Advertisements

Friday, August 31, 2012

Jaji Mkuu: Nimekasirishwa

Jaji Kiongozi, Fakihi Jundu
  Ni majaji kutuhumiwa kwa upendeleo
  Asema uteuzi wake umefuata sheria
Jaji Kiongozi, Fakihi Jundu, amesema amesikitishwa na kitendo cha majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kutuhumiwa bungeni, kwa kuwa hawana nafasi ya kwenda kwenye chombo hicho kujitetea.

Miongoni mwa tuhuma zinazodaiwa kutolewa bungeni na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, dhidi ya majaji hao, ni pamoja na iliyomhusu yeye mwenyewe (Jaji Jundu) ya kuendelea kuwa kwenye kiti hicho kwa kutumia mkataba bandia.



Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) na Mnadhimu Mkuu wa Kambi hiyo, alitoa tuhuma hizo wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kuhusu hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria iliyowasilishwa na Waziri wa wizara hiyo, Mathias Chikawe.

Akizungumza baada ya kumuapisha Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, John Kahyoza, kushika wadhifa huo jana, Jaji Jundu alisema yuko katika nafasi hiyo kwa mujibu wa sheria.

Alisema Rais ana mamlaka ya kuwaongezea muda majaji baada ya wao wenyewe kukubali.

“Taarifa iliyotolewa bungeni kuhusu majaji, imenisikitisha sana. Kwa sababu hatuna nafasi ya kwenda kujitetea. Na kuhusu mimi kuendelea kuwa kwenye kiti hiki kwa mkataba bandia ni suala la uzushi, ambalo halina ukweli,” alisema Jaji Jundu na kuongeza:

“Vyombo vya habari vilivyoandika taarifa hiyo, waanike huo mkataba niliosaini kuendelea kuwa na wadhifa huu.”

Hata hivyo, alisema Mahakama ya Tanzania haiwezi kufanya mabishano ambayo hayana msingi kwa kuwa yote yaliyozungumzwa yamesikilizwa upande mmoja.

Tuhuma hizo zinazodaiwa kutolewa na Lissu dhidi ya majaji wanane wa Mahakama Kuu, mmoja wao akiwa ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania pamoja na Jaji Jundu.

Baadhi ya majaji wanatuhumiwa kuteuliwa wakiwa wamekaribia muda wao wa kustaafu kwingineko katika utumishi wa umma na wanapewa ‘zawadi’ ya ujaji ili kuwawezesha kupata mafao ya majaji wastaafu, ambayo yameboreshwa sana katika miaka ya karibuni.

Wengine wanatuhumiwa kuteuliwa huku wakiwa wagonjwa mahututi, ambapo inadaiwa kuwa hawakuwahi kuandika hukumu hata moja kabla ya mauti kuwafika.

Majaji wengine wanatuhumiwa kwa kutoandika hukumu na hivyo kuwa wacheleweshaji wakubwa wa kesi katika Mahakama Kuu na wengine kwa kupewa mkataba mpya baada ya kustaafu kama Jaji wa mahakama hiyo.

Majaji wengine wanatuhumiwa kwa “kushinikiza au kushawishi kushughulikia au kuamua kwa upendeleo mashauri yaliyowahusu jamaa au rafiki zao na kuwaandalia sababu za rufaa baadhi ya washitakiwa waliotiwa hatiani na mahakama za mahakimu.

Julai 13, 2012 Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliwasilisha maoni yake kuhusu Mpango na Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Pamoja na mambo mengine,  yalihusu utaratibu wa uteuzi wa majaji wa Mahakama ya Tanzania.

Maoni ya Kambi yalizua mjadala mkubwa ndani na nje ya Bunge huku wachangiaji wengi wakimtuhumu Msemaji wa Kambi kwa “kuidhalilisha” Mahakama na “kuwadhalilisha majaji” (Gosbert Blandes-Karagwe CCM); “kuwavunjia heshima majaji” (Naibu Spika Job Ndugai); kuwatukana na kuwadhalilisha majaji (Murtaza Mangungu-Kilwa Kaskazini); “kuwa-offend, kuwadhalilisha na kuwanyanyasa majaji” (Assumpter Mshama-Nkenge CCM); “kufedhehesha Mahakama na majaji” (Mwanasheria Mkuu wa Serikali Frederick Werema).

Aidha, Msemaji wa Kambi ya Upinzani alishambuliwa kwa kudaiwa kuwa mfitini na asiye na akili timamu (Muhammad Chomboh- Magomeni CCM)); na “kujiamini kwamba yeye anajua zaidi kuliko watu wengine wote” (Mangungu).

Kwa upande wake, Waziri Chikawe alilihakikishia Bunge kwamba “... haijatokea hata siku moja katika nchi hii Rais akamteua Jaji wa Mahakama Kuu bila kuzingatia mapendekezo yaliyopelekwa kwake na Tume ya Uajiri wa Mahakama. Zaidi ya hayo labda Mheshimiwa Lissu anamjua Jaji angalau mmoja na anaweza akamtaja aseme Jaji huyu ametolewa tu mitaani na Mheshimiwa Rais, yupi hakuna… hawa majaji wote walioteuliwa wamepitia mchakato huu wa kikao kizito sana cha watu ambao ndiyo wenye sheria ya nchi hii.”

Baadaye Msemaji wa Kambi alitakiwa kufuta kauli yake kuhusu uteuzi wa majaji usiofuata utaratibu uliowekwa na Katiba.

Lissu alikataa kufuta kauli hiyo na Mwenyekiti wa kikao alielekeza Msemaji wa Kambi apelekwe kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa hatua zaidi.

Alichukua uamuzi huo ili masuala hayo yapatiwe ufafanuzi ili wananchi wapate picha kamili na ya kweli kuhusu jambo hilo.

Hata hivyo taarifa zilizovuja kutoka kwenye kamati hiyo zilieleza kile alichowasilisha Lissu kuwa ni kufafanua tuhuma moja baada ya nyingine na kuwataja majaji hao kwa majina na walivyoteuliwa au kushindwa kuwajibika kwa mujibu wa viapo vya kazi yao.
 
Katika maelezo yake kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Lissu alisema, “Nitajitahidi kwa kadri inavyowezekana kutoa ushahidi unaothibitisha kwamba siyo tu kwamba utaratibu wa kikatiba katika uteuzi wa majaji umekiukwa mara nyingi, bali pia majaji wengi walioteuliwa kwa utaratibu wa nje ya Katiba wamekuwa hawana ‘uwezo, ujuzi na kwa kila hali hawakufaa kukabidhiwa madaraka ya Jaji wa Mahakama Kuu.”

Ripoti ya kamati hiyo hajawekwa hadharani, ingawa kuna hisia kwamba utetezi wa Lissu siyo tu umefungua mambo mapya bali umewafanya waliokuwa wanamkejeli na kupuuza kuanza kuwaza mara mbili juu ya misimamo yao ya awali.
CHANZO: NIPASHE

No comments: