ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 4, 2012

UMESHINDWA KABISA KUWA MWAMINIFU KWA MPENZI WAKO? - 2

UAMUZI wako wa kuchagua Gazeti la Ijumaa hasa kwenye kona hii ya Let’s Talk About Love ni wa busara sana. Nakuhakikishia huna cha kupoteza. Thamani ya vilivyomo humu ndani ni kubwa zaidi ya bei ya gazeti!
Hongera sana! Rafiki zangu, tunaendelea na mada yetu ambayo ilianza wiki iliyopita. Ni mada yenye changamoto nyingi sana, nilipata maoni mbalimbali kutoka kwa wadau wakijaribu kuelezea fikra zao.

Nazungumzia suala la uaminifu, wapo watu ambao kwa hakika wameshindwa kabisa kuwa waaminifu. Si kwamba hawapendi kuwa waaminifu, hapana! Wanapenda sana, lakini wanajikuta wameshasaliti.
Kuna dondoo ambazo nilianza kuzizungumzia wiki jana. Kwamba la kwanza kabisa, uweke nia moyoni mwako kuwa unataka kuwa mwaminifu. Kumbukeni kwamba, hapa ninazungumza na wale ambao wanajijua huwa wanateleza mara kwa mara, lakini si kwa hiyari yao – hawapendi tabia hii.
Kama wewe ni msaliti na huna mpango wa kuacha, hata ukipasuliwa kichwa na maandishi haya kuingizwa kwenye ubongo wako, hutaweza kuacha. Jambo kubwa ni wewe kwanza kuwa na nia.
Lingine nililogusia wiki iliyopita ilikuwa ni kutawala kinywa chako. Maneno yako yanawaweza kukuponza na kukuingiza kwenye usaliti hasa kama unazungumza mambo ya hovyo mbele ya marafiki wa jinsia tofauti na yako.
Kwa kufanya hivyo, kunajenga mazoea ambayo baadaye yanabebwa na ‘utani’.
Kwa kuwa rafiki yako atakuwa anajua kuwa mnataniana, ni rahisi kukutongoza au kukutamkia maneno yanayoashiria mapenzi, ukiingia anakuchukua, lakini ukiwa mkali anakuambia alikuwa anafanya utani. Mpo hapo marafiki? Hebu twende kwenye vipengele vinavyofuata;
NIDHAMU YA MAWASILIANO
Unaweza usielewe vyema kipengele hiki, lakini kina maana kubwa kuliko kawaida. Suala la nidhamu ya mawasiliano, lina maana kubwa sana katika eneo la uaminifu.
Kwanza usikubali kutoa namba yako ya simu hovyo, hasa kwa watu ambao una uhakika hutakuwa na haja ya mawasiliano nao mara kwa mara. Epuka kabisa kukubali urafiki kutoka kwa watu usiowafahamu.
Hapa nitakwenda mbali zaidi, kuna tabia ya baadhi ya watu kutunga na kusambaza meseji zenye viashiria vya mapenzi. Mtu anatunga upuuzi wake, halafu anamtumia rafiki yake. Hii ni tabia inayokaribisha usaliti.
Jiulize, ni kwa nini amekutumia meseji yenye ujumbe wa mapenzi? Meseji zimejaa maneno ya kipuuzi tupu! Kwa bahati mbaya au nzuri, kuna watu waliwahi kujaribu kunitumia meseji za namna hiyo, sikujibu. Kuna wengine niliwaambia wazi kuwa sipendi kutumiwa meseji za namna hiyo.
Utakuta mwingine, akitumiwa ndiyo kwanza na yeye ‘anamfowadia’ yake. Ili iweje? Kwani huna kazi ya kufanya hadi uanze kutunga meseji za matusi? Ni kweli umekosa kabisa mambo ya kufikiria?
Afadhali wale wanaotumiana vichekesho, maana kucheka ni afya! Epuka kabisa mkumbo huu, maana husogeza kwenye usaliti. Huwezi kuona hilo mapema, lakini baadaye utagundua ukiwa tayari umeshauvaa mkenge!
Jambo lingine; Ili uweze kuwa kwenye himaya ya uaminifu, hifadhi jina la mpenzio/mumeo/mkeo kwa majina ya kimapenzi. Acha ‘kumsevu’ kwa jina lake. Andika ‘My Ice’, ‘Sweetie’ ‘Baby’, ‘Darling’ na mengineyo. Kwanza inakutengeneza kisaikolojia kuwa upo katika himaya ya mtu.
Yupo anayekupenda na kukuthamini. Hata simu inapoita mbele za watu, halafu mtu akafanikiwa kuiona anaona wazi kwamba una mtu unayempenda.
Kama simu yako ina kamera, weka picha ya mpenzi wako kwenye kioo cha simu. Unajua utakuwa unamuona mara kwa mara, utajikuta mapenzi yako yanazidi kwake, halafu usaliti unakuwa mbali na wewe. Huo ndiyo ukweli.
Linaweza lisionekane kama ni jambo muhimu, lakini kwa hakika kama mtu akifuata hili, anajiweka kwenye uaminifu kwa asilimia kubwa sana. Twende kwenye kipengele kinachofuata.
MITANDAO YA KIJAMII
Utafiti usio rasmi unaonesha kwamba, pamoja na kwamba mitandao ya kijamii imesaidia kwa kiasi kikubwa sana kurahisisha upatikanaji wa taarifa, kuendesha mijadala na kukuza ufahamu wa mambo mengi, suala la mapenzi limetajwa!
Utakutana na mtu Facebook (mfano), mmekuwa marafiki, lakini siku ya siku anaanzisha mambo ya mapenzi.
Kwa sababu umeshakuwa naye karibu kwa muda mrefu, umekuwa wazi kwake kwa muda mrefu ni rahisi kuanguka!
Nafasi yangu ni ndogo, wiki ijayo nitaendelea hapa kwenye kipengele cha mitandao ya kijamii. Utaona jinsi inavyoharibu uhusiano/ndoa za wengi kwa wasio waangalifu. Si ya KUKOSA.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na Who is Your Valentine? vilivyopo mitaani.

No comments: