ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 4, 2012

Polisi aliyekutwa na bangi disko atimuliwa

POLISI imemfukuza kazi askari G845 Konstebo Deogratius (22), kwa kosa la kuingia kwenye ukumbi wa disko akiwa na misokoto minne ya bangi na kufanya fujo. 

Askari huyo amekuwa wa 18 tangu kuanza mwaka huu, kupewa adhabu ikiwamo ya kufukuzwa kazi na kushushwa vyeo kutokana na makosa mbalimbali. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Absalom Mwakyoma, alisema askari huyo alifanya vurugu hizo Machi 24 saa 5.56 usiku kwenye ukumbi wa Pub Alberto. 

Mwakyoma alisema askari huyo alipoingia ukumbini alifanya fujo na kujeruhi watu kadhaa akiwamo mlinzi na mmiliki wa klabu hiyo. 

Kwa mujibu wa Mwakyoma, taarifa zilifika Polisi na askari wenzake walifuatilia na kumkamata na alipopekuliwa, alikutwa na misokoto minne ya dawa hizo za kulevya. 

Alisema baada ya hapo, askari huyo alifikishwa katika mahakama ya kijeshi na kukutwa na hatia ya makosa mawili ya kudhuru mwili na kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi. 

“Kitendo hicho ni cha fedheha na ni kinyume cha maadili kwa Polisi, hatupendi kabisa kuona askari wetu wakifanya hivyo, ila inatokea na Polisi lazima ichukue hatua za kinidhamu ili kukabiliana na fedheha hiyo,” alisema Mwakyoma. 


Aliongeza kuwa Kamati ya Maadili ya Polisi ilikaa na kuamua kumfukuza kazi askari huyo ili kumpa nafasi Wakili wa Serikali kuandaa mashitaka na kumfikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili kiraia. 

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Saidi Mwema alionya kuwa katika mkakati wa kusafisha Jeshi hilo, askari wote wanaokiuka sheria za Polisi na wasio na vigezo vya utendaji kazi watafukuzwa. Mwema alisema hayo wakati akifunga mafunzo ya awali ya askari Polisi katika Chuo cha Taaluma ya Polisi (CCP) mjini hapa. 

Alisema patakuwa na ufuatiliaji wa kila askari na baada ya hapo, kutaandaliwa ripoti ya kila mwezi na kila baada ya miaka mitano, jeshi hilo litafanya tathmini ya utendaji kazi wa kila askari na kufukuza wasiokidhi vigezo. 

Kauli hiyo ya Mwema ilitafsiriwa kuwa ya kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete, ambaye hivi karibuni aliutaka uongozi wa Polisi kuangalia upya utaratibu wa vijana wanaoomba nafasi za kujiunga na Jeshi hilo, kwani itafika mahali litaonekana la wahuni na si la ulinzi wa raia na mali zao. 

Aliwataka kuwa na utaratibu wa ndani wa kuangalia tabia za askari wao, ili wajue tabia zao na kuzirekebisha kabla hazijaleta madhara kwa wananchi. 

Rais katika agizo hilo, alisema amepata malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuwa wapo askari wanaolala baa, walevi, wahuni, wala rushwa na wanaoshirikiana na majambazi. 

Aliagiza wachunguzwe na wakibainika waonywe kwa mara ya kwanza na wakirudia waondolewe kazini. Alisema wapo vijana waadilifu wanaotafuta nafasi hizo lakini hawajazipata. 

Hivi karibuni polisi mwingine aliyeingia katika ukumbi huo akiwa na bunduki aina ya SMG yenye risasi 30 alitimuliwa kazi. 

Kwa mujibu wa Mwakyoma polisi huyo alifukuzwa kazi baada ya kupatikana na hatia katika mahakama ya kijeshi kwa fedheha iliyotokana na kutenda mambo ambayo ni kinyume na mwenendo mwema.


Habari Leo

No comments: