WATU wanne akiwemo Diwani wa Kata ya Kasamwa katika Wilaya ya Geita mkoani Geita kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya hiyo, kwa tuhuma za kuhusika na unyang’anyi wa kutumia silaha.
Watuhumiwa hao walipanda kizimbani jana mbele ya Hakimu wa Wilaya hiyo, Isdory Kamugisha na kusomewa mashitaka hayo na Mwendesha Mashitaka Msaidizi wa Polisi, Thomas Mboya. Alisema upelelezi wa shauri hilo umekamilika.
Mbele ya Kamugisha, Mwendesha Mashitaka huyo aliwataja washitakiwa kuwa ni Nicholaus Busegwa (32), Ngiyu Mwecha (37), Zenze Richard (40), na Diwani Fabian Mahenge (49) wa Chadema.
Mwendesha Mashitaka huyo aliieleza mahakama kuwa washitakiwa kwa pamoja, wanadaiwa kutenda kosa hilo Februari 27, mwaka huu majira ya saa 2 usiku katika kijiji hicho cha Kasamwa.
Alidai siku ya tukio, washitakiwa walivamia nyumbani kwa mtu aliyetambuliwa kwa jina na Lukandya Malimi mkazi wa kijiji hicho na kumpora fedha taslimu Sh 150,000 pamoja na simu moja ya mkononi aina ya Nokia yenye thamani ya Sh 105,000 na kufanya mali zote kuwa na thamani ya Sh 255,000.
Aidha, aliifafanulia mahakama kuwa kabla ya kufanya uporaji, walimkatakata kwa mapanga mlalamikaji na kisha kumfunga kamba shingoni na kumnyonga ambapo alipoteza fahamu kwa zaidi ya saa nane na alikimbizwa hospitalini na madaktari kufanikiwa kuokoa maisha yake.
Watuhumiwa wote wamepelekwa rumande hadi Aprili 12, mwaka huu wakati kesi yao itakapoanza kusikilizwa baada ya polisi kukamilisha upelelezi wa shauri hilo.
No comments:
Post a Comment