WANAFUNZI ambao ni wanachama wa Shirikisho la WanaCCM Vyuo vya Dar es Salaam, wamempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa nia yake ya kutaka kuwaondoa madarakani mawaziri wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu na kupendekeza uamuzi huo uchukuliwe haraka.
Wanafunzi hao jana waliandamana hadi katika Ofisi Ndogo za CCM, Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam wakiwa na mabango mbalimbali, baadhi yao yakisomeka ‘Wasaidizi wa JK wajibikeni kabla ya kuwajibishwa,’ ‘ Wezi wasisimamishwe wafukuzwe na kuchukuliwa hatua’, ‘CCM itadumu’ na ‘Viongozi wala rushwa watatupeleka kuzimu hatuwataki.’
Mengine yalisomeka ‘JK vunja ukimya, chukua hatua jenga chama na Taifa kwa ujumla,’ ‘Takukuru kuweni kama CAG’, ‘JK kawapa uhuru wa kutosha’ na ‘Nape chukua hatua la sivyo tuambie lini tuingie wenyewe maofisini.’ Katika ofisi hizo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi ya CCM, Nape Nnauye aliwapokea na kabla ya kuzungumza nao, walitoa risala yao.
Katika risala yao iliyosomwa na Mwenyekiti wa shirikisho hilo, Assenga Abubakari, wanafunzi hao walitoa mwezi mmoja kwa Serikali iwe imewachukulia hatua mawaziri wote waliohusika vinginevyo shirikisho hilo litawatoa lenyewe maofisini.
Nape awajibu Akijibu risala hiyo, Nape alisema kitendo cha Rais Kikwete kuruhusu kujadiliwa kwa uwazi ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ndicho kilichowezesha kuibuliwa na kubainishwa kwa viongozi wabadhirifu wa fedha za Serikali.
Alisema msimamo wa CCM kwa sasa ni kuisimamia Serikali na kuhakikisha mawaziri wote na wale wote watakaobainika kuhusika katika kashfa ya ubadhirifu wanawajibishwa.
Kwa mujibu wa Nape, tayari Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, imemshauri Rais Kikwete kuwa wahusika wote washughulikiwe na kufikishwa mahakamani.
“Kwa hili halina mjadala, naomba niwahakikishie kuwa waliohusika wote lazima wawajibike tena kisiasa kwa kuwa huku hakuna haja ya ushahidi, ikiwa mtu umetajwa kuwa ni mwizi lazima tukuweke pembeni,” alisisitiza.
Alisema pamoja na hayo NEC pia imemshauri Rais katika suala la kusuka upya Baraza la Mawaziri, lisichukue muda mrefu ili wahusika wote wakiwamo makatibu wakuu na watendaji waliohusika katika ubadhirifu uliobainishwa katika ripoti ya CAG, wanachukuliwa hatua.
Nape alisema kitendo cha ripoti za CAG kujadiliwa bungeni kwa uwazi, kina baraka ya Rais Kikwete na lengo likiwa ni kuhakikisha utendaji wa Serikali unafanyika kwa uwazi tofauti na zamani ambapo ripoti hizo zilikuwa zikiwasilishwa na kujadiliwa katika vikao vya ndani pekee.
Alisisitiza kuwa mara baada ya suala hilo kuibuliwa bungeni, wabunge walitoa mapendekezo yao, Kamati ya wabunge wa CCM nayo ilitoa mapendekezo yake ndipo NEC nayo ilipokutana na kuwasiliana na Rais juu ya hatua za kuchukuliwa dhidi ya wahusika wote.
“Rais tulipomuuliza alisema wazi kuwa hadi taarifa hiyo ya CAG ilipofikia ina baraka zake, napenda niwahakikishie kuwa CCM ndio iliyosaini mkataba wa kuongoza nchi kwa miaka mitano, kamwe haiwezi kunyamazia suala kubwa linalowatafuna wananchi kama hili,” alisisitiza Nape.
Katika Bunge la 10, mkutano wa saba uliomalizika jijini Dodoma hivi karibuni, iliibuka hoja nzito iliyowatupia lawama mawaziri kwa madai ya kutumia vibaya nyadhifa zao.
Ijumaa iliyopita, Kamati Kuu ya CCM ilikutana jijini Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete na kukubaliana na hoja ya Rais Kikwete ya kutaka kufanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri. Kutokana na hiyo, inatarajiwa kuwa wakati wowote Rais Kikwete atafanya mabadiliko hayo ikiwa ni mara ya kwanza tangu aliposhinda muhula wa pili na wa mwisho wa uongozi wake, Oktoba 31, 2010.
Miongoni mwa mawaziri wanaotajwa katika kashfa mbalimbali baada ya kutoka kwa ripoti ya CAG ni Waziri wa Fedha Mustafa Mkulo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, Waziri wa Viwanda na Biashara Cyril Chami na Naibu wake, Lazaro Nyalandu. Mawaziri wengine wanaohusishwa na ubadhirifu huo ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja, Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa George Mkuchika na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige
Habari Leo
No comments:
Post a Comment