MKAZI wa Tandale Uzuri katika Manispaa ya Kinondoni, aliyetambuliwa kwa jina la William Robert (23) amekufa baada ya kunaswa na umeme katika kiwanda cha A.M Trailer kilichopo Mwenge Efatha, Dar es Salaam.
Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 12 jioni, wakati marehemu alipokuwa akimsogelea fundi wa mashine ya kuunganisha vyuma kiwandani hapo.
Kenyela alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa eneo hilo lilikuwa na maji maji na waya wa kebo ya umeme ulikuwa chini hivyo kusababisha shoti ya umeme.
“Robert alinaswa na umeme wakati akimsogelea fundi mashine ya kuchomelea, ndipo akanaswa na shoti ya umeme na kufariki papo hapo,” alisema.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, wakati uchunguzi zaidi ukiendelea. Aidha matukio kama haya yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika vituo vingi vya kazi kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, na nyawa kuwa wazi.
No comments:
Post a Comment