Mbunge huyo na Mbunge wa Ukerewe (Chadema), Salvatory Machemli, walikatwa katwa mapanga wakati wakiwa katika harakati za uchaguzi wa udiwani kata ya Kirumba, mwishoni mwa Machi mwaka huu.
Alikuwa akichangia hotuba ya makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa, iliyowasilishwa bungeni Jumatatu wiki hii.
Kiwia alianza kwa kuwashukuru wananchi wa jimbo lake, wabunge Watanzania wote ambao walimwombea na kupata matibabu ambayo kwa msingi alilazimika kupelekwa nchini India.
“Ninatambua ulikuwepo mpango wa muda mrefu wa kutaka kuniua, taarifa nilizipata nikazipuuzia lakini kilichonikuta nilibaini kuwa mpango huo ni wakweli na bado upo,” alisema.
Alisema mabadiliko katika jiji la Mwanza, hususani Ilemela hayawezi kuzuliwa kwa kuondolewa kwa roho ya mtu mmoja peke yake na kwamba hata asipokuwepo dhamira ya wananchi wa jiji hilo bado iko pale pale.
“Waasisi wa taifa hili walitarajia nchi hii itakuwa na viongozi ambao watakuwa na ndoto ya uzalendo, uadilifu na kiongozi bora, mheshimiwa baba wa taifa,” alisema kabla ya kukatishwa na Naibu Spika, Job Ndugai ambaye alimhoji kuwa anauhakika na jambo hilo.
Bila kujibu aliendelea kuwa kama Mtanzania ni lazima asikitishwe na jambo linaloenda nje na haki za Mtanzania na kueleza kuwa anayasema hayo pamoja na kwamba haungi mkono mgomo wa madaktari.
Hata hivyo, alisimama Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ambapo aliomba mwongozo kwa kutumia kanuni ya 68, alisema hakuna sheria ambayo inaruhusu mtu hasa kiongozi kutishiwa.
“Msemaji amesema kuwa anafahamu watu waliohusiaka kufanya jaribio ni wanachama wa CCM wa Ilemela lakini pili anajua na uhakika juu ya taarifa za nia ya kutaka kumjua sasa huyo ji kiongozi na ni mwenzetu na nchi hii inatawaliwa na utawala wa sheria,” alisema na kuongeza kuwa:
“Hakuna sheria inayoruhusu mtu kutisha wala kufanya vitisho hivyo vya kumuuwa tena akiwa mbunge, nimesimama hapa kuomba kiti chako kimuombe mheshimiwa mbunge atoe huo ushahidi wa hao watu wanaotaka kumuuwa ili serikali iweze kumsaidia…moja ya jukumu la serikali ni kulinda raia wake.”
Akijibu, Kiwia alisema pamoja na kwamba atapeleka ushahidi baadaye lakini siku ya tukio gari la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Maria Hewa, lilikuwepo na kwamba hiyo ni dhahiri wa mpango huo.
Ndugai alisema kwa kuwa anahitaji muda ili aweze kupeleka ushahidi, amempa siku saba awe amewasilisha ushahidi huo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment