Na Luqman Maloto
Leo tunaendelea na mada ya tatizo la wivu kwa wapenzi na namna ya kuondokana nalo. Tuendelee kuanzia pale tulipoishia wiki iliyopita.
Unajidharau? Unakosea sana, muonekano wa juu hubadilika kutokana na wewe mwenyewe unavyoamua na kujipanga. Tatizo ni nguo? Mbona hivyo ni vitu vya kununuliwa? Unayo nafasi ya kutafuta na kupata, kwa hiyo punguza kuchachawa, wekeza upendo kwa sababu ndiyo dawa ya kila kitu.
Jambo lingine ni kuwa hutakiwi kumlazimisha mwenzi wako kuwa kama unavyotaka wewe lakini si vibaya kumshauri akawa na muonekano ambao unakuvutia. Labda anavaa akiwa anaacha wazi maungo yake, haitakiwi upandwe na jazba kisha kumtolea maneno makali, kaa naye mjadili mavazi sahihi.
Mapenzi ni diplomasia, hivyo wewe zungumza halafu muachie nafasi na yeye aseme linalompendeza. Hakikisha hutumii maneno ya kuudhi katika mazungumzo yenu. Vilevile na yeye anapaswa kudhibiti hasira zake. Mwisho mnakubaliana kwa upendo. Vuta picha inavyokuwa, mapenzi yanataka hivyo.
3. UNARUHUSIWA KUULIZA
Kuna jambo linakutatiza au umeona mwenzi wako anawasiliana na watu ambao huwaelewi? Inawezekana pia akawa karibu na mtu wa jinsi yako, kwa hiyo unahisi kwamba unaweza kuibiwa. Suluhu hapo siyo kukaa na msongamano wa vitu kichwani, keti naye ukiwa na hali ya utulivu kisha muombe akupe ufafanuzi.
Kama una hasira usizungumze naye kwa sababu inaweza kuharibu maana. Siku zote, mazungumzo ya uhusiano wa kimapenzi, huendeshwa kwa njia ya upendo. Kama unahisi mbele utapandwa na jazba endapo hutapokea majibu mazuri, vema ungoje siku utakayokuwa na utulivu wa kutosha.
Usiyafanye mazungumzo yenu kuwa mahojiano. Jiweke kwenye kipengele cha mapenzi, kwa hiyo wewe siyo polisi. Pengine majibu yake yakawa siyo ya kunyooka, unachotakiwa kufanya ni kumuelewa au pale anapokuwa anasitasita, jaribu kumuongoza kuelekea kwenye jibu ambalo litasaidia ujenzi wa uhusiano wenu.
Hasira, jazba, ukali na mikunjo ya sura yako, vinaweza kumfanya ashindwe kukupa majibu sahihi. Kutokana na woga ambao atakuwa nao baada ya kuisoma ndita iliyopo usoni mwako, si ajabu akakuongopea. Ni kosa kubwa mno kuwa na uhusiano ambao unadumishwa na uongo. Tafuta uelekeo sahihi wa penzi lako.
Wewe ni muelewa, kwa hiyo unafahamu maana ya ‘kuchati’. Hoja zako zijenge katika mtindo wa majadiliano. Zungumza na yeye azungumze. Tena apewe nafasi anayoona inastahili, asije akasema ulimnyima uhuru, kwa hiyo alishindwa kujibu inavyotakiwa kwa sababu ulimkomalia kupita kiasi.
Hata hivyo, unashauriwa kuachana na vitu vingi, badala yake unatakiwa kukusanya yote uliyopokea kuhusu mwenzi wako, mengine unapuuza halafu yale machache unayoona yanatakiwa majibu, ndiyo uyawasilishe kwake akupe majibu. Kumbuka kwamba unatakiwa uelewe kwa urahisi kile anachokwambia.
Tabia ya kukusanya mambo mengi na kutaka majibu kwa wakati mmoja ni mbaya, kwani hutoa picha kuwa umemkamia kwa maswali, kwa hiyo mwisho wake atakuona una gubu. Ishi kwa upendo, tatua mambo yako kidiplomasia. Usikubali uonekane una gubu, kwani hiyo ikipita itakufanya mapenzi yakushinde.
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info
1 comment:
Wivu hauna dawa mzee wa vijimambo.
Post a Comment