RAIS Bingu wa Mutharika (pichani) wa Malawi amefariki dunia, madaktari na mawaziri
wameiambia BBC, lakini haijatangazwa rasmi na Serikali ya nchi hiyo.
Mmoja wa madaktari ambaye alimhudumia Mutharika (78), amesema, “kitabibu Rais alifariki
dunia jana, baada ya kupata mshituko wa moyo.
"Amefariki dunia … baada ya saa mbili za kujaribu kuokoa maisha yake,” muda mfupi baada
ya usiku wa manane, chanzo katika hospitali ya Lilongwe kilikaririwa kikisema bila kutaka kutajwa jina, kwani Serikali ndiyo inayoweza kutangaza hali hiyo.
Vyombo vya habari vya Serikali hadi jana viliendelea kutangaza kwamba alikimbizwa Afrika Kusini kwa matibabu. Ikithibitishwa, kifo chake kinaweza kusababisha mgogoro wa kikatiba, mchambuzi mmoja amesema.
Kwa mujibu wa Katiba, Makamu wa Rais anapaswa kushika madaraka iwapo mkuu wa nchi atapoteza uwezo wa kutenda wajibu wake au akifa akiwa madarakani.
Lakini Makamu wa Rais, Joyce Banda na Mutharika, walitofautiana baada ya mvutano wa urithi wa madaraka ndani ya chama mwaka juzi na akafukuzwa kutoka chama tawala cha Democratic People's (DPP).
Ndugu wa Mutharika, Waziri wa Mambo ya Nje, Peter Mutharika, alichaguliwa badala ya Banda
kuwa mgombea urais wa DPP katika uchaguzi ujao wa mwaka 2014.
Amekuwa akimwakilisha Rais wakati mwingine kunapokuwa na shughuli za kitaifa. Hivi karibuni Banda aliiambia BBC, kwamba hajazungumza na Bingu kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
BBC jijini Blantyre, inasema mawaziri walikesha usiku wa kuamkia jana, wakijadili hali ilivyo. Madaktari na mawaziri walisema mwili wa Mutharika ulipelekwa Afrika Kusini huku uamuzi ukichukuliwa wa nini kifuate.
Vyanzo ndani ya Serikali viliiambia BBC, kwamba juhudi za kuokoa maisha ya Rais Mutharika
zilishindikana na kwamba taarifa rasmi inaandaliwa.
Gazeti la Daily Times liliandika kwamba Wamalawi wako “njia panda” kuhusu Rais.
“Sintofahamu kwa Taifa imeongezeka baada ya maofisa wa ngazi za juu wakiwamo mawaziri
kadhaa, kuwasili katika hospitali alimokimbizwa na kwenda moja kwa moja katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU),” lilisema.
“Baada ya muda walitoka nje wakionesha sura za huzuni bila kusema lolote.” Gazeti lingine huru la Nation, liliikosoa Serikali kwa jinsi lilivyoichukulia hali ya matibabu ya Rais. “Huu ni wakati wa kufanya mambo vizuri kwa kutoa taarifa kwa wakati,” gazeti hilo liliandika na kuongeza, kwamba Serikali “ingefanya vema zaidi kuliko kutoa taarifa za mkato kupitia redio yake – na watu kuachwa kila mmoja aseme lake kwa hisia zake.”
Gazeti la Nyasa Times liliripoti, kwamba hatua ya Mutharika kupelekwa Afrika Kusini kwa ndege ililenga kuvuta muda kwa chama tawala kujipanga kutokana na kifo hicho.
Mutharika ambaye ni mchumiwa zamani wa Benki ya Dunia, aliingia madarakani mwaka 2004.
Baada ya muda mfupi alikiacha chama chake cha United Democratic (UDF) na kuanzisha DPP, baada ya kuwatuhumu wanachama wa UDF kuwa wanapinga juhudi zake za kupambana na rushwa.
Tangu achaguliwe kwa kishindo mwaka 2009, wanaomkosoa wanadai kuwa ameonesha kujilimbikizia madaraka zaidi.
Rais amekuwa akikabiliwa na shinikizo la kumtaka ajiuzulu, huku akituhumiwa pia kwa upendeleo wa kindugu na usimamizi mbovu wa uchumi.
Ukosoaji huo umesababisha pia kutibuka kwa uhusiano na wafadhili wakubwa hususan Uingereza.
Mwaka jana, Mutharika alimtimua Balozi wa Uingereza nchini Malawi, Fergus Cochrane-Dyet, baada ya taarifa za ubalozi kuvuja zikimkariri balozi huyo akisema Rais havumilii kukosolewa.
Kiongozi huyo wa Malawi alisema hawezi kukubali ‘matusi’ kwa sababu tu Uingereza ni nchi
mfadhili wake mkubwa.
Ikijibu hatua hiyo, Uingereza nayo ilimtimua Balozi wa Malawi nchini humo na kusitisha misaada yake ya moja kwa moja kwa nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika.
Malawi ni moja ya nchi masikini sana duniani, ikiwa na takriban asilimia 75 ya watu wake
wanaoishi chini ya dola moja kwa siku.
Nchi hiyo imekumbwa na upungufu wa mafuta jamii ya petroli na fedha za kigeni tangu Uingereza na wafadhili wengine wafute misaada yao kwake.
Habari Leo
No comments:
Post a Comment