Mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe (CUF) na Naibu katibu Mkuu wa Chama hicho, Ismail Jussa Ladhu.
Posho za vikao, viburudisho, ununuzi wa vifaa, mafunzo ya ndani na nje yameiweka katika wakati mgumu Bajeti ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora baada ya kukosekana maelezo ya kina juu ya matumizi yake.
Wakichagia Bajeti ya Wizara hiyo Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi (BLW), jana walisema kwamba mafungu ya fedha yaliyopangwa kutumika kulipa posho na viburudisho yanatisha katika mwaka huu wa fedha.
Akichangia Bajeti hiyo Mwakilishi (CCM), Panya Ali Abdalla, alisema bajeti hiyo imejaa vifungu vingi kwa ajili ya malipo ya posho na viburudisho kwa watendaji wa serikali badala ya kuangalia mambo ya msingi ya maendeleo.
Alisema kwamba utamaduni wa kupanga fedha nyingi za umma kwa matumizi ya kulipana posho watendaji umeanza kuwa wa kawaida na kuibebesha mzigo mkubwa serikali.
Mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe (CUF) na Naibu katibu Mkuu wa Chama hicho, Ismail Jussa Ladhu, alisema kwamba bajeti ya wizara hiyo ina ongezeko kubwa la matumizi katika vifungu bila ya kuwepo kwa maelezo ya kina juu ya matumizi yake.
Alisema hatakuwa mgumu kupitisha vifungu visivyokuwa na maelezo ya kina juu ya matumizi yake ikiwemo fedha zilizopangwa kwa matumizi ya viburudisho, posho, mafunzo ya ndani na nje, safari gharama za kukodisha kumbi za mikutano na manunuzi ya Televisheni kutokana na maeneo hayo kupangiwa kiwango kikubwa cha fedha matumizi ya fedha za umma mwaka huu.
Jussa alisema mkwamba wizara hiyo imepanga kutumia Sh. milioni 186.8 kwa ajili ya kukodi kumbi za mikutano wakati mamlaka ya kuzuia rushwa na kupambana na uhujumu ikiwa imetengewa kiwango kidogo cha fedha wakati mamlaka hiyo ndiyo inaanzishwa mwaka huu.
Kwa mujibu wa bajeti ya Wizara hiyo Mamlaka hiyo imetengewa Sh. milioni 220.9 kwa ajili ya matumizi ya kazi za kawaida katika mwaka wa fedha 2012/2013.
Wajumbe wengine waliochangia Bajeti hiyo kwa hoja nzito Jaku Hashim Ayob (Muyuni) Hamaza Hassan Juma, (Kwamtipura) Ali Omar Shehe, (Chakechake) Abdalla Juma Abdalla, (Chonga) ambao walisisitiza umuhimu wa serikali kuzingatia vipaumbele katika mipango yake ya maendeleo kila mwaka.
Hamza alisema kwamba mafunzo waliyopata juu ya kuhoji na kuchabua bajeti za serikali yaliyofadhiliwa na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa, (UNDP), yamewasaiduia kwa kiwango kikubwa kufichua mapungufu ya bajeti za serikali mwaka huu.
Mwakilishi wa Jaku Hashim Ayoub, alisema kwamba madhara ya kupanga bajeti ndogo kwa Mamlaka ya kupambana na rushwa ni makubwa kwa vile ni mwanzo wa kutengeneza chombo cha kudai rushwa badala ya kupinga vita rushwa.
Alisema kwamba mazingira ya kazi ya wafanyakazi wa Mamlaka hiyo na maslahi yao lazima yawe mazuri ili kuwaepusha kushawishika na vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa kero kubwa kwa wananchi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment