MDAU wa safu hii, leo naendelea kuwadodosea tabia ya mapenzi bandia inayofanywa na watu bila kujua kama penzi la dhati hujitengeneza lenyewe. Hebu tuungane tena...
Mapenzi si kumuona mtu barabarani akakuvutia basi ukajiaminisha kuwa huyo anakufaa. Mwenzi wa maisha yako ni lazima akidhi vigezo vingi. Wapo ambao utalazimika kuwaacha barabarani wakirandaranda na dunia, halafu yupo mmoja mahususi anayekufaa kwa hali zote kuwa mwandani wako.
Mada hii ikupe tafsiri kwamba siku za mwanzoni za uhusiano wako, inafaa utulize kichwa, ujadili mwenendo wa mwenzi wako kama anakufaa au la! Uzuri wa umbo na sura yake, visikufanye uwe kipofu ukasahau kilicho na faida kwa maisha yako ya leo na kesho. Tazama faida zaidi.
Unapoangalia tafsiri ya mwenzi wa maisha yako katika kipengele cha bahati, ni vizuri ukaweka kando hisia za kuridhishwa kitandani. Ufundi wake wa kukufanya usahau matatizo yako yote pindi mnapokutana faragha, si lolote endapo hatakuwa na sifa za kutimiza matarajio yako ya kimaisha.
Mwenzi wa maisha yako haendani na harufu yake. Kwamba ukiwa naye unajisikia mtulivu kiasi gani, la hasha! Kinachobeba uzito ni kiasi gani huyo uliyenaye anavyokupunguzia mzigo wa maisha yako. Je, mtindo wa maisha yake, haukupi mzigo wa moyo? Kama jibu ni ndiyo, basi iwe heri.
Wengine hutafsiri kwamba mwenzi wa maisha yako utamtambua kwa namna ambavyo anakufanya ujisikie hamu ya tendo mara kwa mara hata baada ya kutoka naye faragha muda mfupi uliopita. Mtazamo huu nao ni potofu, badala yake jiulize tena, je, mwenzi wako anakufanya ujihisi mtulivu?
Je, anakufanya ujione ni mwenye furaha? Nazungumzia furaha ambayo inakuja yenyewe, siyo ile ya kulazimisha. Mwenzi sahihi kwako kwa zaidi ya asilimia 99, anapaswa kuongeza kitu chanya kwenye maisha yako. Endapo ukijitazama unajikuta unazidi kupotea badala ya kusafiri kwenye mstari ulionyooka, hapo unazidi kupotea.
Yatazame maisha yako kabla hujakutana naye, halafu jiulize mabadiliko yako. Je, ni hasi au chanya? Inawezekana kweli ameyafanya maisha yako kuwa na furaha lakini hiyo furaha anaidumisha vipi? Isije ikawa anakufurahisha pale tu anapokuwa na shida zake, pindi unapomtatulia huyo anakwenda zake, akirudi tena ujue ana shida.
Mathalan, mwenzi wako anatimiza kila kitu unachohitaji. Anageuka mtu wa ndiyo na kutekeleza kila ombi lako. Wewe unajiona unatisha kwa kuona kwamba mwenzi wako anakunyenyekea unavyotaka. Kumbe mwenzako ana malengo yake, mkishaingia faragha na kukidhi haja zake, ule unyenyekevu wake wote unaondoka, anarudi kuwa yuleyule.
Mwenzi wako ana asili ya kiburi, mara nyingi ombi lako la kukutana naye faragha hulitolea nje kwa maelezo kwamba eti huwa hajisikii. Lakini anapokuwa na shida ya fedha, anakuwa mpole, kiburi chake chote kinapotea. Hakawii kukwambia ana hamu na wewe. Akili ikae kichwani kwako.
Mfano: Msomaji wangu ambaye naomba nimtaje kwa jina moja la Bryson, aliwahi kunilalamikia kwa njia ya simu, kuhusu tabia ya mke wake.
Itaendelea wiki ijayo.
www.globalpublishers.info.
No comments:
Post a Comment