ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 18, 2012

Chadema yaalika wagombea


Katika jitihada za kujiandaa na uchaguzi mkuu wa 2015 Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewataka wanachama wake wenye nia ya kugombea ubunge na udiwani kuwasilisha barua za maombi, picha, vyeti,  wasifu na jimbo wanalotaka kugombea kwenye Ofisi ya Katibu Mkuu, tayari kwa maandalizi.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema jana na kuwaagiza wanafunzi ambao ni wanachama wa Chadema wanaohitimu mwaka huu katika vyuo vikuu vya Mkoa wa Dodoma kufanya hivyo mara moja.



Akihutubia katika mahafali ya kuwaaga wanachama hao wanaosoma vyuo vikuu vya Dodoma, St. John’s na Chuo cha Biashara (CBE), Mbowe, alisema kila anayetaka kugombea awasilishe maombi na kwamba mwaka 2015 wagombea watakuwa wengi kwa kila jimbo ili kuleta ushindani.

Alisema  taarifa za wagombea hao zitafanywa kuwa siri na watakaojitokeza kugombea 2015 watapata mafunzo maalumu ya uongozi, kampeni na pia watapewa ajenda za kuzungumzia majukwaani wakati wa kampeni.

“Kama CCM ilidhani kuwa mwaka 2015 kutakuwa na jimbo au kata ambalo mgombea atapita bila mgombea, safari hii wameula wa chuya. Tumefanya operesheni Mtwara na Lindi,  tutaendelea na operesheni Dar na Pwani kisha tutaendelea Dodoma, Morogoro na Singida.

“Tunataka kujenga mtandao wa chama ngazi za chini, vijijini na mtaani kama CCM inadhani tunacheza makidamakida  watashangaa,” alisisitiza Mbowe na kuongeza kuwa lengo ni kuwatambua na kuwajenga viongozi mapema.

Katika mkutano huo, Mbowe aliwaambia wanachama wa Chadema vyuoni (Chaso) Mkoa wa Dodoma kuwa CCM inawanyanyasa wanafunzi wanaoiunga mkono Chadema na pia inanyanyasa wafanyakazi na wafanyabiashara wanaoonekana kushabikia chama hicho.

MIKAKATI YA CHADEMA

Mbowe ametangaza kuwa katika uchaguzi mkuu wa 2015 Chadema haitapokea 'maskrepa' yaliyokosa nafasi katika vyama vingine, biashara ya kupokea watu waliokosa nafasi katika vyama vingine ilikuwa 2010.

Alisema tabia ya kukimbilia meli dakika za mwisho ilikuwa zamani na kwamba uchaguzi ujao hawatakubali waliokosa fursa kwa vyama vyao kukimbilia Chadema.

Mipango yao ni  kupata wabunge na viongozi bora watakaopimwa kwa dhamira, uwezo na  uwajibikaji kwa chama.

“Wafanyakazi wanatishiwa kufukuzwa kazi na wafanyabiashara wanafilisiwa na kubambikiwa kodi kisa wameonekana kushabikia Chadema,” alisema.

Baada ya kuhutubia, wanachama wa Chadema vyuoni mkoani Dodoma wameutaka uongozi wa chuo kuondoa bango la CCM lililoko UDOM kwa maelezo kuwa ni kinyume cha Ibara ya 7 ya Sheria ya Vyuo Vikuu ya 2005.

Akisoma risala ya wanafunzi Pasquina Ferdinand mwanafunzi wa  Shahada ya Ualimu  mwaka wa pili, Chuo Kikuu cha St John’s, alisema CCM ina bango ndani ya UDOM kinyume cha sheria ya vyuo vikuu ya 2005, alionyesha kuwa ni sheria inayoihusu Chadema pekee lakini kwa CCM haina tatizo.

“Tunaomba umweleze Waziri Mkuu kama siasa haziruhusiwi vyuoni kwanini basi CCM ina bango UDOM kinyume cha sheria wapewe amri ya kuliondoa kwani UDOM siyo mali ya CCM inajengwa kwa fedha za Watanzania,” alisema.

Akijibu, Mbowe aliwataka wanafunzi wanachama wa Chadema wanaosoma UDOM kumletea taarifa za kunyanyaswa kwa itikadi yao ili azipeleke kwa Waziri Mkuu na awe na ushahidi wa kutosha ili amuulize swali bungeni.

Wakati huo huo, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Tundu Lissu, ametangaza kuwa watatumia nguvu ya umma kupinga kufukuzwa wanafunzi vyuo vikuu.

“Sisi wazazi tunawajibika kuhakikisha kuwa watoto wetu wanasoma kwa kuizuia serikali isiwanyanyase kwa kuwafukuza wakidai haki yao, hili litafanywa kwa njia ya nguvu ya umma ... tukiona wanafunzi wamefukuzwa UDOM umma uingie mitaani kuandamana kama ni Dar es Salaam watu waingie mitaani tuhakikishe kuwa hapatoshi,” alisema Lissu.


 
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Hongera vijana tupo pamoja.