ANGALIA LIVE NEWS
Friday, April 27, 2012
Utajiri wa Waziri Maige wapingwa kila kona
SIKU moja baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige kukiri kununua nyumba jijini Dar es Salaam kwa Dola za Marekani 410,000, taasisi na watu mbalimbali wameeleza kutoridhishwa na utajiri wake, huku Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) likitaka ashtakiwe kwa kuhujumu uchumi.
Wamesema kipato cha Waziri Maige kama mtumishi wa umma, hakilingani na thamani ya mali hiyo anayomiliki, hivyo ni vyema hatua za kisheria zikachukuliwa ili kuthibitisha madai yake kwamba anaimiliki kihalali.
Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya alieleza kushangazwa na utajiri wa waziri huyo kijana akisema kuwa una walakini, hivyo ni vyema sheria ikachukua mkondo.
“Tucta tunasema ashtakiwe kama mhujumu uchumi. Pia tunasema wazi kwamba tunasikitishwa na jinsi Serikali inavyofanya kazi. Tunaungana na wabunge 70 waliosaini kumtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ajiuzulu,” alisema Mgaya.
Mgaya alisema sasa ni wakati mwafaka kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (Takukuru), kumchunguza waziri huyo ili kubaini ukweli wa madai yake kwamba mali hizo anamiliki kihalali.
Alisema haoni msingi wa Waziri Maige kumiliki nyumba ya gharama kubwa kiasi hicho, ikizingatiwa kuwa anatoka katika jimbo la uchaguzi ambalo wanafunzi wa shule za eneo hilo bado wanakaa sakafuni kutokana na ukosefu wa madawati.
“Anasa ya kukaa katika nyumba ya fahari namna hiyo anaitoa wapi wakati kuna watoto jimboni kwake wanakaa sakafuni?,” alihoji Mgaya.
Maige ana miaka 40, aliingia mara kwanza bungeni mwaka 2005 na akachaguliwa kuwa naibu waziri wa maliasili ambako sasa anaitumikia kama waziri kamali baada ya kuchaguliwa bungeni mwaka 2010.
Waziri huyo anatuhumiwa kununua nyumba eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam kwa dola 700, tuhuma ambazo amezikiri na kueleza kuwa nyumba hiyo aliinunua kwa Dola 410,000.
Mwenyekiti wa Chama Cha Madereva wa Malori Tanzania (Chamamata), Rocket Matogolo alisema mapato anayoyapata Waziri Maige kutokana na kumiliki malori mawili yanashangaza.
Matogoro alisema katika kikao walichokaa Februari mwaka huu kati ya chama chao na Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania kuomba kupandishwa posho za kujikimu wakiwa safarini, wamiliki hao waligoma wakidai kuwa wanapata mapato kidogo.
Alisema madereva walitaka kupandishwa posho ya safari kutoka dola 350 kwa safari ya siku 15 kwa nchi jirani hadi dola 500, lakini wamiliki hao waligoma wakidai fedha wanazopata kutokana na malori yao kukodishwa ni ndogo.
Matogolo alisema katika kikao hicho wamiliki hao walitoa hadharani mapato yao ya safari moja ya kusafirisha mzigo kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambayo huchukua mwezi mmoja hupata Dola 6,000.
Alisema baada ya kuondoa gharama za mafuta, mshahara wa dereva na mambo mengine, wamiliki hao wa malori walisema hubakiwa na faida ya Dola 2,100.
“Sasa hii kauli ya Waziri Maige kuwa anapata dola 10,000 kwa lori moja kwa mwezi tunashindwa kuelewa nani mkweli,” alisema Matogolo na kuongeza:
“Kanuni za Chama cha Wamiliki wa Malori, zinataka kabla ya kusafirisha mzigo kwenda nje ya nchi lazima upate kibali kwao”.
Alisema kutokana na kanuni hizo ni wazi kuwa Maige kupitia Kampuni yake alikuwa mwanachama wa chama hicho.
Matogolo aliwataka wamiliki hao kueleza ukweli wa mapato wanayoyapata baada ya kusafirisha mizigo badala ya kuwadanganya na kuwaweka wao katika hali ngumu ya maisha wakati wao (wamiliki) wakifaidi.
Mkurugenzi Mtyendaji Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Ananilea Nkya alisema alishangaa kusikia waziri kijana ambaye hana utumishi wa muda mrefu, akimiliki nyumba yenye thamani ya Dola700,000.
“Hivi inawezekana kweli kipaumbele cha kwanza cha mbunge huyo kijana iwe ni nyumba ya thamani kubwa kiasi hicho? Na kama ndio kipaumbele chake ina maana ana utajiri wa kiasi gani na ameupata vipi?” alihoji Nkya na kuongeza: "Hivi ni vitu vingapi anamiliki ambavyo thamani yake hatujui?”
Nkya alitaka uchunguzi ufanywe kwenye kampuni anayodai ameikodishia magari ya Maige na kumlipa kiasi kikubwa cha fedha namna hiyo na kwamba achunguzwe kama inalipa kodi.
Nkya alisema iwapo hali imefikia hatua hiyo ana wasiwasi juu ya hali ya usalama na utulivu vinavyotajwa kama vitaendelea kuwepo baina ya viongozi, wananchi na Serikali kwa upande mwingine.
Mkurugenzi huyo ameitaka Serikali imchunguze Maige na kuchukua hatua vinginevyo itakuwa ni kujenga chuki na uhasama baina ya jamii, jambo ambalo si zuri kutokea.
“Serikali imchunguze na kuchukua hatua vinginevyo hali inaweza kuwa mbaya zaidi ya hao viongozi wanavyofikiri,” alisema Nkya.
Naye, Mkurugenzi wa Shirika la Sikia, Irenei Kiria amependekeza kufanyika uchunguzi wa kina kubaini ukweli wa uhalali wa mali anazomiliki Waziri Maige.
Alisema ikiwa tume hiyo huru ya uchunguzi inapaswa kuangaliwa ana mali nyingine anazomiliki na endapo itabaini kuwa nyumba aliyonunua haiendani na kipato chake hatua zichukuliwe dhidi yake.
“Wizara anayofanyia kazi inakabiliwa na tuhumu mbalimbali hivyo ufanyike uchunguzi kubaini uwezo wa kipato chake kama ni cha halali na ikibainika kuwa hakupata kihalali hatua za kisheria zichukuliwe ikiwamo kufikishwa mahakamani,” alisema Kiria.
Kiria alikwenda mbali alipendekeza uundwe utaratibu wa kuwachunguza viongozi na watendaji serikali na kwamba watakaobainika kujihusisha na vitendo vya ufisadi wachukuliwe hatua za kisheria.
Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR Mageuzi, Samuel Ruhuza alisema kuwa jambo la msingi siyo kununua nyumba bali ni namna gani amepata fedha zilizomuwezesha kununua hiyo nyumba.
“Kuna watu wamejenga fikra za kuwachukia wenye pesa. Hoja ya msingi sio kuwa na fedha bali amezipataje” anasema na kuongeza kuwa kuna haja ya kuangalia amejaza nini katika fomu za maadili.
Alisema ikithibitika mali hiyo hailingani na mtiririko wa kipato chake hatua kali zichukuliwe dhidi yake ikiwa ni pamoja na kufilisiwa.
“Kama itabainika chanzo cha fedha hizo ni zile zinazolalamikiwa katika ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake ikiwa pamoja na muhusika kufilisiwa”alisema Ruhuza.
Mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam, Daniel Ngapani, alisema Waziri Maige ameudanganya umma wa Watanzania kutokana na kauli yake kuwa magari mawili yanaingiza dola 20,000.
Ngapani alisema yeye ana magari matano ambayo yanapeleka mizigo DRC mara mbili mwezi na malipo hayo bado hayafikii kiwango hicho.
“Kwa mwezi magari yangu husafiri mara mbili tu na kiasi ninachoingiza ni dola 2,500 hadi 3,000 sasa kwa Maige magari mawili tena anayakodisha haanapateje dola 20,000,” alisema Ngapani.
Ngapani amemtaka Waziri Maige kuwaeleza Watanzania ukweli juu ya kiasi anachoingiza kupitia magari hayo badala ya kuudanganya.
Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
3 comments:
ikiwa haya yanayozungumzwa ni madhubuti ,basi na wachunguzwe na wengine kwa taratibu hii hii na kuwekwa hadharani yale tunayohisi hayakubaliani na mwenendo mzima wa mapato na matimizi ya wakubwa.
Yaani kuwaondoa wezi madarakani kunahitaji sayansi ya maroketi. Wakati rais anawateua hakuitisha kikao. Leo kaitisha kikao kinachotumia kodi za walala hoi kujadili namna ya kufukuza wezi, wakati taarifa ya mkaguzi mkuu wa mahesabu anayo mkononi. Kinachonikera ni pale mabomu yakilipuka Mbagala na G'la mboto tunaombwa tuchangie. Wattoto hawana mishahara tunaombwa tuchangie. Nyumba za serikali zimeuzwa kwa wastani wa Sh. milioni kumi baada ya fufanyiwa matengenezo ya Sh. miliono ishirini kila moja. Sasa mawaziri inabidi waibe ili waweze kujinunulia nyumba za bei nafuu kwa dola 700,000.00 tu wakati bunge ltukufu linabariki bajeti zao kila mwaka. Hayo yote yanatokea ndani ya nchi ambayo inaongozwa na wasomi (PhD's) wengi kuliko taifa lolote duniani. Nyerere akifufuka leo atalia sana.
Ndugu,
Mimi niko Marekani hapa na ninanyumba kadhaa hapa na Bongo.Sijawahi kuiba au kuwa na Biashara ya muda mrefu.Ninafanya kazi kwa uaminifu na ninatumuia nyumba zangu kujenga nyumba nyingine nimefanya hivyo kwa miaka zaidi ya 20.
Tanzania,labda kuiba ndio utaweza kufanya hivyo. Nashukuru mungu mimi nilijiondokea zamani kabisa.
Rais wetu J Kikwete inchi immeshinda sana.Anaripoti ya wabadhirifu kwa nini asiwafukuze na kuwashotaki kwa ubadhirifu?Nchi anuza land na watu wake.Rais wetu yupo safarini kila wakati,tena kwa pesa za walipa kodi.Jamani tutaweza kweli kuwa na maendeleo?
Nyerere kweli akifufuka leo atalia na machozi ya damu.
Post a Comment