Advertisements

Friday, June 22, 2012

Kiama chawakumba wakurugenzi H'shauri

  Wanane wafukuzwa, watatu wasimamishwa
  11 wapewa karipio, 22 wahamishwa vituo
Inawezekana serikali imeanza kuifanyia kazi ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na kamati za Bunge juu ya kukithiri kwa ubadhirifu kwenye halmashauri nchini, hivyo wakurugenzi wanane wamefutwa kazi, watatu kusimamishwa huku wengine 22 wakihamishwa vituo vya kazi.


Maamuzi hayo makubwa kuwahi kuchukuliwa dhidi ya watendaji wakuu wa Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (Tamisemi) ambayo ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambako kunadaiwa kujaa mchwa wanaokula fedha za umma, yalitangazwa mjini Dodoma na Waziri wa Nchi  Ofisi ya Waziri Mkuu, (Tamisemi), Hawa Ghasia.

Ghasia alisema wakurugenzi hao wanakabiliwa na makosa mbalimbali, ukiwemo ubadhirifu wa fedha za umma.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ghasia alisema pia wamewateua wakurugenzi wapya 14 kuwa wakurugenzi watendaji.

“Wakurugenzi  22 wamehamishwa vituo vyao vya kazi ili kutoa fursa ya kuimarisha utendaji kazi katika halmashauri,” alisema Ghasia aliyekuwa ameongozana na manaibu wawili wa wizara hiyo, Kassim Mjaliwa (Elimu) na Aggrey Mwanri (Tamisemi).

Aidha, alisema wakurugenzi wawili ambao ni Harold Mdando (Kyela) na Rhoda Nsemwa (Bagamoyo) kesi zao bado zipo mahakamani.
Alisema hatua hizo za kinidhamu zimechukuliwa ili kuongeza nidhamu katika mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa wakurugenzi ambao walionekana kutotimiza wajibu wao ipasavyo.

Ghasia alisema maamuzi hayo yalifanyika katika kipindi cha mwaka 2011/2012.

WALIOVULIWA MADARAKA

Aliwataja wakurugenzi waliovuliwa madaraka na kituo (halmashauri) ambacho kosa lilitendeka katika mabano kuwa ni Consolata Kamuhabwa (Karagwe), Ephraim Kalimalwendo (Kilosa) na Elly Mlaki (Babati).

Wengine ni Eustach Temu (Muheza), Jacob Kayange (Ngorongoro), Hamida Kikwega (Chato), Majuto Mbuguyu (Tanga) na Raphael Mbunda (Arusha).

WALIOSIMAMISHWA KAZI

Ghasia aliwataja waliosimamishwa wakati uchunguzi kuhusu tuhuma zao ukiendelea kufanyika na halmashauri lilipotendeka kosa ni Xavier Tiweselekwa (Misungwi), Erica Mussica (Sengerema) na Theonas Nyamhanga (Kishapu).

WALIOPEWA ONYO

Waliopewa onyo na adhabu zingine ni Judetatheus Mboya (Newala), Lameck Masembejo (Masasi), Abdallah Njovu (Tandahimba), Jane Mutagurwa (Shinyanga) na Silvia Siriwa (Sumbawanga).

Wengine waliopewa onyo ni Lewis Kalinjuna (Kigoma), Kelvin Makonda (Bukombe), Alfred Luanda ( Ulanga), Fanuel Senge (Tabora), Beatrice Msomisi (Bahi) na Maurice Sapanjo (Chunya).

WAKURUGENZI WAPYA

Ghasia alisema wakurugenzi wapya walioteuliwa Aprili 24, mwaka huu na halmashauri zao katika mabano ni Jenifer Omollo (Kibaha), Fedelica Myovela (Musoma), Hadija Mauled Makuwani (Tabora), Ibrahimu Matovu (Muheza) na Iddi Mshili (Mtwara).

Wengine ni Julius Madiga (Morogoro), Kiyungi Mohamed Kiyungi (Shinyanga), Lucas Mweri (Nanyumbu), Mariam Mmbaga (Kigoma), Mwamvua Mrindoko (Nachingwea), Pendo Malembeja (Kwimba), Pudensiana Kisaka (Ulanga), Ruben Mfune (Ruangwa) na Tatu Seleman (Kibaha).

WALIOHAMISHWA VITUO

Aliwataja wakurugenzi watendaji walikotoka na wanakohamishwa katika mabano kuwa ni, Elizabeth Katundu (Maswa-Misenyi), Alfred Luanda (Ulanga-Kigoma Ujiji), Robert Kitembo (Mpwapwa-Dodoma), Shaban Ntarambe (Kwimba-Chato), Francis Namaumbo (Masasi-Mafia) na Hilda Lauwo (Ludewa-Maswa).

Ghasia aliwataja wengine waliohamishwa kuwa ni Fanuel Senge (Tabora-Mpwapwa), Upendo Sanga (Meatu-Mbeya), Isaya Mngurumi (Kisarawe-Meatu), Lewis Kalinjuna (Kigoma Ujiji-Korogwe), Dominic Kweka (Kigoma-Babati) na Lameck Masembejo (Korogwe-Kilosa).

Wengine kuwa ni Azimina Mbilinyi (Kibaha-Kilombero), Bosco Ndunguru (Kilolo-Karagwe), Karaine Kuney (Musoma-Ngorongoro), Mohamed Ngwalima (Mtwara-Kilolo), Gladys Dyamvunye (Nanyumbu-Masasi), Eden Munisi (Morogoro-Ludewa), Chrostina Midelo (Korogwe-Iramba), Anna Mwahalende (Moshi-Korogwe), Mathias Mwangu (Ngara-Singida) na Yona Maki (Singida-Kisarawe).

Ghasia bila kuainisha tuhuma au makosa ya kila mkurugenzi aliyesimamishwa ama kuvuliwa madaraka, alisema baadhi yao wameonekana na tuhuma za ubadhirifu huku waliosimamishwa wakisubiri uchunguzi ufanyike.

Kadhalika, alisema wakurugenzi wengine walihusika na uzembe katika nafasi zao za kazi.
Kuhusu halmashauri na majiji ambayo kwa muda mrefu sasa yako chini ya makaimu, alisema wamepeleka majina kwa Rais ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kuwateua.

Alisema wamepeleka majina Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) ambapo wanatarajia hadi kufikia Julai Mosi, mwaka huu watakuwa wameyafanyia upembuzi na kuteua wakurugenzi wapya katika halmashauri hizo.

Kwa upande wa uhamisho wa wakurugenzi hao, Ghasia alisema baadhi yao ni watumishi wazuri, lakini hawakuweza kuwajibika ipasavyo katika halmashauri walizopelekwa.

Akizungumzia kwa nini wasirudishe utaratibu wa zamani wa watu kuomba ukurugenzi utendaji badala ya utaratibu wa sasa wa kuteuliwa, alisema utaratibu wa zamani ulikuwa na changamoto za watu kutoielewa Tamisemi vizuri.

“Ukitaka watu waombe wengine watakuja kutoka sekta binafsi hawatambui kabisa uendeshaji wa Serikali za Mitaa, ni bora uteuzi kwa kuwa wanakuwa wamekulia humu humu ndani,” alisema Ghasia.

Alisema matarajio ya serikali ni wakurugenzi hao kuwajibika katika hamashauri kwa thamani ya fedha kuonekana katika huduma wanazotoa kwa wananchi.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: