ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 11, 2012

Stars yawapa raha Watanzania

Mwandishi Wetu
SHANGWE shangwe kila kona ya Tanzania baada ya timu ya taifa 'Taifa Stars' kuichapa Gambia kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo Stars walilazimika kusawazisha kabla ya kupata ushindi huo muhimu katika harakati zake za kuwania kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.

Beki Shomari Kapombe aliifungia Stars bao la kusawazisha dakika ya 60 akiunganisha kwa tik tak  krosi ya Erasto Nyoni na kufuta lile bao la mapema la Gambia lililofungwa na Momodou Ceesay anayechezea klabu ya MSK Zilina ya Slovakia.


Kama hiyo haitoshi Nyoni aliyecheza kwa umahiri mkubwa alifunga bao la pili lililoipa Stars ushindi kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 85.

Kwa matokeo hayo Tanzania sasa inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu na ikiwa pointi moja nyuma ya vinara Ivory Coast yenye pointi nne baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Morocco inayoshika nafasi ya pili na Gambia inashika mkia ikiwa na pointi  mbili.

Stars ilianza mchezo wa jana kwa kasi na kufika langoni kwa Gambia dakika ya 3 na 5, lakini washambuliaji wake Mrisho Ngasa na John Boko walikosa umakini wa kumalizia krosi nzuri walizotengenezewa na Mbwana Samata na Nyoni.

Gambia walijibu mapigo na kufanya shambulizi la kustukiza na krosi ya upande wa kulia kutoka kwa Ousman Koli anayechezea klabu ya NK Triglav ya Slovenia ilitua kichwani kwa mshambuliaji mrefu Momodou Ceesay aliyefunga kirahisi bao hilo.

Baada ya kufungwa bao hilo wachezaji wa Stars hawakuonekana kukata tamaa ila waliendelea kucheza kwa kujiamini na kugongeana pasi fupi fupi za chini na kuwachanganya kabisa viungo wa Gambia ambao muda wote walionekana kufukuza vivuli vyao.

Wachezaji Chipukizi wa Stars, Frank Domayo na  Abubakar Salum walishirikiana vizuri na Mwinyi Kazimoto katikati ya uwanja katika kupitisha pasi kwa washambuliaji Boko na Samata na Ngasa.

Katika dakika ya 20, Kazimoto nusura aisawazishie Stars baada ya shuti lake kugonga mwamba na kurudi uwanjani na mabeki wa Gambia kuwahi na kuokoa mpira huo.

Kasi ya Ngasa ilionekana kuwapa taabu mabeki warefu wa Gambia na kuamua kuchezea faulo, ambapo katika  dakika 41 walimpasua Ngasa sehemu ya juu ya jicho, lakini alipewa matibabu na kuendelea na mchezo.

Pamoja na Stars kuwa nyuma hadi mapumziko, bado mashabiki waliwashangilia kwa nguvu kutokana na uwezo mkubwa wa kikosi hicho katika kumiliki mpira na kupigiana pasi fupi fupi zilizowachanganya wapinzani wao.

Kipindi cha pili kocha wa Stars alimpumzisha Boko na kumwingiza Haruna Moshi katika dakika ya 54 mabadiliko ambayo yaliongeza hamasa na nguvu katika safu ya ushambuliaji ya Stars.

Stars ilipata bao la kusawazisha baada ya Nyoni kupokea mpira kutoka upande wa kulia na kuingia nao kwa nguvu kabla ya kupiga krosi iliyounganishwa na Kapombe kwa tik tak na kufunga bao la kusawazisha kwa Stars hivyo kuzidisha kelele za mashabiki uwanjani.

Kuingia kwa bao hilo kuliamsha hali ya Stars kuongeza kufanya mashambulizi, ambapo kati dakika ya 74 na 79 mashuti ya Kazimoto na Ngasa yalipanguliwa na kipa na kuwa kona ambazo hazikuzaa matunda.

Wakati mashabiki wakiamini mechi hiyo itamalizika kwa sare nyota wa TP Mazembe, Samata 'Samagol' alichukua mpira upande wa kulia na kumchekecha beki kabla ya kupiga krosi iliyotua mkononi mwa beki Pa Saikou Kujabu anayechezea klabu ya Hibernian ya Scotland na mwamuzi Ruzive Ruzive kutoka Zimbabwe kuamuru penalti iliyofungwa na Nyoni na kuihakikishia Stars pointi tatu muhimu.

Akizungumza baada ya pambano hilo kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen alisema amefurahishwa na jinsi wachezaji walivyocheza kwa kujituma, umakini na kufanikiwa kupata matokeo yaliyosubiriwa na Watanzania kwa muda mrefu.

"Ni vigumu sana unapokuwa umeanza kufungwa nyumbani, lakini nawapongeza wachezaji jinsi walivyoweza kutulia na kuendelea kucheza kama nilivyowaelekeza na kufanikiwa kupata matokeo,"alisema Kim.

Kim alisema,"wachezaji wangu wanaelewa wakati wa mazoezi nilikuwa nikiwapigia makelele sana kwa sababu nafahamu muda wa kujiandaa ni mfupi na inabidi tupate matokeo mazuri, nashikuru baadhi ya mambo wameyatekeleza

"Kwenye kiungo Domayo na Salum 'Sure boy' walicheza vizuri na uwelewano mkubwa, kwa jumla timu yote ilicheza vizuri,"alisema Kim.

Alisema,"unaweza kuona timu yangu iliyocheza katika mechi hii ilikuwa inaundwa na wachezaji wengi wenye umri mdogo."

Kim alisema ushindi huu ni watanzania na mashabiki wote waliojitokeza hapa na kutushangilia kwa nguvu muda wote.

Naye kocha wa timu ya taifa ya Gambia, Luciano Mancini alikipongeza kikosi cha Stars kwa kuibuka na ushindi, lakini alionyesha kutokubaliana na mwamuzi kwa kutoa penalti katika mchezo huo

Stars leo itarejea kambini kujiandaa na mechi  yake ya marudiano dhidi ya Msumbuji jijini Maputo Jumapili ijayo katika mechi ya kusaka tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa Afrika 2013.

Matokeo ya michezo mingine
Lesotho 0-0 Sudan
Msumbuji 0-0 Zimbabwe
Ethiopia 2-0 Jamhuri ya Afrika ya Kati
Rwanda 1-1 Benin
DR Congo 2-0 Togo


Mwananchi

No comments: