ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 1, 2012

Mwanamke akatwa mapanga kwa kuwa na macho mekundu

MWANAMKE mmoja wa kijiji cha Isonda kata ya Nyugwa ,tarafa ya Msalala wilayani Geita, aliyetambuliwa kwa jina la Tabu Shitunguru (55) amevamiwa nyumbani kwake na kukatwakatwa mapanga. 

Mwanamke huyo kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Geita akiuguza majeraha yaliyotapakaa mwili mzima, akiwa amekatwa vidole vyake sita kati ya kumi vya mikono yote miwili. Vidonda vingine vipo shingoni na mgongoni . 

Akisimulia mkasa huo mwanamke huyo alisema siku hiyo akiwa nyumbani na mwanawe wa kiume aliyemtaja kwa jina la Robert Mathias baada ya kumaliza kula nje ya nyumba yao majira ya saa 2 usiku, ghafla alishangaa akivamiwa na mtu na kumcharanga mapanga shingoni. 


“Wakati tumekaa pale nje kijana wangu akiwa anakula mimi tayari nilikuwa nimemaliza kula chakula, nikashtukia mtu akinivamia na kuanza kunikata mapanga shingoni, alinikata panga la kwanza shingoni kisha mgongoni nikaanguka chini sikujua tena kilichoendelea hadi juzi nilipojikuta niko hapa hospitalini nikiwa nimefungiwa haya mabandeji mgongoni, kichwani, shingoni na mikononi…’’ alisema mwanamke huyo.

Akizungumzia chanzo cha kujeruhiwa kwake mama huyo alisema kwamba wakati mkataji akimkata kwa mapanga alimwambia kwamba aache vitendo vya uchawi, huku akimsisitiza kwamba malipo ya kazi yake hiyo ya uchawi ni kifo. 

Majeruhi huyo alisema kwamba hajawahi kujihusisha na vitendo vya kichawi katika maisha yake ingawa kwa miaka mingi amekuwa akisikia akituhumiwa kwamba yeye ni mchawi kutokana na macho yake kuwa mekundu. 

“Kilichoniponza ni haya macho yangu mekundu….nimekua nikisikia watu wakisema kwamba mimi ni mchawi, lakini naamini Mungu ni shahidi yangu mkuu kwamba siujui uchawi ukoje na katika maisha yangu sijawahi kujihusisha na vitendo hivyo, na kama ningekuwa mchawi kwa nini nisingeutumia hata kwa mke mwenzangu ambaye ameolewa hivi karibuni na mume wangu…?’’ Alisema na kuhoji mwanamke huyo. 

Daktari anayemtibu mwanamke huyo Dk. Daniel Izengo akizungumzia hali ya mwanamke huyo alisema amejeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake na hasa mgongoni, na shingoni hali ambayo imesababisha baadhi ya mishipa kukatika na hivyo kupoteza nguvu za kufanya kazi. 

Mkuu wa Wilaya ya Geita Filemon Shelutete akizungumzia tukio hilo alikiri kulifahamu na kueleza kuwa kujeruhiwa kwa mwanamke huyo kumeongeza idadi ya wanawake wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia kwa kuuawa ama kujeruhiwa kutokana na imani za kishirikina. 

Alisema tangu Mwezi Januari Mwaka 2011 hadi kufikia mwishoni mwa mwezi wa Aprili mwaka huu jumla ya wanawake 21 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia kwa kukatwa kwa mapanga kwa kisingizio cha kuwa wachawi, ambapo 11 kati yao wamepoteza maisha huku 10 wakipata vilema vya maisha. 

Alisema kumekuwepo na tabia ya wanawake wenye macho mekundu katika wilaya hiyo kuuawa kwa kukatwa kwa mapanga kwa kisingizio cha kuwa ni wachawi, hali ambayo aliipinga vikali na kueleza kwamba umefika wakati ambapo wananchi wanapaswa kubadilika na kuachana na tabia za kizamani ambazo zimekuwa zikisababisha madhara makubwa kwa jamii.


Habari Leo

No comments: