ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 26, 2012

Mapenzi ni fursa, iheshimu kwa maana haiji mara mbili



Na Luqman Maloto
Nikuombe msomaji wangu kwamba unaposoma makala haya, soma kwa mtindo wa katikati ya mstari (between the line). Kuna somo kubwa mno kwenye mada hii kwa sababu wengi wapo kwenye mateso makubwa ya kimapenzi kutokana na makosa yao wenyewe.
Ukisoma ujasiriamali, utaelekezwa kwamba mafanikio yako yatatokana pia na namna ulivyo na nidhamu katika fursa unazopata. Inawezekana ukawa na bahati kwenye maisha lakini utabaki kuwa si lolote endapo hutatumia nafasi zako vizuri.

Kama maisha, ndivyo yalivyo mapenzi. Hayatanyooka, wala hayatakaa vema upande wako ikiwa hutakuwa na heshima kwa fursa utakazopata. Si suala la ujana au kujipanga, muhimu kwako ni kuheshimu kile kilichopo jirani yako. Zingatia: Mapenzi ni changamoto nzito.
Ukichezea penzi lako leo kwa sababu unazozijua wewe, tambua kwamba halitakaa kwako daima. Kama yalivyo maisha kwamba yapo mfano wa kioo, ukiyachekea yanacheka, ukiyanunia nayo yananuna. Ndivyo na mapenzi yalivyo. Ukiyachezea, nayo yatakuchezea kweli.
Unapaswa kuyaheshimu. Heshima ya mapenzi ni kumtunuku mapenzi ya kweli huyo ambaye amekujia na mapenzi yake. Umethibitisha anakupenda kweli, sasa kinachokuwasha nini mpaka uunyanyase moyo wake? Fumba macho, mara nyingi bahati huwa haiji mara mbili.
Inawezekana mwenzi wako wa leo ndiye mwenye mapenzi ya kweli. Ila wewe unausimanga moyo wake kwa sababu hana fedha. Unakwenda kuabudu wenye uwezo. Fimbo ya mbali haiui nyoka, kwa hiyo unaweza kufanya lolote, naye hatakuwa na cha kufanya zaidi ya kumuachia machozi na sononeko.
Kuna watu hawajiulizi hili; huyo anayekuja kwako akitumia fedha kukuteka kwenye himaya yake, ameshatumia jeuri hiyo kwa wangapi? Endapo utaujua ukweli, utakuja kufahamu kwamba ni wengi aliwanasa kwa sababu alitanguliza fedha.
Weka akilini kwamba haji kwako kwa sababu anakupenda ila anayo jeuri kuwa hutapindua kutokana na fedha alizonazo. Sasa basi, unapomkubalia unamfanya aongeze kiburi. Kesho atatupa ndoano kwa mwingine na huo ndiyo utakuwa mwendo.
Atakutamani kwa sababu ya muonekano wako, kwa hiyo kutokana na kiburi cha fedha alichonacho, kesho akimuona mwingine atakayemtamanisha, atatumia fedha zake kumnasa. Hii ina maana kuwa mkondo wako, watapita wengi. Mwisho kabisa, utabaini kwamba uliingia katika msafara wa kenge.
Atapita kwa wenye tamaa za fedha, nawe utakuja kuingia humohumo. Hii ndiyo sababu ya kusema utajikuta umeunga msafara wa kenge. Wewe utasema unajiheshimu lakini huyo uliyeangukia kwake, hachagui.
Popote kambi, baadaye unapata jawabu kwamba umechangia mwanaume na machangudoa wengi wa mjini.
Tatizo siyo mvuto wako, wapo machangudoa wengi mjini na wanavutia kwelikweli. Kama kavutiwa na wewe na katumia ngawira kukunasa, inashindikana vipi kuvutiwa na machangudoa wengine, nao akatumia fedha kuwanasa? Tena wao si gharama, kwa maana ndiyo kazi yao.
Vilevile kwa mwanaume, atampuuza mtu anayempenda na kumvaa mwingine anayemuona anavutia zaidi. Wengi wamefanya hivyo bila kujua kwamba hao wanaovutia barabarani, asilimia kubwa ni magubegube. Unahitaji mwandani wa maisha yako, tuliza akili.
Sikukatazi kutupa ndoano, ila jaribu kufikiria mara mbili. Uliyenaye hakutoshelezi? Kumuacha mpenzi wa kweli na kujishughulisha na wengine ni sawa na mfano wa mtu aliyepoteza almasi, wakati alipokuwa ‘bize’ akitafuta mawe. Usilie kama wenzako, tuliza akili leo.
Kuna watu wanateseka leo. Wanadai wana mkosi. Eti, mapenzi yanawachapa bakora kwamba hawana bahati nayo. Kama na wewe upo kwenye kundi hili, fumba macho halafu ufikirie ulipotoka. Je, hukumuacha aliyekupenda kwa dhati? Hukuchezea moyo wa yule aliyekuwa anakujali?
Kama jibu ni ndiyo, basi hutakiwi kulia. Mapenzi yalivyo, kupata mwenye moyo mkunjufu katika kupenda ni bahati nasibu. Hivyo basi, kama ulimchezea, ni zamu yako kuteseka kwa maana uliyachezea mapenzi. Ulimpiga teke anayekupenda, sasa unahangaika na wasiokupenda. Wanakuinjoi tu.
Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

No comments: