CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimempa siku saba Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa (CCM), Nape Nnauye akiombe radhi au wampeleke
mahakamani kwa kusema uongo kuwa chama hicho kimekuwa kikiwachangisha
fedha wananchi huku kikipokea mabilioni ya fedha kutoka kwa wafadhili
nje ya nchi.
Chama hicho kimesema kuwa kama kitampeleka
mahakamani atatakiwa kulipa fidia ya Sh3 bilioni kama fidia ya
kukifedhehesha kwa tuhuma alizozitoa.
Agosti 11, mwaka huu jijini
Dar es Salaam Chadema ilifanya harambee ya kuchangia chama hicho ili
kununulia magari na helkopta kwa ajili ya shughuli za chama na
kushirikisha wanachama na wafuasi wa chama ambao walikichangia zaidi ya
Sh270 milioni.
Siku moja baada ya harambee hiyo, Nnauye aliitisha
mkutano wa waaandishi wa habari na kusema, CCM imeshangazwa kuona
Chadema ikiwahadaa Watanzania kufanya haramee ili kuhalalisha fedha
walizonazo kutoka kwa wafadhili.
“Chama Cha Mapinduzi
kimeshangazwa na kusikitishwa sana na usanii mkubwa unaofanywa na
Chadema kwa kuwahadaa Watanzania kwa usanii wa kufanya harambee
kuhalalisha uwepo wa mabilioni waliyopewa na wafadhili wao wa nje ya
nchi,” alisema Nape.
Hata hivyo, jana Nnauye alipotafutwa kutolea ufafanua kama amepokea barua hiyo ya Chadema alisema atatoa majibu leo.
“Andikeni
kwanza mlichonacho then (kisha) mie kesho (leo) nitawajibu Chadema,”
alisema Nnauye katika ujumbe wa simu wa maandishi.
Mkurugenzi wa
Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam jana alisema chama kimeanza kuchukua hatua
za kisheria dhidi ya msemaji huyo wa CCM kwa ‘madai ya uzushi na uongo’
aliyoyatoa Agosti 12, mwaka huu.
Mnyika ambaye pia ni Mbuge wa
Ubungo, alisema Bodi ya Wadhamini wa Chadema iliagiza wanasheria
wamwandikie barua Nnauye kumtaka kukiomba radhi chama hicho kwa kutumia
njia ile ile aliyotumia kufanya ‘propaganda chafu za kukikashifu kwa
umma wa Watanzania’.
“Tayari chama kimemwandikia barua ya
kisheria Nape tangu Agosti 24 mwaka huu ya kumtaka aombe radhi na kulipa
fidia ya Sh 3 bilioni kwani uongo ni gharama” alisema Mnyika na
kuongeza;
"Nape kusema kuwa upo uwezekano wa Chadema kupewa fedha
hizo kwa mikataba yenye masharti ya kuiweka nchi rehani ni propaganda
ya kukichafua chama kwa wananchi wake," Alisema Mnyika
Mnyika
alisema matamshi yake yalitangazwa na vyombo vya habari vya kielekroniki
ikiwemo vituo vya television, redio na kusambazwa kwenye mitandao ya
kijamii hivyo inambidi kutuomba radhi kwa njia ile ile aliyoitumia
kututuhumu.
“Kama atashindwa kutekeleza yote mawili kwa siku saba
tulizompatia basi tutafuata sheria ikiwemo kumfikisha Mahakama Kuu ili
aweze kuchukuliwa hatua zaidi,” alisema na kuongeza;
"Kipaumbele
cha Chadema katika suala hili ni kuombwa radhi, hata hivyo kiwango cha
fidia ya fedha kwa fedheha kilichotakiwa ni fundisho kuwa uzushi na
uongo unagharimu."
Mnyika ametoa wito kwa Mwenyekiti wa CCM
ambaye ni Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete kueleza Watanzania iwapo
propaganda hizo chafu zina baraka zake kwa kuwa hakuna alichosema mpaka
sasa.
No comments:
Post a Comment