ANGALIA LIVE NEWS
Friday, April 27, 2012
JK aitisha Kamati Kuu CCM ghafla
NI KUJADILI MUSTAKABALI WA MAWAZIRI WALIOTAKIWA KUJIUZULU, WENYEWE WAVUNJA UKIMYA
Waandishi Wetu
WAKATI joto la wabunge, vyama vya siasa na wanaharakati nchini kutaka mawaziri waliohusishwa na kashfa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) wajiuzuluzu likizidi kupanda, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete ameitisha kikao cha ghafla cha Kamati Kuu ya chama hicho kujadili pamoja na mambo mengine, hali ya siasa nchini.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana na kuthibitishwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi Nape Nnauye, zilieleza kuwa kikao hicho kitafanyika leo Ikulu ya Dar es Salaam kuanzia saa 4:00 asubuhi.
Ingawa Nape alisema hawezi kutaja ajenda za kikao hicho kwa kuwa ni siri, habari kutoka baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM, zilidokeza kuwa hakuna namna, Rais Kikwete akakwepa kuzungumzia shinikizo la mawaziri hao kujiuzulu.
"Ni kweli kesho (leo) tuna Kamati Kuu Dar es Salaam, lakini agenda za kikao hicho haziwezi kuwekwa 'public' ujue hivyo tu inatosha," alisema Nape.
Nape alishindwa kuthibitisha au kukanusha taarifa kwamba kikao hicho kitajadili hatima ya mawaziri hao wanaotakiwa kujiuzulu badala yake akasema,"Kama nilivyokwambia hakuna agenda ya kuweka 'public' wewe hayo unayoyazungumza unayajua wewe ukitaka yangu, andika nilichokwambia."
Mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu ni Kepteni George Mkuchika (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), William Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Hadji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara), Profesa Jumanne Maghembe (Kilimo, Chakula na Ushirika), Mhandisi Omar Nundu (Uchukuzi) pamoja na Mkulo na Nyalandu.
Wakati kukiwa na taarifa za Kamati Kuu kuwajadili mawaziri hao, watano kati yao wameonekana kutokuwa tayari kujiuzulu huku baadhi wakihoji sababu za kufanya hivyo na Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo akisema kuwa hajui madai ya wabunge hao dhidi yake.
Waziri Mkulo (Fedha), Lazaro Nyalandu (Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko) na Athuman Mfutakamba (Naibu Waziri wa Uchukuzi), walisema hawafikirii kujiuzulu kwa kuwa hawajui makosa yao.
Shinikizo la kutaka mawaziri nane wajiuzulu liliibuka katika Mkutano wa Saba wa Bunge uliomalizika mjini Dodoma mwanzoni mwa wiki hii, baada ya ripoti hiyo ya CAG kuonyesha tuhuma nzito za ufisadi katika wizara hizo huku baadhi ya mawaziri wakionekana kuhusika moja kwa moja na maamuzi waliyofanya.
Baadhi ya mawaziri hao walitoa utetezi wao bungeni na wengine walipokutana kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari, lakini jitihada hizo za kujisafisha hazikuzaa matunda kutokana na ongezeko la shinikizo hilo kutoka kwa makundi mbalimbali ya kijamii.
Mkulo: Sijui kinachoendelea
Mkulo ambaye alikuwa waziri wa kwanza kutakiwa na wabunge ajiuzulu, kutokana na kashfa ya kuvunja Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) ili kuficha tuhuma zake ikiwemo uuzaji wa kiwanja Na.10 kwa Kampuni ya Mohamed Enterprises (MeTL), alisema hawezi kuzungumzia suala la kujiuzulu kwa sababu hajui kosa lake wala madai ya wabunge dhidi yake.
Waziri huyo alisema yaliyozungumzwa na wabunge hakuyasikia kwa kuwa hakuwapo bungeni Dodoma kwa muda mrefu kutokana na kuwa safarini.
Alipoulizwa kama yuko tayari kujiuzulu kuhusiana na kashfa zinazoikabili wizara yake, Mkulo alijibu, ‘ hapa, no comment," akiwa na maana kwamba hana cha kuzungumza.
“Kwanza sifahamu tuhuma zilizotolewa na wabunge kwa sababu sikuwepo, mimi nilikuwa safari,” alisema.
Hata alipoulizwa kuhusiana na wizara yake kuuza kiwanja hicho cha Serikali kilichopo katika Barabara ya Nyerere, jijini Dar es Salaam kinyume cha taratibu, Mkulo aliendelea kusema, ‘no comment, no comment kwa hilo.’
Mfutakamba
Jana Mfutakamba aliliambia Mwananchi kuwa haoni sababu yoyote ya kujiuzulu kwani hana tuhuma zozote ndiyo maana pia hata wabunge katika orodha yao hawakuweza kumtaja popote.
Mfutakamba alitoa kauli hiyo wakati ambao Waziri Nundu amemtuhumu kwamba amekuwa akishinikiza Kampuni ya China Communication Construction Company (CCCC), ipewe kazi ya kujenga gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuwa ilimgharamia safari kwenda nje ya nchi.
Hata hivyo, Mfutakamba alikiri kusafirishwa na kampuni hiyo na kuongeza kwamba alikwenda huko kutembelea miradi mbalimbali ikiwamo ya ujenzi wa reli na magati kwa kufuata taratibu zote na aliporudi aliieleza Serikali uwezo wa kampuni ya CCCC, Kampuni ambayo inapingwa na Nundu aliyedai kuwa ilimsafirisha Mfutakamba baada ya yeye kukataa.
Nyalandu
Jana, Nyalandu alisema kuwa, mpaka sasa haelewi kwanini ameingizwa kwenye kashfa hiyo kwa sababu katika ripoti ya CAG, hakutajwa na wenyeviti wa kamati mbalimbali za kumudu za Bunge.
“Sielewi kwanini nimeingizwa kwenye kashfa hii kwa sababu katika ripoti ya CAG sikuwemo. Ripoti ya Mwenyekiti wa Kamati ya POAC na PAC simo pia, lakini nilishangaa nilipoanza kusikia jina langu,” alisema Nyalandu.
Aliongeza kuwa baadhi ya mawaziri waliotuhumiwa kwenye kashfa hiyo waliitwa na Kamati ya CCM kwa ajili ya mahojiano, lakini yeye hakuitwa.
Alisema kutokana na hali hiyo anashindwa kuelewa kwanini jina lake lilikuwa miongoni mwa watu waliotajwa wakati hayumo kwenye ripoti yoyote.
Alisema kutokana na hali hiyo anaamini kuwa watu waliomtaja wana sababu zao binafsi, kwamba Kamati za Bunge ndizo zenye majukumu ya kuthibitisha ukweli kuhusu tuhuma anazopewa.
Tayari Nyalandu alitoa waraka unaonyesha msimamo tofauti na wa bosi wake, Dk Chami kuhusu kashfa zinazowakabili ambazo ni tuhuma alizonazo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Viwango (TBS), Charles Ekelege anayedaiwa kuanzisha kampuni hewa za ukaguzi wa magari nje ya nchi hususani, Hong Kong na Singapore.
Wakati Nyalandu akishauri Ekelege asimamishwe kazi ili apishe uchunguzi wa CAG na endapo hatakuwa na tuhuma za kujibu arudishwe kazini, waziri wake (Chami) alisema kuwa Ekelege ni mteule wa rais, hivyo hawezi kwenda kwa Rais Jakaya Kikwete kumtaka amwondoe wakati hakuna taarifa yoyote inayoonyesha tuhuma zake.
Sakata la kuwepo kwa kampuni hizo hewa za ukaguzi wa magari liliwekwa wazi katika ripoti iliyotolewa na CAG na wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge za Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) inayoongozwa na Zitto Kabwe na ile ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC) ya John Momose Cheyo huku ikielezwa kuwa wanamkingia kifua Ekelege kutokana na kushindwa kumchukulia hatua.
Mponda aahidi kuweka mambo hadharani leo
Kwa upande wake, Dk Mponda alipoulizwa kama atajiuzulu kutokana na kashfa zinazoikumba wizara yake alisema atazungumzia suala hilo kesho (leo) na kuongeza, “Njoo Ijumaa tutazungumza, leo sisemi chochote, nipigie asubuhi ili nikupangie muda wa kuja ofisini,”alisema Dk Mponda.
Waziri huyo anakabiliwa na kashfa ya Bohari ya Dawa (MSD) ambako ukaguzi maalum katika bohari hiyo uliofanyika ulibaini kuwapo tofauti ya Sh 658.9 milioni ikiwa ni pungufu ya kiasi ambacho kilipokelewa na kuripotiwa wizarani kwenda MSD, huku ushahidi wa kuzipokea kutotolewa.
Pia, uchunguzi unaonyesha kuwapo Sh 100 milioni zilizopelekwa MSD kutoka Wizara ya Afya na kutumiwa na bohari hiyo bila kuwepo kwa mchanganuo wa matumizi.
Ukaguzi pia ulibaini kuwepo kwa kiasi cha Sh 4.5 bilioni zilizotoka Hazina kwenda Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa vya hospitali, lakini kiasi cha Sh 4.344 bilioni ndio kilichopelekwa MSD ukiondoa Sh 196 milioni ambazo zilitumika bila kuwapo kwa ushahidi wa kupokelewa MSD kutoka Wizara ya Afya.
Maige anena
Waziri Maige juzi aliamua kueleza baadhi ya tuhuma zinazomkabili ikiwamo umiliki wa nyumba aliyodaiwa kuinunua kwa Dola 700,000 za Marekani, akisema nyumba hiyo aliinunua kwa dola 410,000 na siyo dola 700,000 kama ilivyoelezwa.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Malisili na Mazingira, James Lembeli alipinga kauli hiyo akisema taarifa alizonazo zinaonyesha Maige alinunua nyumba hiyo kwa fedha taslimu dola 700,000.
Kashfa nyingine inayomkabili Maige ni ile iliyotolewa na Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira huku ikitaka awajibishwe kwa kutengeneza mazingira ya rushwa katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji kwa kampuni ambazo hazina sifa na kusafitishwa nje kwa wanyama wakiwamo twiga na tembo kinyume cha sheria.
Hata hivyo, Maige alisema hivi sasa kuna mapambano ya kisiasa baina ya viongozi mbalimbali na kwamba habari mbaya dhidi yake zinalenga kumchafua kutokana na kuwa mkali katika utendaji wake wa kazi na kuongeza, kuna chuki kutokana na kwamba aliwahi kuwafukuza kazi baadhi ya watendaji wizarani kwake jambo ambalo limewaudhi baadhi yao.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema) Zitto Kabwe ndiye aliyenogesha hoja hiyo ya kutaka mawaziri hao wajiuzulu baada ya kutaka Bunge lipige kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kama Serikali haitawafukuza kazi mawaziri hao.
Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment