ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 30, 2012

BAADHI YA WABUNGE NI WAGANGA NJAA NA WABABAISHAJI


Ndugu Watanzania wenzangu,
Baadhi ya mambo aliyoibua Waziri Muhongo na Katibu Mkuu wake katika Wizara ya nishati ametusaidia kufungua njia na kuelewa u “Ndumila Kuwili” wa Wabunge wetu jinsi walivyo na sura mbili.Nikisema sema hivi nina maana ya kwamba Wabunge hawa wamekuwa wakipiga kelele za UFISADI kwenye Taasisi na Wizara mbali mbali, huku wenyewe ndio wakiwa ndio wakumbatiaji ya mambo ya ki FISADI  yanayofanyika katika taasisi na Wizara hizo.

Aidha wamekuwa wakifaidika kwa kupata marupurupu toka kwa baadhi ya watu wao au ndugu zao wanaofanya biashara na Taasisi au Wizara au wanapatiwa viziba mdomo kutoka kwa Watendaji wa Taasisi au Wizara.
Hapa  napenda kutahadharisha,(bali hizi ni hisia zangu mwenyewe) kwa jinsi Ufisadi huu ulivyoibuliwa katika Wizara ya Nishati inaelekea  kulikuwa na kutoelewana au mgongano wa maslahi baina ya Watendaji/Menejimenti na Bodi na kamati ya Bunge ya Nishati.
Uozo wote ulioanishwa na Mhe Waziri na Katibu wake, ni ukweli kabisa mambo haya yamekuwa yakifanyika muda mrefu lakini kwa kulindana na kukingiana vifua aidha kwa Wabunge wanaofaidika kwa kupata chochote toka kwa watendaji au wajumbe wa bodi nao walikuwa wakifaidika kwa namna Fulani.


Nina hakika kabisa kwa Bw Mhando kumpatia tenda mke wake na kuagiza PAKACHA LA MISUMARI badala ya vipuri kwa dhamani ya $ 50.000.000 toka nje ya nchi, hii ilikuwa dili lilopangwa kwa kuwashirikisha wahusika wote katika wizara,Tanesco, bodi na kamati ya wabunge wa nishati. Tatizo lililojitokeza hapa nadhani mgao haukwenda vizuri kwa wahusika wengine. Hivyo wameamua kumtonya Waziri (lugha ya mjini au kumuuzia dili Waziri).Na Waziri Muhogo bila kusita akayaweka mambo hadharani.
Nimesoma kwa makini hoja za baadhi yaWabunge husika katika kamati ya Nishati jinsi walivyojitetea na kujisafisha ya kwamba hawajahongwa au kufanya biashara na wizara. Ki ukweli kwa sheria zetu za Tanzania itakuwa ni vigumu sana sana kuthibitisha jambo hili.

Nikisema hivyo nina maana unaweza kwenda Tanesco ukaambiwa kampuni yenye tenda ya vipuri inaitwa, Masamaki General Traders na ukifuatilia kwenye kumbukumbu za usajili wa kampuni unakuta mmiliki anaitwa Mr, Tulia bin Unyolewe. Ukimtafuta huyu bwana hutampata aslani kabisa bali utaambiwa kuna tetesi kampuni hii inahusuka na Mbunge Fulani,Waziri Fulani au Mwenyekiti wa Bodi Fulani. Hapo ndio itakuwa umekwama kuthibitisha. Utaanza kukutana na hekaya za ABUNUWASI.

Na pia ukisema ufuatilie kwenye Benki akaunti ili ujue ni nani anasaini kutoa au kuingiza fedha, hata benki watakwambia hawamjui mteja huyu bali wao kazi yao ni kutunza na kuhifadhi fedha za mteja.
Nina hakika katika mabenki kuna Camera sehemu zote, mlangoni, kwa keshia na kwingineko, lakini pia watakwambia akiingia huyu bwana kuweka au kuchukua fedha mitandao inakuwa imezima, hivyo ni vigumu kupata picha yake. Ukifuatilia kwenye kadi ya ufunguzi wa benki akaunti ambayo inawekwa picha yako, utakuta imewekwa picha ya mtoto wa miaka 12.
Huu ndio ubabaishaji uliopo katika nchi yetu ndio maana inakuwa ni vigumu kudhibitisha tuhuma yoyote kwa vigogo na wabunge wababaishaji.

Ndio maana wanajigamba hadharani ya kwamba kama kuna udhibitisho basi utolewe ili sheria ifuate mkondo wake, wana hakika kabisa ya kushinda kwenye tuhuma hizi kwa sababu ya kukosa ushahidi kamilifu.
Napenda kuwaambia Watanzania wenzangu, ufisadi kama huu upo kila kwenye taasisi na wizara zote serikali bali hapajapatika watu makini wenye uchungu na nchi yao kama Muhongo na Katibu wake.
Bali nina hakika Waziri Muhongo na Katibu wake wamefungua njia kwa Watendaji wengine kufuayta nyayo zao ili tuikomboe nchi yetu katika dimbwi la ufisadi.

Hakika kwa sasa tusubiri kusikia mengi yatakayoibuliwa kutokana na sakata hili, kwani mtego umenasa na kila mtu anajitetea kutoka ndani ya mtego.
Waziri Muhongo, keep it up
Mungu Ibariki Tanzania , Mungu ibariki Afrika
ALUTA KONTINUA.

1 comment:

Anonymous said...

Kila kitu kina mwanzo na mwisho wake,mwizi siku zake arobaini,kuna siku Mafisadi wote watakuja kubainika kwa uwezo wa Mola wetu,Maana wananchi tunahangaika na maisha ya kila siku,tunalipa kodi na huduma hatupati,Na baadhi ya viongozi wanakula nchi yetu kiurahisi hivi na kuzidi kuididimiza kimaendeleo,Ubinafsi ni kitu kibaya sana.