ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 14, 2012

UKITAKA SALAMA KWENYE MAPENZI, USIFANYE MAKOSA HAYA-6



MPENZI msomaji wa makala haya, leo naendelea na vipengele vilivyosalia ambavyo naamini ukivinzingatia kwa makini hautafanya makosa kwenye mapenzi ambayo yatamuumiza mwenzako. Tuwe pamoja.
Wengi huishi na maumivu kwa kuona kwamba anachowaza, hakipo kwa mwenzi wake. Mathalan, unapenda mpenzi wako akununulie zawadi, hilo lirekebishe kwa kumuelekeza kwa upole.

Mwambie: “Mpenzi wangu, napenda sana ile simu.” Zungumza hivyo halafu ukae kimya. Naye akili inafanya kazi, kwa hiyo kama uwezo unaruhusu atakununulia. Jiepusha na tabia ya kuomba jamvi msibani. Pengine hana lakini wewe unalaumu kuwa hakujali ndiyo maana hajakununulia.
Kosa lingine kubwa ambalo wengi hulifanya ni kufananisha uhusiano wa watu wengine na kutaka kulazimisha uhusika wao ufanane na wenu. Mfano; mtu anaona jinsi rafiki yake anavyotendewa na mpenzi wake, kwa hiyo naye anatamani iwe hivyo. Ni binadamu wawili tofauti, ni ngumu kuwa na tabia za kufanana. Uvumilivu unahitajika.
KUKOSEA TAFSIRI
Binadamu kila mmoja kwa namna yake, anayo njia ya kuonesha ishara za mapenzi. Hata hivyo, ipo wazi kuwa wengi hufanana pale wanapochachawa kutokana na kuzidiwa na hisia za kupenda. Kila mmoja anaruhusiwa kupenda lakini pupa zikikuzidi, ni rahisi kuonekana mapepe. Haipendezi kuonekana hivyo.
Ieleweke kuwa ipo jamii ya watu ambao wanaweza kupenda lakini wasioneshe waziwazi hisia zao.
Wakakomaa kisabuni, wewe ukadhani hawapendi kumbe wanaumia ndani ya nyoyo zao. Hili likae kichwani kwako, usije ukafanya kosa kubwa la kukosea tafsiri, matokeo yake uhusiano wako ukakaa tenge.
Tambua pia kuwa ipo jamii ambayo inaweza kuonesha waziwazi kwamba wanapenda kumbe hakuna lolote. Ni uchangamfu tu uliopo ndani yao. Anaweza akawa anakujali, ukiwa mbali anakupigia simu. Ukiwa na tatizo anajitoa kukusaidia lakini hiyo haina ishara kuwa anakuhitaji kimapenzi. Ni mambo ya urafiki tu hayo.
Hivyo basi, kabla hujaingia kwenye uhusiano wa kimapenzi, hakikisha huchanganyi mambo. Usimtafsiri mtu kwa alama za juujuu. Fanyia kazi kile unachohisi. Usije ukachukia kwamba mtu unayempenda anakuchukia, wakati kumbe mwenzako ndiyo swaga zake. Lazima aweke madoido kidogo kwa kuhofia kuonekana mwepesi.
Wala usije ukadandia mti ambao siyo kwa kudhani unapendwa, wakati mwenzako ni geresha tu! Chukua hatua sahihi, kabidhi moyo wako kwa yule anayekupenda, si kwa sababu akikuona anakuchekea na kujishaua, la hasha! Kaa kwa yule ambaye amedhihirisha mapenzi ya kweli kwako. Ukikosea tafsiri, utaumia mbele ya safari.
KUTARAJI UHUSIANO UKUPE FURAHA PEKEE
Ni vizuri kutaraji furaha kwenye uhusiano wako, kwani ndivyo inavyotakiwa. Kosa linalojitokeza hapo ni kuwa wahusika huwa hawapigi mahesabu ya changamoto ambazo hujitokeza. Ni vizuri kuyabeba mapenzi katika sura halisi kwa maana zipo siku ambazo hutafurahi. Ni changamoto.
Tatizo ni kwamba kila mmoja anapoyatafakari mapenzi, huwaza kuwa mpenzi wake ndiye atayabadilisha maisha yake na kumfanya awe na furaha. Hata siku moja hawezi kwenda mbele na kuutesa ubongo wake, akiwaza na kuwazua jinsi ambayo yeye anaweza kufanya ili kumpa furaha na amani mwenzi wake.
Angalau wanaume wachache hufikiria mema kwa ajili ya wapenzi wao lakini kwa wanawake, tafiti zinaonesha kwamba asilimia 98 ya wanawake kabla ya kuingia kwenye uhusiano, husumbuliwa na ubinafsi kwa sababu huwaza mambo ambayo wao watafanyiwa na wapenzi wao na siyo wao kuwafanyia.
Kwa kuweka hoja zote kwenye kapu moja, ni vizuri kila mmoja akawekeza furaha yake kwa mwenzi wake. Ni makosa makubwa kutegemea matunda ambayo hujafanya jitihada zozote kuyapanda na kuyastawisha.

www.globpublishers.info


No comments: