WAKILI anayemtetea msanii Elizabeth Michael ‘Lulu’ anayedaiwa kumuua msanii Steven Kanumba, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ihamishie kesi hiyo kwenye mahakama ya watoto kwa kuwa mteja wake ana umri chini ya miaka 18.
Upande wa mashitaka ulieleza kushangazwa na ombi hilo kwa madai kwamba mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambako kesi hiyo inatajwa haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo ya mauaji.
Wakili wa Serikali katika kesi hiyo, Elizabeth Kaganda amedai kwamba kesi hiyo ipo hatua ya upelelezi ambao haujakamilika na kwamba miongoni mwa vitu wanavyovichunguza ni pamoja na umri wa mshitakiwa huyo.
Katika kesi hiyo iliyotajwa leo, Wakili Kened Fungamtama mbele ya Hakimu Agustina Mmbando ameomba mahakama imuone Lulu kuwa hana umri wa miaka 18.
Fungamtama alidai mahakamani kwamba Lulu ana umri wa miaka 17.
Aliendelea kudai kwamba upande wa mashtaka haujawasilisha mahakamani hapo pingamizi lolote kuhusu umri huo hata pale mshitakiwa alipoieleza mahakama kuwa ana miaka 17 na si 18.
Wakili huyo wa utetezi aliwasilisha cheti cha kuzaliwa alichodai kuwa ni cha Lulu ili mahakama hiyo ijiridhishe kuhusu umri wake.
Wakili wa Serikali Kaganda alipinga ombi hilo na kudai kuwa ameshtushwa na ombi hilo kwa kuwa kesi imekuja kutajwa kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza ombi lolote.
Kwa mujibu wa Kaganda, katika cheti cha kuzaliwa kilichooneshwa mahakamani hapo na Fungamtama, hawawezi kukiamini kwani kina jina la Dayana Elizabeth wakati mshtakiwa anaitwa Elizabeth Michael.
"Mheshimiwa hakimu tunaomba tupewe hicho cheti tukichunguze, pia tupewe muda tuchunguze zaidi kuhusu umri wake, kama itabainika ana miaka chini ya 18 mshitakiwa ana haki zote za kushitakiwa katika mahakama ya watoto," alidai Kaganda.
Akitoa uamuzi wa maombi hayo, Hakimu Mmbando aliutaka upande wa utetezi kusubiri kesi hiyo itakapowasilishwa katika Mahakama Kuu ndipo wawasilishe maombi hayo kwa kuwa mahakama hiyo hivi sasa haina mamlaka.
"Mahakama hii inajua kuwa shauri lililo mbele yake ni la mauaji, hatuna mamlaka ya kutoa uamuzi wowote kwa sasa, maombi yoyote yafanyike Mahakama Kuu," alisema Mmbando.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 21 mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Habari Leo
3 comments:
Mdau mmoja alisema kesi zetu huwa zinaahirishwa mpaka unaweza kuwa mzee ndio ianze kusikilizwa... pole sana lulu sasa hivi watatumia zile pati ulizofanya kusema una umri mkubwa na intavyu zote zitatoka... pole mdogo wangu omba sana mastaa wenzio (kama bado wapo) wakushike mkono.
wahenga walisema "rafiki mkia wa fisi .....
Lawyers will always have their views but dont forget its business, never personal to them.
Lawyers' business is to make sure their clients win their cases. That means lieying is still a part of their job.
Post a Comment