MWANAFUNZI wa chuo cha Azania, Steven Likandamila (24) amekufa ghafla baada ya kudondoka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 4 asubuhi katika eneo la Magomeni Makanya.
Alisema siku ya tukio mwanafunzi huyo akiwa na mwenzake Emmanuel Shoo, waliagiza soda dukani na baada ya kumaliza kunywa soda hiyo alianza kulalamika tumbo na hatimaye alianguka chini na kuanza kutoa mapovu mdomoni na kufariki dunia.
Chanzo cha kifo hicho bado hakijafahamika, maiti imehifadhiwa katika hospitali ya Mwananyamala.
Wakati huo huo, watu 18 wamenusurika kufa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupoteza uelekeo na kutumbukia mtaroni katika eneo la Mtoni Mtongani.
Mmoja wa majeruhi hao, Hassan Mohamed alisema kuwa dereva wa gari hilo alikuwa katika mwendo kasi, ndipo gari hilo lilipomshinda na kuingia katika korongo lilipo pembezoni mwa barabara hiyo.
Kwa mujibu wa muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Temeke, Curtias Mbalamula alisema kuwa walipokea jumla ya majeruhi 18 hospitalini hapo ambapo majeruhi wanne ambao hali zao si nzuri wamepelekwa katika Hospitali ya taifa ya Muhimbili.
Aliwataja waliopelekwa Hospitali ya Muhimbili kuwa ni Magreth Mvungi ambaye amekatika mkono, Julius Josiah, Hassan Omary na Rashid Mohamed.
Hata hivyo, juhudi za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke kuzungumzia ajali hiyo zilishindikana.
No comments:
Post a Comment