ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, June 9, 2012

Waislamu waizidi kete polisi, waandamana


Waipa serikali siku 7
Mmoja wa wafuasi wa Kiislamu
Licha ya Jeshi la Polisi Kanda Maalum mkoa wa Dar es Salaam kuzuia maandamano ya Waislamu jijini Dar es Salaam yasifanyike, jana Waislamu hao walifanya maandamano hayo kiaina na kukutana kwenye viwanja vya Kidongo Chekundu ambako walitoa siku saba kwa serikali kutekeleza matakwa yao.

Walidai kuwa kama matakwa yao hayatashughulikiwa katika kipindi hicho walichotoa wataandamana tena kudai haki itendeke.

Katika matakwa yao wameitaka serikali kuunda tume huru kuchunguza utendaji kazi wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita, Katibu Mkuu Necta, Joyce Ndalichako ajiuzulu, watendaji wakuu wa kitengo cha mitihani na wanaohusika na mfumo wa kompyuta Necta wawajibishwe.


Madai mengine ni hatua za kisheria na kinidhamu zichukuliwe dhidi ya watumishi wa Necta watakaothibitika kuhusika na kashfa ya kuvuruga matokeo ya wanafunzi wa Kiislamu na pia muundo wa Baraza la Mitihani la Taifa uzingatie uwiano wa kidini badala ya hivi sasa ambapo linaongozwa na Wakristo tu.

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Ahmedi Msangi, juzi akizungumza na waandishi wa habari alisema kuwa Jeshi hilo halioni sababu ya kufanyika kwa maandamano hayo na badala yake aliwataka Waislamu kufanya mkutano pekee.

Hata hivyo, mara baada ya kufanikiwa kukusanyika kwenye viwanja hivyo kwa staili ya kiaina, Waislamu hao wametoa wiki moja kwa Serikali kuyapatia ufumbuzi madai yao matano vinginevyo watachukua hatua wanazoona zinafaa ili kuhakikisha madai yao yanapatiwa majibu.

Waislamu hao walianza kuwasili viwanjani hapo kwa staili kuanzia majira ya saa 8:00 mchana ambapo walikuwa wakitembea kwa miguu bila kuweka kundi kubwa na wengine wakitumia magari ya daladala na binafsi kuwasili eneo hilo.

Polisi waliokuwa kwenye magari yenye namba za usajiri PT 1858 na T 671 BEQ  walishindwa kuzuia mkusanyiko huo ambao kwa muda mfupi wa nusu saa uwanja ulijaa hasa kutokana na staili iliyokuwa ikitumika ya watu kujitokeza maeneo mbalimbali tofauti.

Staili hiyo ya maandamano iliwafanya polisi kushindwa kuchukua hatua zozote ambapo waandamanaji hao baada ya kuwasili kwenye viwanja hivyo walikuwa na mabango yaliyokuwa na ujumbe mbalimbali mengi yakiwa ya kulilaumu Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kwamba linahujumu matokeo ya mitihani ya Waislamu.

Baadhi ya mabango hayo yalikuwa na ujumbe kama "Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) acheni udini", "NECTA ilaaniwe",  "NECTA ivunjwe",  "NECTA acheni kufelisha Waislamu", "Ndalichako jiuzulu", "Dhuluma sasa basi",  "Rais Jakaya Kikwete tumechoka kuhujumiwa Waislamu" na "Ndalichako zako sasa zimefika ondoka NECTA".

Mara baada kufanikiwa kukusanyika, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, aliwatangazia Waislamu kwamba kwa kuwa siyo rahisi kwa Waislamu wote kwenye Wizara ya Elimu na Mafunzo kupeleka madai yao, hivyo waliteuliwa watu watatu kuwakilisha .

Walioteuliwa kwenda kuonana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk.Shukuru Kawabwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Kiislamu Tanzania, Shabani Mapeyo, Sheikh Selemani Daudi na Sheikh Nkondo Bungo.

Wawakilishi hao walikwenda makao makuu ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, majira ya saa 8:30 mchana ambapo walipanda gari la polisi T 671 BEQ wakisindikizwa na gari jingine lililokuwa na askari wa Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia (FFU)
.
Wajumbe hao waliokwenda wizarani walirejea kwenye viwanja hivyo majira ya saa 9:13 alasiri, ambapo Selemani Daudi alisoma mambo matano waliyoyawasilisha serikalini ili yapatiwe ufumbuzi.

Daudi alisema baada ya kuwasili makao makuu ya wizara, walipokelewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Selestine Kisimba, ambaye walimkabidhi mambo ambayo wanataka serikali iyafanyie kazi ndani siku saba.
Kwa upande wake Nkondo Bungo alisema serikali isipotekeza madai hayo ndani ya wiki moja wataandamana tena kudai haki itendeke ambapo alimtupia lawama Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk.Kawabwa kwamba ameshindwa kushughulikia madai ya Waislamu dhidi ya Necta.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk.Kawambwa, akizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dar es salaam, alisema serikali inakiri kuwepo kwa makosa wakati wa usahihishaji wa somo la Islamic Knowledge katika mtihani wa taifa wa kidato cha sita ulioofanyika Februari mwaka huu.

Alisema kutokana na makosa hayo serikali itaunda kamati ya wataalam kwa ajili ya kuiwezesha serikali kukabiliana na makosa ya jinsi hiyo yasitokee tena.

 
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

siyo soma la islamic knowledge tu peke yapo mengi kama kuwapendela wakiristo kuenda kusoma masomo ya juu na kuonekana kama wao ndo wenye kuthamini elimu na waislamu kuonekana mabumbubu mzungu wa reli na kitu hicho si kweli kabisa.

Uno uonevu huu tumeaka sasa na bado mizizi ya uonevu ipo mingi na upendeleo halafu sisi tunaonekana kwamba madrasa tu hatusomi elimu ya dunia which is not true

mungu yupo na atatusaida hili na jinginewe amin