ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 6, 2012

Ijue dunia ya wanawake wakorofi!

RAFIKI yangu, kama wewe ni mara yako ya kwanza kufungua ukurasa huu hutakiwi kukosa kila wiki, maana utakuza ufahamu wako na kukujenga katika uhusiano wako.
Leo nakwenda kuzungumza nanyi jambo muhimu sana; tatizo la wanawake wakorofi. Katika jamii yetu, kuna baadhi ya wanawake wana tabia ya ukorofi na ujeuri.
Kila atakachokiongea mwenzake, yeye hubisha bila sababu za msingi. Akielekezwa kwamba jambo fulani halifai, hupinga. Hili ni tatizo kubwa sana kwa wanaume wengi. Kwa kawaida hulka ya mwanaume ni kuheshimiwa, kunyenyekewa na kusikilizwa.
Hivi ndivyo walivyoumbwa, ndiyo maana inapotokea mwanamke akashindwa kumheshimu mwanaume, hasira huweza kupanda na kusababisha kumuangushia kipigo. Kimsingi ni tatizo ambalo kama lisipothibitiwa mapema, linaweza kusababisha mgogoro katika familia.
KWA NINI WANAUME?
Kama nilivyoeleza hapo juu, hulka ya mwanaume ni kusikilizwa, kupewa nafasi ya kwanza na kumuongoza mwanamke wake. Kwa msingi inapotokea ametoa agizo fulani au wapo kwenye mazungumzo na mwenzi wake, halafu akajaribu kumweleza mpenzi wake kitu fulani, akampinga ndipo tatizo linapoanzia.
Mwanaume anajiamini, anaamini mawazo yake, lakini pia anapenda kutoa maelekezo kwa njia bora na ya kirafiki. Kwa tabia ya wanawake ninaowazungumzia hapa, hata kama mwanaume wake atazungumza kwa lugha nzuri kiasi gani, kama hataki ataleta jeuri huku akiwa hana pointi za kushibisha msimamo wake.

KIBURI/DHARAU
Ni hali ya kukiuka, kukataa au kubisha bila sababu za msingi. Mwanamke huyu ni kidomodomo, muongeaji sana na hataki kuelekezwa. Anajiamini yupo sahihi kwa kila hatua na mbishi kupitiliza.
Yote haya kwa pamoja, yakifanywa kwa mwanaume anayejua haki na wajibu wake, ndipo msuguano unapoanzia.

NI SABABU YA KUACHANA?
Yupo jamaa mmoja alinitumia meseji akisema: “Brother Shaluwa mimi nimechoshwa kabisa na tabia ya mpenzi wangu. Yaani ni kiburi kupindukia, kila ninachomwambia, anapingana na mimi. Kiukweli nimemchoka na ninataka kuachana naye moja kwa moja. Nimechoka sasa. Je, wewe unaonaje?”
Umeona maneno ya msomaji wetu huyo wa Iringa? Je, unadhani yupo sawa? Nilimwambia nitamjibu kwenye gazeti, ndivyo ninavyofanya sasa hivi. Kiukweli hayupo sawa. Kwa kawaida, kuna kasoro ambazo tunaziita ndogondogo na nyingine kubwa.
Wakati wa kuchagua mwenzi wa kuingia naye kwenye ndoa ni muhimu kukagua kasoro za mwenzako. Kuna nyingine zinavumilika na nyingine ni kubwa. Kwa bahati mbaya kuna wengine hadi wanaingia kwenye ndoa wanakuwa bado hawajajua kasoro za wenzao, mara anagundua kwamba mke wake ana kiburi na jeuri – siyo sababu ya kumuacha!
Rafiki zangu, kuna kitu cha kufanya zaidi ya kuachana. Hebu tuendelee kuona?

UPO UPANDE UPI?
Je, wewe unasumbuliwa na mwanamke mkorofi? Unaishi naye au ni mchumba wako? Rafiki yangu, msingi mkubwa unaoweza kubeba penzi lenu wakati unatafuta dawa ya ukorofi wake ni penzi la kweli moyoni mwako.
Kwanza umpende, utambue thamani yake kwako, uuchukulie udhaifu wake kama sehemu ya mapenzi yako kwake, halafu tafuta tiba ya tatizo lake. Je, mpenzi wako yupo upande upi?
Unajua kuna wanawake wengine ni wakorofi, lakini ukifuatilia sana ukorofi wao una maana. Unasaidia kwenye maeneo fulani. Si kila kinachozungumzwa na mwanaume kipo sahihi. Mwanaume anatakiwa kukubali kupewa mawazo na mwanamke wake. Tatizo lililopo ni namna mwenzi wake anavyowasilisha kwa mwanaume wake.
Usiamini kila kinachotoka kinywani mwako kipo sawasawa, wakati mwingine unaweza kukosea na mwenzi wako akataka kukushauri. Jambo kubwa hapa ni namna gani basi, anavyoweza kuwasilisha hisia zake.
Mwanamke mwenye busara hana maneno mengi, huomba samahani kwanza, kisha kuanza kumweleza mwenzake anavyojisikia taratibu na kwa hoja. Si kuropoka. Si kejeli wala jeuri. Atajenga hoja yake kikamilifu kwa kutumia mifano na maneno yenye staha.
Natamani sana kuendelea na mada hii, lakini nafasi yangu haitoshi. Wiki ijayo tutakwenda moja kwa moja kwenye nini cha kufanya, ikiwa upo kwenye uhusiano na mwanamke mkorofi. Tafadhali USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na Who is Your Valentine? vilivyopo mitaani.

No comments: