ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 13, 2012

Profesa Lipumba atoa somo la uchumi

Mwenyekiti wa CUF Professa Ibrahimu Lipumba
Geofrey Nyang’oro
MWENYEKITI wa CUF Professa Ibrahimu Lipumba amesema  mfumuko wa bei za bidhaa nchini umetokana na matumizi makubwa yanayofanywa na serikali ikilinganishwa na mapato yake.

Lipumba ambaye kitaalamu ni mchumi alisema hayo jana alipokuwa akizungumza katika kipindi cha asubuhi njema  kinachorushwa na kituo cha Television cha Channel Ten cha jijini Dar es Salam.

“Inapotokea  fedha zinazokuwa nyingi kwenye mzunguko kuliko bidhaa zilizopo sokoni hali hiyo hulazimika kuongezeka kwa mfumo wa bei na hilo linatoka na matumizi mabaya ya serikali ambapo fedha nyingi zinatumika bila tija,” alisema Lipumba.

Alisema njia pekee ya kuondoa hali hiyo ni serikali kupunguza matumizi na  kujenga mazingira ya kuongeza uzalishaji wa bidhaa za kilimo na viwandani kupitia wakulima wadogo.

“Vita dhidi ya umaskini ni ngumu kufanikiwa kwa nchi kama Tanzania kwa sababu inategemea kilimo na wakulima wadogo hawajajengewa uwezo wa kunufaika na kazi zao,”alisema Lipumba.

Akizungumzia vitendo vya rushwa katika mashirika ya  umma, Profesa Lipumba alisema hali hiyo inatokana na  uteuzi wa wajumbe katika bodi za mashirika hayo kufanywa kisiasa.

“Kazi ya Mbunge ni kutunga sheria na kuisimamia serikali, lakini mbunge ndiye anayeteuliwa  kuiongoza bodi ambayo mwisho wa siku inapaswa kukaguliwa na wabunge,”alisema Lipumba

Rushwa katika uchaguzi

Profesa Lipumba alisema rushwa katika changuzi zitakomeshwa endapo serikali itatoa fedha za uchaguzi na kuvibana vyama vya siasa kujitegemea.

“Rushwa kwenye uchaguzi itapungua iwapo serikali itatenga kiasi cha fedha zinazostahili kutumika katika uchaguzi na kuzitoa kwa ajili ya shughuli za uchaguzi,”alisema.

Mwenyekiti huyo pamoja na kupongeza hatua ya Rais kuunda Tume ya katiba pia alielezea umuhimu wa kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi akisema haitasaidia kuboresha uchaguzi katika nchi.

“Tunahitaji Tume huru ya uchaguzi,pia inapaswa kuwa na watendaji wake ambao watafanya kazi ya kuandaa daftarila wapiga kura na mazingira yake badala yakutegemea wafanyakazi toka sehemu nyingine”alisema.

Mwananchi

No comments: