ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 1, 2012

Aungua na kufa katika mchezo wa kupika

MTOTO mwenye umri wa miaka miwili, Zakaria Ayubu ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Land Makuti katika Tarafa ya Chita wilayani Kilombero, amefariki dunia baada ya kuungua kwa moto wakati akijipikia. 

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Adolfina Chialo, mtoto huyo alifariki Aprili 27, mwaka huu saa 12 jioni kijijini hapo. 

Kamanda Chialo alisema mtoto huyo akiwa na watoto wenzake, walikuwa wakicheza mchezo wa kupika karibu na nyumba ya nyasi ambapo moto ulishika nyasi na kuanza kuunguza nyumba; na hatimaye mtoto huyo kuungua baada ya kushindwa kujiokoa. 

Katika tukio jingine, mkazi wa Viwanja 60 Ifakara wilayani Kilombero, Salum Rashidi (14), amefariki dunia baada ya kuzama katika kivuko cha mto Kameta Lumemo. 

Kamanda Chialo alisema Rashid alikutwa akielea katika mto huo Aprili 29, mwaka huu saa 4 asubuhi ambapo taarifa za awali zilidai kuwa alienda kuoga katika mto huo ambako alizidiwa na maji na kuzama. 


Katika tukio la tatu, mkazi wa Kijiji cha Lubungo Morogoro Vijijini, Musa Paga (28) amefariki dunia baada ya kuzama katika bwawa la maji alipoenda kuoga. 

Chialo alisema Paga alienda kulima katika shamba lake Aprili 25, ambapo baada ya kumaliza kulima, aliamua kwenda kuoga katika bwawa lililokuwa karibu na shamba lake, ambako alizama na mwili wake kuonekana Aprili 27, mwaka huu saa 12 jioni akiwa anaelea katika bwawa hilo. 

Aidha, Augustino Nickolaus (72) mkazi wa Melela Wilaya ya Mvomero, amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa baada ya kugongwa na pikipiki. 

Kamanda huyo alisema tukio hilo limetokea Aprili 27, mwaka huu saa 11 jioni katika maeneo la Melela Barabara ya Morogoro - Iringa ambapo pikipiki aina ya Honda ikiendeshwa na Paramise Fumito, ilimgonga mtu huyo na kusababisha kifo chake akiwa anapatiwa matibabu hospitalini.


Habari Leo

No comments: