ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 30, 2012

Kashfa nyingine yaibuka bungeni *Mbatia adai Kamati ya Maadili imekosa sifa *Awalipua wajumbe wake kuhusika na rushwa

Na Benedict Kaguo, Dodoma

MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Bw. James Mbatia, amekosoa uadilifu wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge iliyopewa jukumu la kuwachunguza wabunge waliohusika na kashfa za rushwa katika Wizara ya Nishati na Madini na kutaka wajumbe wa kamati hiyo, wajitakase kwanza kabla hawajaanza kazi hiyo kwani baadhi yao wananuka rushwa.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Bw. Mbatia alisema licha ya Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda, kuagiza kamati hiyo kuwachunguza wabunge hao, bado itashindwa kutenda haki kwani miongoni mwa wajumbe wake wanatuhumiwa kwa rushwa.

Alisema mbali ya Bi. Makinda kuvunja kamati ya Nishati na Madini, kuna kamati nyingine sita za Bunge ambazo zinakabiliwa na kashfa ya rushwa vivyo Spika anapaswa kutangaza kuzivunja kwenye kipindi cha wiki moja.

“Miongoni mwa kamati hizi ni pamoja na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ambayo inaongozwa na Bw Augustino Mrema, chama changu kinatoa muda wa wiki moja kwa Bi. Makinda awe amewataja kwa majina wabunge wote wanaotuhumiwa kwa rushwa.

“Kimsingi wabunge hawa wanafahamika na asipofanya hivyo, tutachukua uamuzi wa kupeleka hoja binafsi ndani ya Bunge ili lichukue uamuzi wa kuwafukuza ubunge na kuwapeleka mahakamani kwa kutumia Sheria namba 3 ya Bunge ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2002,” alisema Bw. Mbatia.


Alisema wabunge wa Chama hicho wote ni wasafi hakuna anayehusika na tuhuma hizo na kwamba kama ikithibitika basi wachukuliwe hatua zinazostahili za kufukuzwa.


Alisema kwa sheria kama hiyo tayari Bunge la Uingereza limeshawahi kufanya maamuzi 59 ya kuwafukuza wabunge wake walituhumiwa kwa rushwa huku bunge la India nalo likichukua maamuzi ya kuwafukuza wabunge 11 kwa rushwa mwaka 2005.

Hata hivyo, Bw. Mbatia alisema mwaka 2004 wabunge wanane wa CUF ambao walihusika na kashfa ya kuwasaidia raia wa Somaria kupata hati za kusafiria na kudai ni wake zao, walifukuzwa na kupelekwa mahakamani ambapo chama hicho kiliwafuta wabunge hao uanachama na kujitakasa kwa kashfa hiyo.

Bw. Mbatia aliwataka wabunge wote wote wanaotuhumiwa kwa rushwa, kujiondoa katika kamati zao wenyewe na vyama vyao vichukue jukumu la kuwafukuza uanachama ili kujisafisha.

“Ili Bunge letu liwe takatifu, wabunge wala rushwa watajwe na wafukuzwe kwani wamelitia najisi Bunge na kuliondolea hadhi ya kuitwa Bunge takatifu,” alisema Bw. Mbatia.

Katika mkutano huo, Bw. Mbatia aliambatana wabunge wa chama hicho Bw. Moses Machali (Kasulu Mjini) na Agripina Buyegera (Kasulu Vijijini) ambao wote walitaka hatua za haraka zichukuliwe kuliondoa Bunge kwenye kashfa nzito za rushwa.


Majira

No comments: