Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Tanzania bara, Bw, Julius Mtatiro, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana, kuhusu wabunge wa vyama vya CCM na CHADEMA wanaotuhumiwa kupokea rushwa kushindwa kuwajibika. (Picha na Peter Mwenda)
Na Peter MwendaCHAMA cha Wananchi (CUF), kimetoa tamko la kuutaka uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), utamke kuwavua madaraka ya ubunge wabunge wote wa vyama hivyo waliotuhumiwa kuhusishwa na vitendo vya rushwa.
Alisema baadhi ya wabunge wa vyama hivyo, wanatuhumiwa kuchukua rushwa kutoka kwa kampuni za mafuta ili wajenge hoja ambazo zitawaondoa madarakani Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu Bw. Eliakim Maswi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Bw. Julius Mtatiro, alisema CUF kimehuzunishwa na taarifa za wabunge hao ambao kimsingi kuwa kinara wa kupinga rushwa kwenye jamii.
Alisema ukimya wa vyama vivyo kutotoa tamko lolote juu ya wabunge wao, unaonesha baadhi ya Mawaziri, wabunge pamoja na viongozi wa juu, wanamasilahi katika kiwanda, kampuni mbalimbali na idara ambazo zinavurunda lakini hazichukuliwi hatua.
Akiwasafisha wabunge wa CUF, Bw. Mtatiro alisema hawana kashfa yoyote ya rushwa kama ilivyo kwa wabunge wa CCM na CHADEMA.
“Hivi karibuni Meli ya Mv. Skagit ilizama ambapo Waziri ambaye hakuhusika kuinunua, amelazimika kujiuzulu, sasa umefika wakati wa vyama hivi kujisafisha kwa tuhuma ambazo zinazowakabili wabunge wake kwa kujisafisha,” alisema Bw. Mtatiro.
Katika hatua nyingine, CUF kimeitaka Serikali kuongeza muda wa wananchi kujiandikisha kwenye mchakato wa kupata vitambulisho vya Taifa kwani mfumo unaotumika sasa, unawanyima nafasi wanachama wa vyama vingine vya siasa nje ya CCM.
Alisema Serikali na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), wameandaa mfumo wa kuwalazimisha mabalozi ya mashina wa CCM, kujenga mazingira ya rushwa.
“Asilimia 90 ya viongozi wa Serikali za Mitaa ni CCM na ndio waliopewa jukumu la kutoa barua za utambulisho hivyo kulazimisha rushwa ya waziwazi,” alisema.
Bw. Mtatiro aliongeza kuwa, vitambulisho vya Taifa ni haki ya kikatiba ya kila Mtanzania hivyo wananchi wanapotakiwa kutoa fedha ili kupata haki hiyo ni kulazimisha rushwa hivyo kusababisha mchakato huo kuwa na mizingwe.
“Wananchi wanafika Ofisi za Serikali za Mitaa saa 12 asubuhi lakini watoa fomu na waandikishaji wanafika saa tatu, kutokana na wingi wa watu wanatumia siku nzima kuandikisha,” alisema.
Alisema Sheria Mpya ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii mwaka 2012, inayomtaka mfanyakazi aliyejitoa kazini atimize miaka 55 hadi 60 ndipo aweze kupata mafao yake ni kandamizi.
Alisema kutokana na hali hiyo, CUF inapinga vikali sheria hiyo ambayo ni mbovu na haiwasaidii wahusika bali mfanyakazi anastahili kupewa mafao yake anapoacha kazi au kustaafu.
Majira
No comments:
Post a Comment