Mhe.Balozi Mwanaidi Sinare Maajar akiwa na Mhe. Dan Boren, Mbunge wa
Bunge la Marekani kutoka Oklahoma.
Mhe.Balozi Maajar akiwa katika picha ya pamoja na Mbunge Dan Boren,
Mkurugenzi wa Bunge, Bi.Hilary Moffett,na kushoto na kulia na Bibi Lily
Munanka Mkuu wa Utawala Ubalozini na Afisa Ubalozi Bw. Suleiman Saleh.
Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico, Mhe. Mwanaidi Sinare Maajar,
Jumatano Mei 9, 2012 alimpokea Ubalozini, Mhe. Dan Boren na kufanya naye
mazungumzo ya uanzishwaji wa Tanzania Caucus katika Bunge la Marekani
ambapo Tanzania itakuwa imepata mtetezi na msemaji bungeni humo kila
linapotokea jambo linalohusu Tanzania.
Mhe. Boren ni mbunge wa Bunge la Marekani kutoka Wilaya ya Pili, Jimbo la
Oklahoma, amehamasisha na hatimaye kuanzisha kundi la wabunge wenye
mapenzi na Tanzania, kamati ndogo (caucus) ya kuisemea Tanzania kwenye
Bunge la Marekani.
Mhe. Boren ambaye ni mbunge kutoka Chama Tawala cha Democrat ameasisi
Kundi hilo hilo akishirikiana na wabunge wenzake kadhaa wa chama chake na
wengine kutoka Chama cha Republican kutokana na kufurahishwa kwao na
juhudi za Serikali ya Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika kuimarisha
demokrasia, utawala bora pamoja na juhudi za kimaendeleo katika sekta za
uchumi, nishati, kilimo na hifadhi ya mazingira.
Katika ziara yake hapa ubalozini Mhe. Boren aliyeambatana na Bi. Hilary
Moffett, Mkurugenzi wa Sheria Bungeni, alimhakikishia Mhe. Balozi Maajar
utayari wake wa kuisaidia Tanzania katika juhudi zake hizo.
Aidha alibainisha kwamba Tanzania ina changamoto nyingi sana mbele yake na
hivyo kuwepo kwa sauti mpya ya kuisemea katika Bunge la Marekani ni jambo
ambalo analiona litakuwa na manufaa makubwa kwa nchi.
Sambamba na hilo, Mhe. Boren alibainisha kwamba Tanzania imekuwa ni moja
ya nchi ambazo Serikali ya Marekani inaziangalia kwa umakini kama mfano wa
nchi bora na hivyo ameona ni vyema naye akaunga mkono juhudi hizo za
Serikali ya Rais Barack Obama.
Kwa upande wake, Mhe.Balozi Mwanaidi Sinare Maajar alifurahishwa na
kufarijika na ujio wa Mhe. Boren Ubalozini na kumueleza kwamba
atashirikiana naye bega kwa bega na kuahidi kwamba muda wowote
atakapohitajika kukutana na kamati hiyo ya Bw. Boren yupo tayari.
Mhe. Maajar alimshukuru Mhe.Boren kwa mwaliko wake kutembelea Jimbo la
Oklahoma ili Tanzania ipate kueleweka zaidi na hivyo kufungua pazia la
ushirikiano katika sekta mbali mbali za Uchumi, Kilimo, Nishati na Utalii.
Imetolewa na:
Ubalozi wa Tanzania Washington DC
1232 22nd Street NW, Washington DC 20037
www.tanzaniaembassy-us.org
5.11.2012
Ubalozi wa Tanzania Washington DC
1232 22nd Street NW, Washington DC 20037
www.tanzaniaembassy-us.org
5.11.2012
No comments:
Post a Comment