ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 20, 2012

Mrwanda anogesha mazoezi Simba

Mshambuliaji wa zamani wa timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars), Danny Mrwanda, juzi jioni alianza rasmi mazoezi na timu yake ya zamani Simba kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya Kombe la Kagame yatakayofanyika kuanzia Julai 14 hadi 29 jijini Dar es Salaam.

Mrwanda amerejea Simba baada ya kumaliza mkataba na klabu yake ya Dong Tam Long An ya Vietnam.

Mchezaji mwingine ambaye alionekana kivutio katika mazoezi ya Simba juzi ni Kigi Makasi ambaye ametua kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu huu akitokea kwa watani zao Yanga.


Meneja wa Simba, Nico Nyagawa, alisema kuwa mazoezi ya timu hiyo yanaendelea vizuri na kuanzia kesho wanatarajia kikosi chao kitakamilika kwani wachezaji waliokuwa Stars watakuwa wameshajiunga tayari kwa maandalizi ya kuelekea Mwanza ambako watacheza mechi za kirafiki.

Nyagawa alisema kuwa wachezaji ambao hawajafika wametoa taarifa.

Wachezaji ambao wanaendelea na mazoezi ni pamoja na Salim Kinje, Abdallah Juma, William Mweta, Hamadi Waziri, Abuu Hashim, Haroun Athumani, Haruna Shamte, Amri Kiemba, Paul Ngalema, Uhuru Suleiman, Patrick Kanu Mbivayanga na Abdallah Seseme.

Mazoezi ya Simba yanaongozwa na kocha wa msaidizi, Mganda Amatre Richard kwa kuwa Mserbia Milovan Cirkovic bado hajarejea nchini kutoka kwao alikoenda likizo.

Cirkovic anatarajiwa kurejea nchini Jumapili na moja kwa moja timu hiyo itaingia kambini kujiandaa na mashindano hayo ya kimataifa yatakayoshirikisha timu za nchi 12.

Wakati huo huo, taarifa kutoka marafiki wa kiungo Salum Machaku zinasema kuwa mchezaji huyo hataki kupelekwa timu nyingine kwa mkopo badala yake anataka aachwe moja kwa moja.

Tayari Simba imemsajili kiungo wa Yanga, Kiggi kuziba nafasi ya Machaku, ambaye kwa sasa anadaiwa kuwa kwenye mazungumzo na Yanga.
CHANZO: NIPASHE

No comments: