwa majukwaani.” 

Alidai wakati akitafakari hali hiyo, alimpigia simu Mkuu wa Polisi wa Kituo ambaye alimwambia ndio kwanza anaingia nyumbani na kudai kuwa gari la askari wa doria haliko karibu liko Bwiru. Akaamua kumpigia rafiki yake Machemli. 

Alisema Machemli alikwenda hadi kituo cha Polisi akiomba askari ili afuatane nao eneo hilo, wakamtaka atangulie na alipofika eneo hilo, akakuta umati mkubwa wa wananchi bila kuwapo askari hata mmoja jambo lililomshangaza. 

Kiwia alidai akiwa amepandisha vioo vya gari lake akisubiri kitakachotokea kwa mwenzake, lilifika gari la Polisi likiwa na askari wanne, watatu wanaume na mmoja mwanamke wakashuka na kushika bunduki zao mkononi wakifuatilia tukio hilo.

“Baada ya hapo kundi lile lilikwenda kwenye gari la Machemli wakalitikisa na wakamtoa kwenye gari na kumpiga hadi akazirai na polisi kumbeba na kumweka kwenye gari lao na kuendelea kusimama wakifuatilia tukio hilo licha ya kelele za kuomba msaada zilizokuwa zikitolewa,” alidai Kiwia. 

Alidai baada ya kuhisi mauti yamemfika Machemli, kundi lile lilihamia kwa Kiwia likamshusha kwenye gari baada ya kuvunja kioo na kumpiga kwa mapanga, marungu na mawe huku wakidai kuwa ndio mwisho wake. 

“Waliponichomoa kwenye gari waliniuliza iko wapi bastola, nikawajibu sina… walinigawanya kama fisi kwa kunipiga hadi nikajifanya kuzirai, wakasema tayari wamemaliza kazi,” alisema lakini alinyanyuka na kutimua mbio hadi kwenye gari la Polisi na kuingia kwenye buti, na baadaye askari wale wakawapa fomu ya polisi kwa ajili ya matibabu (PF3). 

Machemli alidai kuwa lengo lilikuwa kumwua Kiwia na ndiyo maana walikuwa wakiulizia bastola ili ionekane kuwa alikuwa na lengo la kushambulia na ndiyo maana askari wa Polisi walikuwa wakiangalia tukio hilo bila kutoa ushirikiano. 

Akizungumzia tukio hilo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kitendo hicho ni cha kinyama, lakini alisikitikishwa pale ambapo lawama za tukio hilo zimetupiwa CCM wakati chama hicho hakihusiki. 

“Tunawapa pole wenzetu na tunaungana nao kulaani kitendo hicho kwa sababu hata kama wangekuwa wanafanya jambo kinyume cha sheria, waliowapiga hawakupaswa kuchukua hatua mikononi, vipo vyombo vya Dola vingechukua hatua, tunaomba viwasake wahusika na kuwafikisha mbele ya sheria,” Nape aliwaambia waandishi wa habari jana Dar es Salaam. 

Alisema CCM kama chama cha siasa hakina mpango wala hakitakuwa nao wa kupiga watu au kutetea wanaochukua sheria mikononi. “Tukio hili limetokea saa nane usiku iwapo wawili hawa wangekuwa hawafanyi jambo baya wangeshirikisha Polisi,” alisema Nape.


Habari Leo

No comments: