ANGALIA LIVE NEWS
Saturday, June 16, 2012
Lembeli adaiwa kutishiwa kifo
Neville Meena, Dodoma
MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli anadaiwa kutishiwa kifo na watu wasiofahamika.
Habari ambazo Mwananchi ilizipata mjini Dodoma na kuthibitishwa na Lembeli mwenyewe, zilisema Mbunge huyo wa Kahama (CCM), alitishwa kwa kutumiwa ujumbe kupitia simu yake ya mkononi mara baada mkutano wa saba wa Bunge wa Aprili mwaka huu.
Vitisho vya kifo dhidi ya Lembeli vinahusishwa na uongozi wake katika Kamati ya Bunge ambayo katika mkutano huo uliopita ilitoa taarifa kutokana na uchunguzi uliofanywa na Kamati yake ndogo kuhusu ugawaji wa vitalu vya wanyamapori.
Ripoti hiyo iliwatuhumu baadhi ya watendaji wa juu wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwamba walihusika kwa namna moja au nyingine na kukiuka sheria katika ugawaji vitalu vya uwindaji.
Katika ripoti yake hiyo, Kamati pamoja na mambo mengine ilipendekeza kwamba Bunge liitake Serikali kunyang’anya vitalu kampuni 16 zilizopewa ambazo ilisema hazikuwa na sifa.
Kutokana na ripoti hiyo, aliyekuwa Waziri wa Utalii na Maliasili, Ezekiel Maige aliachwa katika Baraza la Mawaziri lililotangazwa na Rais Jakaya Kikwete Mei mwaka huu.
Kauli ya Lembeli, Polisi
Lembeli akizungumza na gazeti hili jana kwa simu kutoka nchini Brazil alikokwenda kuhudhuria mkutano, alikiri kupokea ujumbe wa vitisho na kwamba tayari ametoa taarifa polisi katika Mkoa wa Shinyanga.
“Samahani nakusikia kwa mbali...ndiyo unachosema ni kweli kwamba nimetishiwa kifo na taarifa hii watafute polisi wa Kahama watakwambia nilisharipoti kuhusu suala hilo, sasa wamefikia wapi katika uchunguzi wao hilo sijui,” alisema Lembeli na kuongeza:
“Mimi nahusisha tukio hili na kazi ya kamati yetu ya Bunge hasa taarifa ya kamati yetu, wapo watu wanapotosha umma kwamba eti ile taarifa kuhusu wizi wa maliasili za nchi ilikuwa ya Lembeli, huu ni upotoshaji. Kazi hiyo ilikuwa ni ya Kamati na haikuwasilishwa bungeni bila kibali cha Spika,” alisema.
Hata hivyo, alisema licha ya vitisho hivyo, ataendelea kufanya kazi yake bila woga na kwamba yuko tayari kwa lolote hata kama ni kifo kuliko kuwasaliti Watanzania kwa maslahi ya watu wachache ambao aliwaita “wasio na huruma kwa wenzao”.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Onesmo Lyanga akizungumza kwa simu na gazeti hili jana alikiri kupokea taarifa za mbunge huyo kutishiwa kifo na kwamba wanaendelea na uchunguzi.
“Tulipokea taarifa hizo ndiyo na kweli tumezifanyia kazi sana, lakini hadi sasa bado tunaendelea na uchunguzi wa suala hili kama unavyofahamu uchunguzi wa mambo haya ya simu ni mgumu sana, maana mtu anaweka laini ya simu anatuma ujumbe halafu anaitoa na kuitupa,”alisema Kamanda Lyanga na kuongeza:
“Kwa hiyo hapo ni kwamba tunamtafuta mtu aliyetuma ujumbe huo wa vitisho, lakini lazima ujue kwamba ni mtu ambaye hatumfahamu kwa jina wala sura. Hata hivyo, tunajitahidi kuhakikisha kwamba mwisho wa siku tunampata muhusika, na akipatikana utaratibu unajulikana kwamba atafikishwa mbele ya sheria”.
Ofisi ya Bunge haina taarifa
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema ofisi yake haijapokea taarifa za mbunge huyo kutishiwa na kwamba ikiwa zitawasilishwa kwake, basi Bunge linawajibika kumlinda kwa mujibu wa Sheria za Haki na Madaraka ya Bunge.
“Pengine liko njiani ila mimi kwangu halijafika, lakini kama kuna mazingira ambayo yanathibitisha kwamba alitishiwa kifo kutokana na kazi zake kama mbunge, basi nasi tunapaswa kuchukua hatua za kiutawala dhidi ya vitisho hivyo wa kuzingatia sheria zilizopo,”alisema Kashililah.
Alikiri kufahamu safari ya Lembeli kwenda kuhudhuria mkutano nchini Brazil na kwamba huenda akatoa taarifa za kutishiwa kifo baada ya kurejea nchini.
Mwanachi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment