Aliyekuwa mshambulizi matata wa Chelsea Didier Drogba amehamia klabu ya Shanghai Shenhua ya China.
Mwamba huyo ametia kandarasi ya miaka miwili-na-nusu na timu hiyo ya China.
Kujiunga na klabu hicho, kimemfanya awe timu moja na mchezaji mwengine wa Chelsea Nicolas Anelka.
Drogba mwenye umri wa miaka 34 amesema kabla ya kuamua kuhamia China alifikiria kwa makini sana.
"Nilitilia maanani mialiko chungu nzima niliyopata katika kipindi cha wiki chache zilizopita, lakini nafikiri kwa wakati huu kuhamia timu ya Shanghai Shenhua ulikuwa uamuzi mzuri"
Mwamba huyo wa Ivory Coast atakumbukwa kwa bao alilofungia Chelsea walipocheza na Bayern Munich ya Ujerumani. Bao hilo liliifanya Chelsea ijiandikie historia ya kushinda kombe la Klabu bingwa bara Ulaya.
Drogba alijiunga na Chelsea mwaka wa 2004 kutoka Olympic Marseille ya Ufaransa kwa pauni million 24. Alikuwa baadhi ya wachezaji wa kwanza kusajiliwa na Meneja Jose Mourinho alipojiunga na Chelsea.
Akiwa Chelsea kwa kipindi cha miaka minane, Drogba aliisaidia klabu hiyo kushinda kombe la ligi kuu ya Uingereza mara tatu na kombe la FA mara nne.
Mwamba huyo wa Ivory Coast anaondoka Chelsea akiwa ameandikisha historia ya kuifungia timu hiyo jumla ya magoli 157 hivyo kuwa mchezaji nambari nne kwa ufungaji wa magoli katika historia ya Chelsea.
Katika kujiunga kwake na timu hiyo ya Shanghai Shenhua, Drogba anasema jukumu lake la kwanza ni kufanya soka ya China itambulike duniani.
No comments:
Post a Comment