ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 7, 2012

Wabunge CCM wataka Rais ahojiwe bungeni


Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda


Hali ya kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inatazamiwa kukumbwa na mtikisiko kutokana na kuwepo nia ya kumtaka Rais Jakaya Kikwete, ahojiwe bungeni.
Taarifa za ndani zilizolifikia NIPASHE  Jumamosi zinaeleza kuwa, hatua hiyo inatarajiwa kufanikishwa kupitia mabadiliko ya kanuni yatakayoamuru Rais wa nchi kuhojiwa na Bunge kupitia maswali ya papo kwa hapo, badala ya Waziri Mkuu kama ilivyo sasa.
Wachunguzi wa mambo ya siasa wanaielezea hali hiyo kuwa huenda ikakumbwa na mtikisiko na malumbano ya kisheria kati ya makundi yanayounga mkono mfumo uliopo sasa na wale wanaomtaka Rais aulizwe maswali.
Hadi kufikia sasa, imebainika kuwa hoja hiyo inatarajiwa kuwasilishwa na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ritta Enespher Kabati.

Kabati amethibitisha azma hiyo lakini akapinga kwamba inatokana na shinikizo la kundi moja kati ya yanayopingana ndani ya CCM.
“Mimi sina haja ya kupata shinikizo lolote, nina akili na uwezo wangu, ninatambua kwamba ninawatumikia wananchi wa Iringa hasa wanawake,” alisema katika mahojiano yake na NIPASHE Jumamosi.

Kabati alisema nia ya kuwasilisha hoja hiyo inatokana na uchunguzi aliowahi kuufanya kwa nyakati tofauti na kubaini kwamba asili ya kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu ni Bunge la Uingereza ambapo Waziri Mkuu ana mamlaka ya kuwa Mtendaji Mkuu wa serikali, tofauti na ilivyo hapa nchini.
“Ninavyouona mfumo huu, tunahitaji kufanya marekebisho ili badala ya Waziri Mkuu kuulizwa maswali ya papo kwa hapo, awe anakuja Rais wa nchi,” alisema.
Kabati alisema mfumo uliopo sasa ambapo Waziri Mkuu anashindwa kutoa majawabu ya baadhi ya hoja za wabunge anazoulizwa, isipokuwa kuelekeza kwenye mamlaka ya Rais, kunatoa fursa ya kufanya mabadiliko hayo.
“Kama unavyolifuatilia Bunge kuna wakati Waziri Mkuu anatoa majawabu yasiyowaridhisha wabunge, inafikia wakati anaonekana anadanganya na hata kufikia hatua ya kudhalilishwa kama ilivyowahi kutokea wakati  Godless Lema alipokuwa Mbunge wa Arusha Mjini.
Lema aliwahi kuliambia Bunge kuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alilidanganya Bunge wakati akitoa majibu kuhusu mgogoro uliosababisha mauaji ya raia mjini Arusha, hali iliyosababisha kiti cha Spika kumpa siku saba kuthibitisha kabla ya kutolewa mwongozo.
Hadi kufikia sasa, gazeti hili halijapata kumbukumbu zinazoonyesha kuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda ama wasaidizi wake walishatoa bungeni utetezi wa Lema kuhusu hoja hiyo.
“Kwa hiyo ninaona kwamba kama Rais atakuwa anakuja kujibu maswali kila Alhamis, itasaidia kupunguza mkanganyiko na wakati mwingine kumfanya aonekane anadanganya,” Kabati alisema.   
Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia NIPASHE Jumamosi, baadhi ya wabunge wa CCM wanaamini kuwa kukosekana kwa majibu ya uhakika na yale yanayotofautiana miongoni mwa mawaziri wa serikali hususani Waziri Mkuu, kunasababishwa na kukosekana kwa Rais kujibu hoja za wabunge kwa niaba ya serikali yake.
Kabati alisema hivi sasa anaendelea na maandalizi ya hoja hiyo, akitarajia kuwashirikisha wanasheria na kutafuta kuungwa mkono na wabunge bila kujali tofauti za kiitikadi.
Waziri wa Uchukuzi ambaye kitaaluma ni Mwanasheria, Dk Harrison Mwakyembe, alisema hoja hiyo iliwahi kutolewa na Kabati, lakini kinachoonekana ni upungufu katika kuitafsiri Katiba ya nchi.
Dk Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela(CCM) mkoani Mbeya, alisema kimsingi, Rais anagawana mamlaka ya utawala na Waziri Mkuu, ambapo pamoja na mambo mengine, (Waziri Mkuu) anakuwa Kiongozi wa shughuli za kiserikali.
Pia Dk. Mwakyembe alisema mfumo unaotumika nchini upo kwa mujibu wa mfumo wa mabunge ya nchi za Jumuiya ya Madola ambayo Tanzania ni mwanachama wake.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, ibara za 52, 53 na 57 zinatoa uhalali wa Waziri Mkuu kuwa na mamlaka ya kiutendaji yenye hadhi sawa na Rais, hivyo kustahili jukumu la kuendelea kujibu maswali ya papo kwa hapo bungeni.
Ikiwa hoja binafsi ya Kabati itawasilishwa kwenye kikao cha Kamati ya Wabunge wa CCM na hatimaye bungeni, inatabiriwa na wachunguzi wa mambo ya siasa kwamba inaweza kuibua mjadala na kuzidisha mgawanyiko wa kifikra ndani ya chama hicho.

KATIBA MPYA

Wakati huo huo, Dk Mwakyembe alisema pamoja na mchakato wa kuandikwa Katiba Mpya, taifa linapaswa kurejea katika hali ya uwajibikaji utakaochochea tija kwa maendeleo ya nchi na ustawi wa wananchi.

Alisema upatikanaji wa huduma muhimu za jamii kwa wananchi ni moja ya nyenzo muhimu zinazochochea nchi zilizoendelea, zikiwa na Katiba mbovu kuliko ya Tanzania, lakini zinakubalika pasipo kuwepo shinikizo la mabadiliko.
“Kama watu wanapata huduma kama za afya, maji safi na salama, elimu bora na nyinginezo kupewa kipaumbele, hakuna raia atakefikiria kudai Katiba, kwa maana mfumo unaoistawisha jamii ukifanya kazi, matatizo yote yanaondoka,” alisema.
Alitoa mfano kuwa Katiba ya Marekani inatoa fursa kwa raia kuwachagua wawakilishi wanaoshiriki kumchagua Rais wa taifa hilo kubwa kiuchumi na kijeshi, lakini hakuna vuguvugu la mabadiliko yake (Katiba) kwa vile mfumo endelevu wa upatikanaji huduma za jamii unawanufaisha raia wake.
Hata hivyo, alisema nia nzuri ya Rais Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba inapaswa kuungwa mkono na kuihamasisha jamii ishiriki kutoa maoni yao.
Dk Mwakyembe alisema maoni yanayopaswa kutolewa kwenye tume hiyo hayahusiani na uelewa wa Katiba, bali wananchi wayaelekeza mahitaji yao yanayostahili kutatuliwa kwa mujibu wa Katiba.
CHANZO: NIPASHE

No comments: